GGML yapokea Gold Peer Exchange Programme
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mhandisi Baraka Manyama, akizungumza na Wanachama wa mpango wa UK-Ghana Gold peer exchange programme, kuhusu uzoefu wa STAMICO katika kusaidia mabadiliko kwenye sekta ya wachimbaji wadogo wa madini nchini. Ziara hiyo iliwezeshwa na Kampuni ya AngloGold Ashanti - Geita Gold Mining Limited (GGML) katika jitihada za kuendeleza uwajibikaji katika uchimbaji.
Wajumbe wa mpango wa UK-Ghana Gold peer exchange wametembelea Tanzania wiki hii kwa ziara ya mafunzo inayolenga kujenga uwezo wa wachimbaji wadogo na wa kati (ASM) pamoja na kuimarisha uchimbaji wa madini wa dhahabu unaozingatia uwajibikaji.
Ziara hiyo imewezeshwa na Kampuni ya AngloGold Ashanti – Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na taasisi muhimu za sekta ya madini nchini.
Wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mhandisi Baraka Manyama, alieleza uzoefu wa shirika hilo katika kusaidia mabadiliko kwenye sekta ya wachimbaji wadogo kupitia mafunzo, upatikanaji wa fedha, na urahisishaji wa taratibu za kisheria.
Aidha, Mwanajiolojia wa STAMICO, Denis Nkwabi, alitoa maelezo kuhusu juhudi zinazoendelea za kufanikisha urasimishaji wa shughuli za wachimbaji wadogo nchini.
Wajumbe hao pia walikutana na viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Geita akiwemo Mkuu wa Mkoa, Martin Shigella, na Afisa Madini wa Mkoa, kujifunza namna ushirikiano wa serikali za mitaa na wadau wa sekta unavyosaidia kuongeza usalama na uendelevu katika uchimbaji.
Vilevile, walitembelea Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na taasisi nyingine muhimu za sekta.
Uzoefu wa Tanzania katika kudhibiti uchimbaji haramu na magendo ya madini kupitia ushirikishwaji mpana wa wachimbaji wadogo ulitoa somo muhimu kwa wajumbe hao, ambao wanatarajia kutumia maarifa hayo kuboresha mifumo yao nchini Ghana na Uingereza.