Hatari ya kisukari kwa mwanamke

Ugonjwa wa kisukari unaweza kuleta changamoto nyingi katika maisha ya wanawake wanaoishi na ugonjwa huu, moja ya athari kubwa za kisukari kwa wanawake ni kuendeleza matatizo ya moyo na mishipa ya damu.

Wanawake wenye kisukari wapo katika hatari kubwa ya kupata shinikizo la damu, maambukizi katika njia ya mkojo, kiharusi na hata matatizo ya moyo na yanaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya na hata kusababisha kifo.

Mbali na matatizo ya moyo, wanawake wenye kisukari wanaweza pia kukabiliwa na matatizo ya figo. Kisukari kinaweza kusababisha uharibifu kwa figo na hatimaye kusababisha ugonjwa wa figo. Hii inaweza kuhitaji matibabu ya mara kwa mara.

Kisukari pia kinaweza kuathiri afya ya macho. Baadhi ya madhara ya kawaida ya kisukari kuathiri mishipa ya damu nyuma ya pazia la jicho, ambayo inaweza kusababisha upofu na tatizo la mtoto wa jicho, ambayo inaweza kusababisha upotevu wa uwezo wa kuona vizuri.

Wanawake wenye kisukari pia wanaweza kukabiliwa na shida ya kushika mimba kwa sababu kisukari kinaathiri homoni, mimba kuharibika mara kwa mara. Lakini pia kupata shida wakati wa kujifungua.

Kisukari inaweza kusababisha matatizo kipindi cha ujauzito kama vile mtoto kuongezeka uzito akiwa bado yupo tumboni kwa mama na hali hii husababisha wakati wa kujifungua, mama anaweza kuwa na hatari kubwa ya kujifungua watoto walio na uzito mkubwa au hata matatizo ya kujifungua kama vile kuvuja kwa damu au kupasuka kwa kifuko cha maji.

Wanawake wenye ugonjwa wa kisukari watapata maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI) mara kwa mara na hii husababishwa na hali kushindwa kuthibiti viwango vya sukari mara kwa mara.

Mbali na athari za kimwili, kisukari pia kinaweza kuathiri afya ya akili ya mwanamke. Wanawake wenye kisukari wanaweza kuwa na hatari kubwa ya kupata matatizo ya kiafya ya akili kama vile unyogovu au wasiwasi.

Hali hizi zinaweza kuathiri sana ubora wa maisha ya mwanamke na uwezo wake wa kufanya shughuli za kila siku.

Kisukari ni tatizo kubwa la kiafya kwa wanawake na linaweza kuwa na athari kubwa kwa afya zao na ustawi wao kwa ujumla.

Ni muhimu kwa wanawake kufahamu hatari za kisukari na kuchukua hatua za kudhibiti na kushughulikia hali hii mapema.
Kwa kufanya hivyo, wanaweza kuepuka au kupunguza athari za kisukari kwa maisha yao na kudumisha afya njema na ustawi.

Ni muhimu pia kwa wanawake kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kufuata maelekezo ya madaktari wao ili kudhibiti viwango vyao vya sukari na kuzuia matatizo ya kiafya yanayoweza kutokea.