Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gramu 900 za heroin zawatupa jela maisha ‘wazungu wa unga’ wawili

Muktasari:

  • Waliohukumiwa adhabu hiyo ni mshtakiwa wa kwanza, Hassan Aziz Mohamed na wa pili, Hassan Shabani Hassan huku mshtakiwa wa tatu, William Sebastian Daraja akiachiwa huru kwa kukosekana kwa ushahidi dhidi yake.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi, imewahukumu kifungo cha maisha, wakazi wawili wa Tegeta Jijini Dar es Salaam kwa kosa la kusafirisha gramu 983 za dawa za kulevya aina ya Heroin.

Hukumu hiyo imetolewa Dar es Salaam Desemba 17, 2024 na Jaji Sedekia Kisanya wa mahakama hiyo, ambapo aliamuru wafungwa hao warejeshewe simu nne na fedha ikiwamo Rand 900 za Afrika Kusini walizokutwa nazo.

Katika hukumu yake ambayo ilipatikana leo Desemba 18, 2024 katika tovuti ya mahakama, Jaji Kisanya alisema ushahidi uliotolewa umeonyesha fedha hizo pamoja na Sh150, 000 na Dola 77 za Marekani hazina uhusiano na kosa hilo.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni mshtakiwa wa kwanza, Hassan Aziz Mohamed na wa pili, Hassan Shabani Hassan huku mshtakiwa wa tatu, William Sebastian Daraja akiachiwa huru kwa kukosekana kwa ushahidi dhidi yake.

Jaji alisema ushahidi umethibitisha kuwa begi la rangi ya kijani lililokuwa na dawa hizo, kwanza lilikuwa mikononi mwa mshtakiwa wa pili, na baadaye likawa kwa mshtakiwa wa kwanza kabla ya kukamatwa kwao Septemba 4, 2019.

“Kukutwa na dawa kama ilivyoelezwa awali, ni kigezo muhimu (critical component) cha kosa la kusafirisha dawa za kulevya kama inavyoelezwa katika kifungu cha 2 cha sheria ya udhibiti dawa za kelevya au DCE Act,”alisema Jaji.

Jaji alisema ushahidi unaonyesha sampuli za dawa hizo zilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo vipimo vilithibitisha ni dawa aina ya Heroin yenye uzito wa gramu 983.5 hivyo Jamhuri ilithibitisha kosa bila kuacha mashaka.

“Baada ya kuchambua ushahidi na vielelezo, ninawaona mshtakiwa wa kwanza na wa pili wana hatia ya kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha sheria lakini namuona mshtakiwa wa tatu (William) hana hatia ya kosa hilo,”alieleza Jaji.

Walivyodakwa na dawa

Ushahidi uliotolewa unaeleza jioni ya Septemba 4, 2019, shahidi wa tatu, mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Hassan Msangi alikuwa akiongoza timu ya doria kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Lengo la timu hiyo ilikuwa ni kuwapata wahalifu wanaojihusisha na dawa za kulevya ambapo wakiwa katika doria hiyo eneo la Madale Jijini Dar es Salaam, ASP Msangi alipokea simu kutoka kwa msiri wake kuhusiana na suala hilo.

Msiri huyo alimjulisha kuwa kungekuwa na biashara ya dawa za kulevya itakayofanyika eneo la Tegeta Nyaishozi, ambapo waliwajulisha wenzake na kumjulisha bosi wake ambaye alitoa baraka za kuifanya kazi hiyo.

ASP Msangi aliandaa kikao cha siri na mtoa taarifa huyo ambaye baadaye aliwaongoza hadi eneo husika ambapo maofisa walijificha. Baadaye mshtakiwa wa kwanza, Hassan Aziz alijitokeza katika eneo hilo.

Haikupita muda mrefu dereva pikipiki, maarufu kama bodaboda akiwa amembeba abiria aliwasili eneo hilo na dereva huyo alitambuliwa kuwa ni William Sebastian aliyekuwa mshtakiwa wa tatu, aliyeachiwa na mahakama.

