Hakimu agoma ucheleweshaji kesi, sasa kusikilizwa kwa siku 30

Muktasari:

  • Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka 51 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu wa kupanga na kusafirisha vipande 660 vya meno ya Tembo vyenye thamani ya Sh 4.6bilioni.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesema kesi ya kusafirisha vipande 660 vya meno ya Tembo vyenye thamani ya Sh4.6 bilioni, inayowakabili wafanyabiashara 12, itasikilizwa ndani ya mwezi mmoja kuanzia Mei 30 Hadi Juni 30 na kisha kutolewa hukumu.

Pia Mahakama hiyo imewataka washtakiwa kujiandaa kisaikolojia kujisimamia wenyewe mahakamani iwapo mawakili wao hawatafika mahakamani.

Lengo la kusikiliza kesi hiyo ndani ya mwezi mmoja ni kutokana na kuwa kesi hiyo kuwa ya muda mrefu na imekuwa iliahirishwa mara kwa mara bila kuendelea na usikilizwaji.

Uamuzi huo umetolewa leo, Mei 24, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya kusikilizwa mfulumizo.

" Hii kesi ilikuwa kwa hakimu mwingi, nimepewa mimi nimepitia na kusoma jalada zima, kesi hii ni miongoni mwa kesi zilizopo katika mrundikano wa kesi nyingi ambazo zinatakiwa kusikilizwa ndani ya mwezi mmoja na kutolewa Hukumu, hivyo katika hili niwatake mawakili wa pande zote kutokuwa na sababu zitakazopeleka kesi hii ishindwe kuendelea" amesema Hakimu Mrio na kuongeza

"Sitaahirisha kesi hii kwa kigezo kuwa wakili wa utetezi hayupo mahakamani, hivyo washtakiwa mnatakiwa kujiandaa kisaikolojia, wakili wako asipokuwepo mahakamani utajisimamia mwenyewe na kesi itaendelea, hatutahirisha kesi kwa sababu hizo" amesema hakimu Mrio.

Hakimu Mrio baada ya kusema hayo, aliahirisha kesi hiyo Mei 30, 2023 itakapoendelea na ushahidi wa upade wa mashtaka.

Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi Karen Mrango akishirikiana na Timotheo Mmari amedia kuwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 19/2022 ilipangwa Leo kwa ajili ya kupangiwa tarehe baada ya kuhamishwa kutoka kwa Hakimu Mkazi, Rhoda Ngimilanga kwenda kwa Hakimu Mrio.

Mrango amedai kuwa upande wa mashtaka wapo tayari kuendelea na ushahadi tarehe yoyote ambayo Mahakama hiyo itakuwa imepanga.

Hata hivyo upande wa utetezi ukiongozwa na Josephat Mabula uliomba Mahakama iwape muda ili waweze kupangilia kesi za wateja wao wengine ambazo nazo zinaendelea katika Mahakama tofauti.

Ombi hiyo lilipingwa na hakimu Mrio kwa maelezo kuwa kesi iliyopo mbele yake inatakiwa kuisha ndani ya muda wa mwezi mmoja.

Idadi ya mashtaka yanayowakabili; wafanyabiasha hao wanaokabiliwa na mashtaka 51 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu wa kupanga na kusafirisha vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh 4.6bilioni.

Pia, wanadaiwa kukutwa pesa taslimu dola za kimarekani 5662, ambazo ni sawa na Sh 12,270,492.

Tayari shahidi mmoja wa upande wa mashtaka, Wilfred Olomi, ambaye ni Mtunza vielelezo kutoka Wizara ya Maliasili, ameshatoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Ally Sharif (28) raia wa Guinea, mfanyabiashara na mkazi wa Tabata Segerea; Victor Mawalla (29) maarufu kama Daudi Minja, mfanyabiashara na mkazi wa Kimara Korogwe; Haruna Kassa (37) mfanyabiashara na mkazi wa Mwanagati; Abasi Hassan (40) maarufu kama Jabu, mfanyabiashara na mkazi wa Mwanagati Kitunda; Solomon Mtenya (46) maarufu kama Kuhembe, mkulima na mkazi wa Kimara Baruti pamoja na Mussa Ligagabile (59) ambaye ni dereva na mkazi wa kibonde maji- Mbagala.

Wengine ni Khalfani Kahengele (64) fundi randa na mkazi wa Keko; Ismail Kassa (53) fundi cherehani na mkazi wa Kipunguni B; Kassim Saidi (50) maarufu kama Bedui, mfanyabiashara na mkazi wa Arusha; Peter Nyanchiwa (46) mfanyabiashara na mkazi wa Isenye; John Buhanza (60) maarufu kama John Muya au Tariye, mfanyabiashara na mkazi wa Gongolamboto pamoja na mfanyabiashara Musa Musa (46) maarufu kama Musa Abdallah.

 Kesi ya msingi:

Sharifu na wenzake wanadaiwa  kuongoza uhalifu wa kupangwa, tukio wanalodaiwa  kutenda kati ya Januari 2006 na Juni 2016 katika jiji la Dar es Salaam.

Pia, katika kipindi hicho, washtakiwa wanadaiwa kuuza, kununua, kupokea, kuhamisha, kusafirisha na kumiliki nyara za Serikali ambazo ni vipande 660 vya meno ya tembo yenye thamani ya 4,656,795,000 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na sheria ya wanyama pori.

Shtaka jingine,  kati ya April Mosi , 2016 na Juni 24, 2016 katika eneo la Mbezi Msakuzi, lililopo wilaya ya Ubungo, washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakimiliki vipande hivyo, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori