Gazeti la Mwananchi lilivyomwongezea ujasiri Masimba kuhamisha nyuki kwa mkono

Athuman Masimba akiwahamisha nyuki kutoka kwenye tawi la mti na kuwahamishia mkononi mwake ili aweze kuondoka nao na kuwapeleka msituni ili wasidhuriwe au kuwadhuru watu.
Muktasari:
- Athuman Masimba amejizolea umaarufu katika viunga vya mji wa Geita kutokana na uwezo wake wa kukamata kundi la nyuki kwa mkono na kuwaondoa kwenye makazi ya watu, kisha kuwapeleka msituni bila kuvaa mavazi ya kujikinga wakati mwingine akitumia usafiri wa bodaboda na wenyewe kuendelea kuwa watulivu bila kusababisha madhara kwake wala kwa wengine.
Geita. Ni maajabu ya kweli. Unaweza kusema hivyo. Ni kutokana na uwezo wa kipekee wa Athuman Masimba (30), mzaliwa wa Muheza mkoani Tanga anayeishi Geita, wa kukamata kundi la nyuki kwa mkono bila kudhurika.

Masimba anayesema ujasiri huo, pamoja na mambo mengine, ameupata baada ya kusoma makala ya gazeti la Mwananchi mwaka 2019, amekuwa kivutio kwa wananchi pale inapotokea kundi la nyuki limeingia kwenye makazi ya watu, yeye huwahamisha kwa kuwabeba mkononi na kuwarudisha msituni bila kujeruhiwa wala watu kudhurika, jambo linalowaacha wengi mdomo wazi.
Masimba anasema alipokuwa shule, alipendelea kusoma majarida mbalimbali yenye habari za nyuki.
Anasema Jumamosi ya Mei 4, 2019 alisoma makala moja iliyoandikwa na Gazeti la Mwananchi ikiwa na kichwa cha habari ‘Unavyoweza kufuga nyuki kisasa’.

Masimba anasema Makala ile ilimvutia sana na siku hiyo alikata shauri la kumfanya nyuki kuwa rafiki kwake.
“Mwanzoni haikuwa rahisi, niling’atwa mara kadhaa lakini sikuacha nilivumilia hadi pale nilipoweza kuwadhibiti, naamini unapokuwa na nia na kitu, Mungu anakupa njia, kwenye ile makala mwandishi ameeleza hatari iliyopo kama nyuki hawatatunzwa na ipo hatari ya wadudu hao kutoweka,” anasema Masimba.
Kwa harakaharaka kazi hii ya Masimba inaweza kuonekana ya kawaida, lakini ukweli ni kwamba ina mvuto wa kipekee, na inahitaji ujasiri wa hali ya juu na maarifa ya ziada.

Katika mazingira ya kawaida, nyuki wanaweza kuwa hatari, lakini Masimba amekuwa akikabiliana nao kwa ujuzi na ujasiri akithibitisha uwezo wake wa kipekee.
Masimba ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya tisa wa mzee Ramadhani Masimba, ana elimu ya kidato cha nne na hakufanikiwa kuendelea na masomo lakini hiyo haikuwa kikwazo cha kushindwa kupambana kutafuta maisha nje ya elimu ya darasani.
Akifanya mahojiano na Mwananchi hivi karibuni kuhusu uwezo wake huo, amesema kipaji hicho kilianza kukua akiwa kwao Muheza.
Anasema alijifunza mbinu za asili za kukamata nyuki kutoka kwa ndugu zake waliokuwa wakirina asali msituni.

