Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Halmashauri kudhibiti matumizi majengo yasiyokamilika Kariakoo

Muktasari:

  • Serikali imeanza kudhibiti matumizi ya majengo yasiyokamilika kwa kuweka ukaguzi maalum na vibali vya muda ili kuhakikisha usalama wa wananchi ambapo hatua hii imepunguza hatari za moto Kariakoo, kuongeza uwajibikaji wa wamiliki, na kuimarisha usalama wa biashara na ujenzi kwa ujumla.



Dar es Salaam. Serikali imeweka utaratibu wa ukaguzi maalumu na utoaji vibali ili kudhibiti matumizi ya majengo yasiyokamilika, ambayo awali yalitumika kwa shughuli mbalimbali za biashara na huduma.

Hatua hiyo ya Serikali, imekuja baada ya ripoti ya uchunguzi wa Mwananchi ya Aprili mwaka huu, kuibua ongezeko la matumizi ya majengo yasiyokamilika kwa shughuli mbalimbali, hali inayohatarisha maisha ya watumiaji.

Kuanzia Aprili 20 hadi 22, 2026 Mwananchi ilitoa ripoti maalumu ya miezi mitatu Desemba 2025 na Februari 2026 kuhusu matumizi ya majengo yasiyokamilika Kariakoo na athari zake ikiwepo majanga ya moto ya mara kwa mara.

Ripoti hiyo ilibainisha kwamba nyuma ya kasi ujenzi wa maghorofa, kuna taswira nyingine isiyoonekana kirahisi ya matumizi ya majengo ambayo bado yapo kwenye hatua za ujenzi kabla ya kukamilika na kukaguliwa rasmi na mamlaka husika.

Chini ya majengo hayo, wafanyabiashara wamefungua maduka, wateja wanaingia na kutoka, huku juu mafundi wakiendelea na kazi. Nyaya za umeme zikiwa wazi, vifaa vya ujenzi vimepangwa pembezoni mwa sakafu za juu na njia za dharura hazionekani.

Ujenzi unaoendelea sambamba na biashara, unaacha mianya mikubwa ya hatari kuanzia kuanguka kwa mbao, nondo na milunda, achilia mbali mifumo duni ya umeme hadi kukosekana kwa maandalizi ya kukabiliana na majanga kama moto au jengo kuporomoka.

Akizungumza na Mwananchi Juni 10, 2026 ikiwa zaidi ya mwezi kupita tangu ilipotoka ripoti hiyo maalumu, mmoja wa maofisa wa Halmashauri ya jiji la Dar e salaam ambaye ameomba hifadhi ya jina lake amesema tangu gazeti hili litoe habari kuhusu hatari hiyo, kumekuwa na ukaguzi kwa kila jengo linalohitajika kutumika kabla ya kutoa kibali cha matumizi.

Anasema jiji kwa sasa wanatoa cheti cha muda cha kutumika sehemu ya jengo (Partial Certificate of Occupation) inayoruhusu matumizi ya sehemu ya jengo kwa masharti maalumu ya kiusalama, ikiwemo ujenzi kufanyika usiku.

Ukaguzi huo, anasema unahusisha tathmini ya uimara wa sehemu zinazotumika, mazingira ya kazi pamoja na vifaa vya ujenzi vilivyofungwa katika jengo husika.

"Lengo ni kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao bila kuwekwa kwenye hatari ya kuangukiwa na vifaa au sehemu za jengo ambazo bado hazijakamilika pamoja na kufanya uhakiki wa vibali vyao vya ujenzi kikamilifu," anasema.

Ofisa huyo, anaeleza kumekuwa na maombi ya kutumika kwa majengo yasiyokamilika kwa upande wa Kariakoo kutokana na uwepo wa madeni ya mikopo ya benki, hivyo wamewataka wamiliki kupeleka vielelezo ambavyo vitashirikisha idara zote za ujenzi katika ukaguzi.

Katika kuhakikisha ukaguzi huo unafanyiwa kazi, anasema wamekuwa wakiwataka wale wote ambao wanakiuka taratibu zilizowekwa kufika katika ofisi za jiji huku wengine wakitozwa faini kulingana na kosa.

“Hili limesaidia kuondoa kero kadhaa ambayo zilikuwa zinawakumba wafanyabiashara na wateja wanaofika eneo la Kariakoo,” anasema.


Zimamoto yakazia

Akizungumza na Mwananchi Juni 11, 2026 Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Peter Mwabusi, alisema wameanza operesheni ya ukaguzi miezi miwili sasa ikiwa na lengo la kuhakikisha majengo yote yanawekewa mifumo ya kinga dhidi ya moto.

Hatua mbalimbali zilizochukuliwa kupitia operesheni hiyo, alisema zimechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa matukio ya moto katika eneo la Kariakoo hususani kwa majengo yanayoendelea na ujenzi kwa kuwa yamekuwa na idadi kubwa.

Alisema katika ukaguzi huo, wamiliki wa majengo walipewa muda wa kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na jeshi hilo ili kuboresha usalama wa majengo yao.

“Operesheni hii inalenga kufanya ukaguzi wa majengo na kuhakikisha yana mifumo ya kuzuia na kudhibiti moto, baadhi ya wamiliki tayari wameanza kutekeleza maelekezo tuliyowapa, huku wale watakaoshindwa kutekeleza wakitarajiwa kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Mwabusi.

Mwabusi, alisema kati ya  Februari hadi Juni, 2026 jeshi hilo limechukua hatua kali kwa watu ambao moto umetokea katika maeneo yao kutokana na uzembe, jambo ambalo limeongeza umakini kwa wananchi na wamiliki wa majengo.

Alieleza baadhi ya watu waliochukuliwa hatua wamefika katika ofisi za jeshi hilo kueleza kuwa hawatarudia tena makosa yaliyosababisha matukio hayo.

Pamoja na hatua hizo, alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limefungua kituo cha zimamoto katika eneo la Kariakoo ili kuimarisha huduma za dharura na kuongeza kasi ya mwitikio pindi matukio ya moto yanapotokea.


Mkandarasi


Mkandarasi wa jengo lililopo Mtaa wa Sikukuu na Mchikichi, Jamali Mloko, anasema kwa sasa ukaguzi umekuwa ukifanyika katika kila hatua ya mradi kuanzia ubomoaji wa jengo la awali, hatua za msingi za ujenzi, hadi pale sehemu za jengo zinapoanza kutumika.

“Ukaguzi unafanywa kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali pamoja na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) na wadau walioingia ubia katika miradi husika ili kuhakikisha kila hatua inazingatia viwango vya usalama," anasema Mloko.

Anasema lengo ni kuhakikisha shughuli za ujenzi zinaendelea sambamba na matumizi ya jengo bila kuhatarisha maisha ya watu, ndiyo maana kuna ukaguzi wa mara kwa mara wa vifaa vya usalama na  miundombinu umeme.