Fumanizi la wapenzi lasababisha kifo
Muktasari:
- Polisi mkoani Morogoro inamshikilia Salipina Thomas (21) mkazi wa kijiji cha Kiroka kwa tuhuma za mauaji ya Rashid Maharangande (20) aliyefumaniwa akiwa ndani ya chumba cha mwanamke huyo, huku anayedaiwa kuwafumania akitoweka kusikojulikana.
Morogoro. Polisi mkoani Morogoro inamshikilia Salipina Thomas (21) mkazi wa kijiji cha Kiroka kwa tuhuma za mauaji ya Rashid Maharangande (20) aliyefumaniwa akiwa ndani ya chumba cha mwanamke huyo, huku anayedaiwa kuwafumania akitoweka kusikojulikana.
Akizungumza mjini Morogoro leo Jumamosi Septemba 17, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Fortunatus Musilimu amesema mauaji hayo yametokea saa 8 usiku wa kuamkia Septemba 16, 2022 katika kitongoji cha Temekero tarafa ya Mkuyuni wilayani Morogoro.
Amesema mauaji hayo yanahusishwa na wivu wa kimapenzi ambapo kijana aitwaye Richard Stephen Chanzila (23) mkazi wa Kitongoji cha Maembe, Kijiji cha Kiloka ndiye anatuhumiwa kutekeleza mauaji hayo, baada ya kumkuta Maharagande akiwa amelala kwa Salpina ambaye ni mzazi mwenzake.
Kamanda Musilimu amesema, mtuhumiwa huyo inadaiwa alimkata na kitu chenye ncha kali shingoni kijana Mahalagande (20), mkazi wa Sultan Area, aliyekuwa dereva wa bodaboda.
Kamanda Musilimu amesema baada ya Maharagande kukatwa na kitu chenye ncha kali, mwanamke huyo alifanikiwa kukimbia na kwenda kuomba msaada.
Musilimu amesema, Chanzila baada ya kufanya mauaji hayo aliubeba mwili wa marehemu na kwenda kuutupa porini umbali wa mita 100 kutoka eneo alilofanyika mauaji.
Amesema mtuhumiwa huyo alikimbia kijijini hapo kwenda kusikojulikana baada ya mauaji hayo na Polisi inaendelea kumtafuta ili kumtia mbaroni na kufikishwa katika vyombo vya sheria ili kuchukua mkondo wake.
“Nawasihi wananchi ya kwamba kufanya mauaji ya aina mbalimbali kutokana na mapenzi, ushirikina au migogoro mbalimbali sio maamuzi sahihi, ni kinyume cha sheria, zipo njia ambazo zinaweza kutumika kupata suluhu ya mambo yanayojitokeza badala ya kuchukua maamuzi ya kuua mtu,” amesema Kamanda Musilimu.