Gekul ataka biashara ya gongo ikomeshwe Babati
Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Pauline Gekul ambaye ni mbunge wa Babati Mjini mkoani Manyara akizungumza na wananchi wa jimbo lake. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amewaagiza watendaji wa mitaa ya Mji wa Babati Mkoani Manyara kukomesha biashara ya pombe haramu aina ya gongo
Babati. Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amewaagiza watendaji wa mitaa na vitongoji wa mji wa Babati kuwakamata wapikaji, wauzaji na wanywaji wa pombe haramu ya moshi, kwani inapunguza nguvu kazi ya Taifa.
Gekul ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Babati Mjini, ameyasema hayo leo Jumapili Julai 16 mtaa wa Imbilili kata ya Sigino, alipokuwa akizungumzia changamoto ya baadhi ya vijana kunywa gongo kwa wingi.
Amesema unywaji wa pombe hiyo haramu kwa baadhi ya vijana wengi husababisha washindwe kufanya kazi hivyo wapikaji, wauzaji na wanywaji, wanapaswa kukamatwa.
“Maofsia watendaji wa mitaa mnapaswa kukagua mitaa yenu na kusaka nyumba kwa nyumba zinazipikwa gongo na kuiharibu mitambo, muwapeleke polisi kisha mahakamani,” amesema.
Mkazi wa eneo hilo, John Beda amesema unywaji wa pombe haramu ya gongo imekuwa ikitajwa mara nyingi kuwaangamiza vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.
Beda amesema pombe hiyo ambayo inaonekana ikinyweka maeneo ya vijijini na mijini huwaathiri watumiaji kwa njia mbalimbali na kusababisha vifo vyao.
"Vijana wengi huwa wanasingizia baridi kuwa inachangia wanywe gongo japokuwa siyo kweli kwani wangetafuta njia mbadala hata ya michezo watoe baridi na siyo kunywa gongo," amesema.