Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gereji pembezoni mwa barabara, vyuma chakavu marufuku Dar

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa siku 90, majengo yote kando ya barabara kuu yapakwe rangi huku mafundi gereji wakitakiwa kuondoa zana zao mbele ya barabara hizo

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewaagiza wafanyabiashara wote wa vyuma chakavu pamoja na wamiliki wa biashara nyingine zinazotazama barabarani na kuathiri mandhari ya jiji, kuondoa vifaa hivyo na kuvipeleka ndani ya maeneo yao ya biashara.

Amesema Serikali ya mkoa imetoa mwezi mmoja kwa wamiliki wa gereji na biashara zote zilizopo kandokando ya barabara ambazo zimeweka vyuma chakavu au vifaa vinavyoonekana kutoka barabarani, kuhakikisha vinaondolewa na kuhifadhiwa ndani ya maeneo yao.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo leo Jumatatu Juni 15, 2026 alipozungumza katika kikao kilichowakutanisha watendaji wa Serikali za mitaa, wenyeviti wa mitaa na kata wote wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Natoa mwezi mmoja kwa wote wenye gereji zilizopo barabarani na ambao wameweka vyuma chakavu vinavyoonekana kutoka barabarani. Viondolewe na virudishwe nyuma ndani ya maeneo yao. “Atakayeshindwa kutekeleza agizo hili, biashara yake itafungwa hadi atakapolizingatia,” amesema Chalamila.

Amesisitiza hatua hiyo inalenga kuboresha usafi, mwonekano na hadhi ya Jiji la Dar es Salaam, ambalo ni kitovu cha biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini.

Akitoa mifano ya maeneo yaliyoathirika zaidi, Chalamila ametaja Barabara ya Tandale na baadhi ya maeneo ya Magomeni, akisema yamejaa vyuma chakavu vilivyowekwa pembezoni mwa barabara, hivyo kuharibu mandhari ya jiji.

Agizo la gereji kuhamishwa liliwahi kutolewa Oktoba15, 2021 na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla ambaye alipiga marufuku gereji bubu mkoani humo akieleza gereji hizo zilizokuwa katika hifadhi za barabara zilikuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira.

Mkakati huo uliambatana na operesheni maalumu ya kuwaondoa watu waliokuwa wakifanya shughuli hizo pamoja na wamachinga, ili kuruhusu usafi na kuondoa uchafu uliotokana na vifaa vya magari vilivyokuwa vimehifadhiwa katika maeneo ya gereji hizo; hata hivyo agizo hilo halikutekelezwa.

Katika kikao, Chalamila amesema wamiliki wa majengo machafu jijini humo wametakiwa kuhakikisha yanakuwa safi ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

"Kwa muda mrefu tumekuwa na majengo chakavu kando kando ya barabara kuu, bati zimechakaa zimeliwa na kutu.

“Ukipanda ndege unapokaribia kutua uwanja wa ndege Dar es Salaam, unachokiona unaweza kujiuliza humo ndani kuna watu au ni majengo yameachwa kuwa majumba ya makumbusho," amesema.

Ameelekeza majengo yote yaliyopo kandokando ya barabara kuu yapakwe rangi kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu.

"Ikiwezekana na bati zipigwe rangi, kwa ambaye hauwezi kubadilisha. Ili mgeni akija ajue majengo hayo ni masafi," ameagiza.

Amewataka pia wanaofanya biashara ya gereji mbele ya barabara wanapaswa kuondoa zana zao kwenye uso wa barabara.

Amewataka pia wanaouza mbao kuacha tabia ya kuweka mbao pembezoni mwa barabara ili kuweka safi uso wa mji.

Amewataka pia wanaohusika na bustani za barabarani kutumia wataalamu wenye sifa ili kuwa na barabara zenye bustani bora.

Amezungumzia pia dampo la Pugu Kinyamwezi, akiagiza mchakato kutangaza ubia wa kuendesha dampo hilo uanze.

"Naagiza mpaka Julai 30, mchakato wa kupata ubia wa kuendesha dampo hilo uwe umeanza," amesema.

Chalamila ameagiza halmashauri zote jijini humo kuwa na madampo ya taka, akisisitiza elimu ya utenganishaji na urejereshaji wa taka.

Pia, amekemea ubandikaji wa picha katika maeneo mbalimbali akiagiza matangazo yote yawekwe katika maeneo yanayostahili.

"Unakuta mtu anaweka tangazo lake kesho ninachinja kiti moto halafu anakwenda kubandika msikitini. Lazima ujue jambo gani liwekwe mahali gani," amesema.

Akizungumza katika kikao hicho, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal ameahidi kufanyia kazi maelekezo hayo, akiwaagiza viongozi na watendaji wa jiji hilo kuhakikisha maelekezo hayo wanayafanyia kazi.

"Na mimi kwa niaba ya wenzangu na wananchi nikuahidi maelekezo tunakwenda kuyafanya kazi. Maelekezo haya uliyoyatoa kimsingi ndiyo dira ya kiongozi wa nchi yetu," amesema.