Hata hivyo, anasemauwa ujuzi wa kuhamisha kundi la nyuki kwa mkono, umekuwa kivutio kwa wakazi wengi wa Geita na umemsaidia pia kupata ajira kwa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), licha ya kuwa hajasomea utaalamu wa nyuki.
Anasema alipokuwa anafanya kazi ya kurina asali kwa kutumia moto au sumu, alikuwa anaumia anapoona nyuki wakifa kwa kuwa anawapenda, licha ya kuwa ni wadudu hatari.
Hivyo kutokana na hilo, aliamua kujifunza mbinu ya kuwazoea bila kusababisha madhara kwao au kwa watu.
“Kuanzia mwaka 2010 nilipomaliza darasa la saba nilikua naongozana na ndugu zangu kwenda kurina asali msituni, huko nilijifunza njia mbalimbali na nikafahamu sababu za kwa nini mtu anaweka mzinga na nyuki wanapita hawaingii, nikaamua kujifunza namna ya kuwavuta,” anasema.
Anasema siku moja akiwa nyumbani kwao, alichukua boksi akalitengeneza mfano wa mzinga kisha akachukua nta kama kivutio cha kuwaita nyuki waingie kwenye boksi hilo.
“Walikuja wengi wakaingia kwenye boksi wakawa wanaongezeka nikaamua kulihamisha, nao wakahamia kwenye mti na pale wakakaa kwa siku mbili na badaye waliondoka, hapo nikajua kumbe inawezekana kuwavuta nyuki na kuwatuliza wasilete madhara kwa watu,” anasema Masimba.
Anasema baada ya elimu ya vitendo aliyoipata kijijini kwao kabla ya kuhamia Geita, alikutana na wafanyakazi wawili wa TFS – Mzirai na Kwaselema anaosema pia walimsaidia kujifunza zaidi kwa kuwa alikuwa akifanya nao kazi kwa vitendo.
“Wazee hawa Mzirai na Kwaselema wamenisaidia sana, walikuwa wafanyakazi wa TFS Tanga licha ya kuwa nimekutana nao nikiwa tayari nina ujuzi kidogo, wamenisaidia kufika hapa nilipo japokuwa wao hawakamati nyuki kwa mkono kama mimi,” anasema Masimba.
Anasema wao kabla ya kuwahamisha nyuki, huvaa mavazi rasmi ya kujikinga wasiumwe lakini yeye havai chochote, bali huwa anatumia bomba la moshi linalotumiwa na warina asali tu.
Na anasema mara chache hutumia kitambaa kufunga kichwani hasa pale anapohamisha makundi makubwa ya nyuki.
Anasema akifunga kitambaa kichwani, humsaidia kuifanya akili yake itulie na kufanya kazi kwa utulivu zaidi.
Anavyowakamata bila kuumizwa
Masimba anasema moja ya mbinu anazotumia ni kufahamu aina ya kundi la nyuki na eneo lilipo. Anapofika eneo hilo, anachunguza mazingira na kuweka vizuizi ili kuzuia watu kupata madhara na kutoa tahadhari kwa watu wasogee mbali ili wasishtuke.
“Nikishahakikisha mazingira ni salama, nasogea kwenye kundi la nyuki nikitumia 'smoker' na baadaye nawahamisha kutoka walipo na kuwaweka mkononi mwangu. Kisha nawasafirisha hadi msituni na kuwaachia waendelee na shughuli zao,” anasema Masimba.
Kuhusu kuchomwa na miiba ya nyuki, Masimba anakiri kukumbana na kadhia hiyo lakini anasema uzoefu wake unamsaidia kuepukana na hilo.
Anasema kwenye kundi la zaidi ya nyuki 1,000, ni nadra sana nyuki mmoja kumchoma. Anaamini nyuki wana uwezo wa kutambua nia ya mtu, kama ni nzuri au mbaya.
Anasema mara nyingi hivi yeye hutumia usafiri wa bodaboda kuwasafirisha nyuki hadi msituni, na hata dereva wa bodaboda haadhuriki kwa sababu nyuki wakiwa mikononi mwake hujihisi wako salama.
Mbinu atumiazo
Akizungumzia mbinu za kuingia kwenye kundi la nyuki, Masimba anasema kwenye makundi hayo huwa kuna malkia, madume na nyuki vibaraka. Akimshika malkia, nyuki wengine wote humfuata.
