Gharama kubwa, mazoea vyakwamisha matumizi nishati safi

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa NBS, zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanatumia nishati chafu ya kupikia, sababi zikitajwa kuwa ni gharama kubwa za nishati safi na mazoea mabaya ya watumiaji.

Morogoro. Wadau katika sekta ya nishati safi ya kupikia wamebainisha changamoto ya upatikanaji wa nishati hiyo kuwa ni pamoja na gharama kubwa na mazoea mabaya kwa watumiaji kuendelea kutumia nishati chafu ya kupikia.

Hali hiyo imeelezwa kukwaza utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa 2033 unaolenga kuongeza idadi ya watumiaji wa nishati safi hadi kufikia asilimia 80 nchini.

Kwa mujibu wa ripoti ya Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Maralia (THDS) ya mwaka 2022 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ni asilimia saba pekee ya Watanzania wanaotumia nishati safi kupikia nchini.

Akizungumza juzi Novemba 22 mkoani Morogoro katika kongamano lililowakutanisha wadau wa nishati safi kupikia chini ya mradi wa Inclusive Green Economy (IGE), mhadhiri wa uchumi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk Remidius Ruhinduka alisema changamoto inayokwamisha matumizi ya nishati safi ni pamoja na gharama na mazoea mabaya.

“Gharama za kununua nishati inapoisha ni kubwa na kingine ni tabia tu, kwani kuna mtu anaamini ni lazima awe na jiko linalotumia nishati isiyo safi," alisema.

Pia alisema licha ya umeme kufika maeneo ya vijijini kwa zaidi ya asilimia 75, lakini ni asilimia 45 pekee waliounganisha nishati hiyo kutokana na gharama kubwa za kuunganisha ikiwa ni pamoja na zile ya kuweka mfumo wa waya kwenye nyumba.

"Mfano unakuta mtumiaji anapika chai bila kufunika hivyo kuchukua muda mrefu hadi kuwa tayari, lakini kama angefunika ingechukuchua muda mfupi na kuokoa kiwango fulani cha gesi kwa hiyo anaona ni gharama kumbe ni namna anavyotumia," alisema.

Akielezea jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ameitaja miradi ya kimkakati ukiwemo ujenzi wa bwawa la umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na Mradi wa Umeme Vijijini (REA).

Pia ameutaja mradi wa Cook Fund unaosimamiwa na Serikali kwa udhamini wa Umoja wa Ulaya (EU) wenye lengo la kuhakikisha idadi kubwa ya Watanzania wanatumia nishati safi kupikia.

Dk Ruhinduka alisema kwa sasa nishati kuni ndiyo inayoongoza ikiwa na asilimia 60.9 ya watumiaji ikifuatiwa na mkaa asilimia 28.8, gesi 3.2 na umeme 2.1, Sola 1.1 na nishati nyingine 2.5.

Alisema matumizi ya kuni yako juu vijijini ikiwa ni asilimia 84.8 ikilinganishwa na asilimia 17.4 mijini huku matumizi ya mkaa yakiwa juu mijini kwa asilimia 65.5 akilinganishwa na asilimia 11.5 vijijini.

Hata hivyo, Dk Ruhinduka alisema kuna matumaini ya kuwepo kwa ongezeko la watumiaji wa nishati safi kutokana na ongezeko la wadau katika sekta hiyo.

"Kwa mfano kwa takriban miaka 15 (2001 - 2015) hakukuwa na ongezeko la watumiaji wa gesi nchini, lakini ndani ya miaka saba iliyopita tumeona asilimia ya watumiaji ikiongezeka kutoka asilimia 0.3 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 3.2 mwaka jana," alisema Dk Ruhinduka.

Naye Mhandisi Shukurani Rugaimukamu wa Wizara ya Nishati alisema ili kufanikisha mkakati wa Kitaifa wa nishati safi ya kupikia kwa asilimia 80 ya Watanzania ifikapo 2033 Serikali inaendelea kutoa elimu ili kuongeza uelewa kwa umma na taasisi juu ya umuhimu wa kutumia nishati safi.

“Tumejikita katika kupanua wigo wa utafiti na uvumbuzi katika teknolojia zinazohusiana na njia safi na salama za kupikia pamoja na kujenga uwezo wa watekelezaji katika miradi ya nishati safi za kupikia,” alisema.

Mtafiti mwandamizi wa mradi wa Inclusive Green Economy (IGE) na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Aloyce Hepelwa alisema mbali na kukaa na wadau wa sekta hiyo, pia mradi huo unawahusisha watunga sera.

"Zamani utafiti ulikuwa ukifanyika bila kuhusisha watunga sera hivyo ilikuwa vigumu kwa tafiti kufanyiwa kazi lakini sasahivi tunafanya kwa pamoja ili waweze kuona ukubwa wa tatizo na hatimaye kufanyia kazi tafiti ambazo tunazifanya kwa pamoja," alisema Dk Hepelwa.