Abiria huyo alitambuliwa na msiri wa maofisa hao kuwa ni mshtakiwa wa pili, Hassan Shaban, ambapo mshtakiwa huyo alionekana akimkabidhi mshtakiwa wa kwanza begi lililokuwa na rangi ya kijani na hapo wakatiwa mbaroni.

Kulingana na mashahidi hao waliotoa ushahidi wao, wakiwa hapo na tayari wamewakamata washukiwa hao watatu, ilikuja pikipiki nyingine ya pili lakini haraka ilitokomea kusikojulikana baada ya kubaini hali si shwari.

Baada ya kukamatwa, washukiwa hao walipekuliwa na ndani ya begi la kijani kulikutwa mfuko wa nailoni ukiwa na unga unayodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya, ambapo baadaye  vipimo vya maabara vilithibitisha ni Heroin.

Mshtakiwa wa kwanza alikutwa na pochi nyeusi ambayo ndani yake ilikuwa na fedha za Tanzania Sh150,000, Dola 77 za Marekani na pesa za Afrika Kusini (Rand) 900 na simu za mkononi ambazo washtakiwa wote walikuwa nazo.

Walivyojitetea kortini

Katika utetezi wake, mshtakiwa wa kwanza alidai kuwa Septemba 4,2019, yeye na mkewe, Amina Mbaruku Simba, walikuwa wanatoka hospitali ya Rabininsia kwenda eneo la Tegeta Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumjulia hali mjomba.

Baada ya kutoka kumsalimia mjomba wao huyo, kuna magari mawili yalijitokeza mbele yao eneo la Dawasco na kumkamata na alipohoji kwa nini wanamkamata, hakujibiwa bali alisukumwa hadi ardhini katika eneo hilo.

Alidai kuwa mshtakiwa wa pili naye alikamatwa alipojitokeza kuulizia kulikoni wakati mshtakiwa wa tatu alikamatwa alipokwenda kuulizia fedha zake za kumbeba mshtakiwa wa pili hadi eneo la tukio alipokamatwa na polisi.

Mshtakiwa wa pili yeye alieleza kuwa alikuwa akisafiri na bodaboda iliyokuwa ikiendeshwa na mshtakiwa wa tatu kwa ajili ya kununua mahitaji ya salon yake, lakini walipofika eneo la Tegeta Dawasco walikuta kuna umati mkubwa wa watu.

Hapo aliwaona polisi wakimshambulia kwa kipigo Hassan Aziz ambaye alikuwa ni mteja wake na kwa kuwa lilikuwa si tukio la kawaida, alisogelea eneo hilo na kuhoji kulikoni na ndipo alipokamatwa naye kupigwa na polisi hao.

Alisema msitakiwa wa tatu alihusishwa na suala hilo alipokuja kudai fedha yake ya nauli na ndipo shahidi wa tatu alitoa begi lenye rangi ya kijani alilodai lilikuwa na dawa za kulevya na alipelekwa ofisi za DCEA kuandika maelezo.

Kwa upande wake, mshtakiwa wa tatu alijitetea kuwa yeye ni dereva bodaboda na anaishi eneo la Boko Chasimba na kwamba siku ya tukio alimbeba abiria ambaye baadaye alimtambua kama mshtakiwa wa pili, kwenda Tegeta Nyuki.

Walipokuwa wanakaribia eneo la Tegeta Dawasco, walikutana na kundi kubwa la watu ambapo abiria wake alimtambua mtu mmoja aliyekuwa anapigwa ambapo alimtaka asimame ili aweze kwenda kuulizia kwa nini anapigwa.

Baada ya kusubiri kwa muda, alimshuhudia abiria wake akiwekwa chini ya ulinzi hivyo akaenda kumdai pesa yake ya nauli, na ndipo kuna mtu mmoja alimwambia kuwa anawaingilia polisi ili wasiweze kutekeleza majukumu yao.

Hapo alishangaa kuona anakamatwa na polisi, kupigwa hadi kuumizwa na baadaye alifungwa pingu na kwa ujumla akakanusha tuhuma dhidi yake na kushangaa namna alivyounganishwa kwa kosa ambalo halifahamu.