Anasisitiza hakuna uchawi wala ushirikina, bali anatumia maarifa ya asili na kipaji alichopewa na Mungu. "Sihusishi uchawi katika kazi yangu. Hii ni kwa sababu ya mapenzi yangu kwa nyuki na elimu ya vitendo niliyopata kutoka kwa wale waliokuwa wakifuga nyuki nyumbani kwetu," anasisitiza.
Katika kazi hiyo, anasema huchukua kila tukio la kuokoa nyuki kama fursa ya kujifunza zaidi na anasema kazi hiyo ina mchango mkubwa kwa jamii.
Anasema mbali ya kuwaokoa nyuki, anasaidia pia kuzuia madhara kwa watu iwapo watawashambuliwa.
Anasema nyuki ni viumbe muhimu katika mazingira na hutoa mazao muhimu kama asali, nta na gundi nyeusi.
Katika utendaji wake wa kazi, Masimba anasema hutoa pia elimu kwa watu kuhusu faida za nyuki na mchango wao kwa mazingira.
Nini malengo yake ya baadaye
Masimba anasema ana mipango ya kuanzisha eneo maalumu la utunzaji wa nyuki na atakuwa anatoa mafunzo kwa jamii jinsi ya kutunza nyuki. Anasema licha ya kuwa na uwezo wa kuwakamata kwa mkono, anaamini elimu ya wadudu hao ni muhimu, hivyo anahitaji msaada kutoka serikalini na mashirika mengine ili kuboresha ujuzi wake.
“Nina ndoto ya kukuza kipaji changu na kuelewa zaidi kuhusu nyuki. Ikiwa nitapata nafasi ya kusoma chuoni, ningeweza kujifunza jinsi ya kunufaika na mazao ya nyuki kama sumu na maziwa ya nyuki na jinsi ya kuyahifadhi. Hii ni kiu yangu kubwa ya kupata utaalamu huu zaidi,” anasema Masimba.
Hata hivyo, anatoa wito kwa jamii kuacha mitazamo mibaya kuhusu nyuki badala yake watambue umuhimu wao.
“Nyuki ni wadudu muhimu sana katika mazingira yetu. Badala ya kuwaangamiza kwa sumu au moto, tunapaswa kujifunza jinsi ya kuwaweka salama na kutumia faida wanazotoa,” anasisitiza Masimba.
Wasemavyo wataalamu
Wakati Masimba akitumia njia hiyo, Ofisa wa nyuki wa Wilaya ya Geita, Egnasio Benjamin anasema kuna namna ya kuwahamisha kitaalamu ya kuwahamisha nyuki wanaovamia makazi ya watu.
Benjamin anasema ni muhimu mtaalamu anyewahamisha ajikinge kwa mavazi maalumu na kutumia bomba la moshi ili kupunguza ukali wa nyuki.
“Masimba anatumia njia yake ya kipekee, anawahamisha nyuki kwa mkono bila mavazi maalumu, jambo ambalo linahitaji ujasiri mkubwa,” anasema Benjamin.
Naye kaimu Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Geita, Sandusi Ngunyale anasema Masimba ana kipaji cha kipekee cha kucheza na nyuki bila kupata madhara.
Anasema jambo hilo liliwavutia TFS wakaamua kumwajiri kwa lengo la kuendeleza uwezo wake zaidi.
Hata wananchi wa Geita wameeleza kushangazwa na kipaji hiki cha Masimba, wakiona ni uwezo wa kipekee usio wa kawaida.
Basi Elias, mkazi wa Geita anasema; “Yaani haya ni maajabu kama sanaa, lakini anaisaidia jamii isidhulike na wadudu hawa hasa watoto ambao wakona makundi ya nyuki yapo kwenye mti hurusha mawe kutaka kuwatawanya hali hiyo inaweza kuleta madhara makubwa kwao.”
Naye Sagar Mganga, mkazi pia wa Geita anasema ni mara yake ya kwanza kumuona mtu akiwashika nyuki bila kuvaa vifaa vya kujikinga.
“Kwa kutazama na ninavyomfahamu nyuki bado siamini kama ni uwezo wa kawaida labda ana njia nyingine,” anasema.
Mkazi mwongine wa Katundu, Eliza Salenga anasema kazi aifanyao Masimba ni ya kipekee na inawaachia maswali mengi.
“Wapo wanaosema ni ushirikina, lakini mimi nimejifunza jambo la tofauti kwake, jamaa ana utaalamu,” amesema Salenga.