Fursa ziara ya Rais wa Poland nchini

Rais  Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na mgeni wake Rais wa Poland, Andrzej Duda, Ikulu jijini Dar es Salaam leo. Picha Ikulu

Muktasari:

 Mkakati kuandaliwa safari za moja kwa moja za ndege kati ya Tanzania na Poland

Dar es Salaam. Tanzania na Poland zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya mataifa hayo.

Poland pia, itatoa bima kwa benki za biashara kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Makubaliano hayo yamefikiwa leo Februari 9, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Rais wa Poland, Andrzej Duda aliyekutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Uhusiano baina ya mataifa hayo ulianza mwaka 1962 na tangu wakati huo, Rais Duda amekuwa kiongozi wa kwanza wa Poland kuzuru Tanzania.

Katika miaka 62 ya uhusiano huo, Taifa hilo la Ulaya limekuwa likisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya mazungumzo yao, Rais Samia amesema Poland ni mbia mkubwa wa Tanzania ndani ya Umoja wa Ulaya (EU) katika shughuli za kiuchumi na uwekezaji, hususani utalii.

Amesema Poland ni miongoni mwa nchi 10 ambazo raia wake hutembelea Tanzania kwa wingi kwa madhumuni ya utalii.

Taifa hilo pia, linachangia shughuli za maendeleo nchini, ikiwamo katika sekta za afya.

Rais Samia amesema Poland inatekeleza mradi wa uboreshaji huduma unaotekelezwa katika hospitali tano nchini, Dar es Salaam zikiwa ni Aga Khan, hospitali za rufaa za mikoa za Temeke na Mwanayamala, Hospitali ya Chanika na Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.

“Ziara hii inatupa fursa ya kuimarisha uhusiano wetu wa kiuchumi na Poland ambayo ni ya 21 kiuchumi duniani,” amesema Rais Samia.

Amesema wamekubaliana kushirikiana kwenye maeneo ya elimu, kilimo, biashara, uwekezaji, utalii na Tehama pamoja  na kuimarisha uhusiano uliopo na kuhamasisha uwekezaji zaidi kwenye sekta za kimkakati kama vile viwanda, uzalishaji, nishati, madini na uchumi wa buluu.

“Nimemshukuru Rais Duda kwa utayari wake kupitia wakala wa mikopo ya usafirishaji wa Poland, kule kwao wanaita Kuke, kutoa bima kwa benki za biashara kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa vipande vya Makutupora hadi Tabora na Tabora hadi Isaka,” amesema Rais Samia.

“Hii ni hatua muhimu sana kwetu katika kutekeleza mradi huu wa kimkakati utakaoifungua zaidi nchi yetu. Pia, ni ishara kuwa Poland inatambua umuhimu wa mradi huu kwa maendeleo ya Tanzania lakini pia katika kukuza biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla.”

Maeneo mengine amesema ni utalii, biashara na uwekezaji.

Katika miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko la watalii kutoka Poland wanaotembelea nchini, hususani Zanzibar ambao mwaka 2023 walikuwa 41,000.

“Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita (Januari) watalii 6,000 kutoka Poland walitembelea nchi yetu. Ili kuchochea zaidi utalii na biashara, tumewaelekeza wataalamu wetu kuchukua hatua zitakazowezesha kuanza kwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Poland kuja Tanzania na tumeweka msisitizo huo kwa wenzetu Poland,” amesema Rais Samia.

Amesema amewakaribisha wawekezaji kutoka Poland kuja kuwekeza nchini kwenye sekta ya utalii, hususani ujenzi wa hoteli.

Rais Samia amesema Poland wameeleza maeneo ambayo wako vizuri ambayo ni uzalishaji viwandani na Tehama.

Kwa upande wake, Rais Duda ameishukuru Tanzania kwa kuwahifadhi raia wa Poland walioachwa na Russia wakati wa utawala wa Joseph Stalin.

Amesema kwenye mazungumzo na Rais Samia, amemhakikishia watalii zaidi kutoka Poland wataendelea kuja Tanzania, hasa kipindi hiki cha baridi kwao.

“Watalii wengi wataendelea kuja Tanzania kwa kuwa hali ya uchumi ya Poland iko vizuri na wengi wanataka kuja hapa. Kampuni nyingi zinatarajia kuja kuwekeza Tanzania, hususani Zanzibar,” amesema.

“Tumezungumza kuimarisha ushirikiano kwenye kilimo na elimu. Kuna kampuni moja ya uwekezaji kwenye kilimo iko tayari kuja kuwekeza,” amesema na kuongeza kuwa amemualika Rais Samia kuzuru Poland.

Pia, amewaalika vijana wa Tanzania kuenda Poland kutafuta fursa za masomo, akisema Taifa hilo lina vyuo vikuu bora vinavyotoka mafunzo kwenye fani tofauti ikiwemo uhandisi wa madini, Tehama na kilimo.

Atembelea Aga Khan

Akizungumza alipoitembelea Hospitali ya Aga Khan, Rais Duda amesema katika sekta ya afya, miongoni mwa miradi ambayo Serikali ya Poland imewekeza ni katika hospitali hiyo.

“Kwa hapa Aga Khan tumefanya maboresho ya utoaji wa huduma katika kitengo cha wagonjwa wa dharura ikiwa ni sehemu ya mradi huu wa kuboresha huduma ya dharura nchini Tanzania (IMECT) kupitia kupitia Polish Aid,” amesema.

Ameahidi kuendeleza ushirikiano kupitia mradi huo akisema umeweza kutoa mafunzo kwa wataalamu mbalimbali wanaohusika na uokoaji, wakiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Skauti.