Hakimu atupa tena hoja za utetezi kesi ya Sabaya

Hakimu atupa tena hoja za utetezi kesi ya Sabaya

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, leo imetupilia mbali ombi la wakili wa utetezi, Sylvester Kahunduka la kuomba kumkumbusha shahidi wa sita wa jamhuri, Bakari Msangi maelezo aliyoandika polisi kutokana na shahidi huyo kuonekana kutokukumbuka vitu vingi alivyoandika polisi.

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, leo imetupilia mbali ombi la wakili wa utetezi, Sylvester Kahunduka la kuomba kumkumbusha shahidi wa sita wa jamhuri, Bakari Msangi maelezo aliyoandika polisi kutokana na shahidi huyo kuonekana kutokukumbuka vitu vingi alivyoandika polisi.


Ombi hilo liliwasilishwa leo Jumatatu Agosti 2, 2021 na wakili huyo wakati akiendelea kumhoji shahidi huyo wa sita wa upande wa jamhuri katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili.


Mahakama ilitupilia mbali ombi hilo la wakili Kahunduka ambaye anamtetea mshitakiwa wa pili Sylvester Nyegu aliyeomba kutumia kifungu cha 168 (1, 2) cha Sheria ya Ushahidi kumkumbusha shahidi maelezo aliyoandika polisi kwa sababu inaonekana vitu vingi hakumbuki ili aweze kukumbuka.


Wakili huyo aliomba mahakama hiyo iridhie upande wa jamhuri kutoa nakala halisi ya maelezo ya shahidi huyo aliyoyatoa polisi.


Kahunduka aliieleza mahakama kuwa shahidi amesema vitu vingi hakumbuki hivyo ndiyo maana ameomna tena maelezo hayo shahidi aliyoyatoa polisi asomewe ili aweze kukumbuka.


Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka aliieleza mahakama kuwa kabla hawajampa maelezo hayo wana hoja za kisheria kuhusu matumizi ya kifungu hicho na kudai kifungu walichokitumia siyo sahihi wao (utetezi) kukitumia.


"Kama jamhuri tunapinga matumizi ya hiki kifungu ambapo tunaona wakili anataka kutumia mlango wa nyuma katika kutumia kile ambacho mahakama ilishakataa,"alieleza
Wakili Kweka alidai ombi hilo la wakili wa utetezi haliko kisheria hivyo ni ombi lao kuwa lisikubaliwe.


Akiwasilisha hoja ya nyongeza wakili wa Serikali, Baraka Mgaya aliieleza mahakama kuwa kifungu hicho cha 168(1, 2)hoja ya kuomba kukumbushwa inatakiwa itoke kwa shahidi mwenyewe na kinampa shahidi aliyepo mbele ya mahakama iwapo anaona ameulizwa kitu hakumbuki vizuri anaomba kurejea.


"Shahidi aliyepo mbele yako hakutoa ombi hilo kuwa anahitaji kukumbuka maandiko yoyote aliyoyatoa awali, kwa sababu shahidi hajaomba wakili anachojaribu kufanya ni kutumia mlango wa nyuma kuingiza haya maelezo kwa kujifanya anataka kumkumbusha shahidi  na mahakama ilishatoa uamuzi kwenye hilo kwamba alishakosea."


Wakili Kweka aliongeza kuwa kifungu namba 172 cha sheria hiyo ya ushahidi kimetoa mwongozo wa ni nani anayepaswa kutumia kifungu hicho cha 168(1, 2) ambapo wanaotajwa kutakiwa kukitumka ni upande waliomuita shahidi na siyo upande unaomhoji.  


Akitoa uamuzi mdogo Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo anayesikiliza shauri hilo alisema mahakama inatupilia mbali ombi la wakili wa utetezi kwani kifungu namba 168 (1, 2) kiko kwa yule aliyemleta shahidi kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 172.


Baada ya uamuzi huo wakili Kahunduka alimalizia kumhoji shahidi huyo.