Mambo 14 muhimu kwa mwanamke wa miaka zaidi ya 45

Leo ni siku ya kimataifa ya wanawake duniani, makala hii ni maalum kwa wanawake wote hapa nchini ambao kijamii wao ni sehemu ya kundi maalum.

Ufahamu wa leo utalenga kundi la wanawake ambalo linaelekea uzeeni yaani miaka 45 na kuendelea, ambao ndio wako katika hatari zaidi kupata magonjwa mbalimbali.

Mambo yafuatayo yanaweza kusaidia kujikinga na kupunguza hatari ya kupata magonjwa mbalimbali ikiwamo yale ya kuambukiza, yanayoenea kwa njia ya kujamiiana na yasiyoambukiza ikiwamo saratani, magonjwa ya moyo na mishipa, kisukari, kiharusi na magonjwa ya figo.

Bima ya Afya. Ukiumwa unatibiwa kwa njia ipi? Bima ya afya, uchangiaji au malipo tasilimu? Weka mipango yako vizuri uwe na bima ya afya. Kumbuka kujikinga ni rahisi ila kujitibu ni gharama.

Kula lishe inayoendana na umri. Epuka ulaji holela wa vyakula vyenye chumvi, sukari, wanga mwingi na mafuta mengi. Tumia zaidi mboga majani, matunda, nafaka isiyokobolewa na protini rafiki kama jamii za kunde na samaki.

Zingatia kanuni za afya. Uandaaji wa vyakula uzingatie usafi na kunywa maji ambayo ni safi na salama, glasi nane hadi 10 kwa siku.

Epuka matumizi ya pombe na uvutaji wa tumbaku. Hivi vinakuweka katika hatari ya kupata saratani mbalimbali na magonjwa mengine ikiwamo ya moyo.

Mazoezi mepesi. Fanya mazoezi ya kutembea kwa siku dakika 30-60 katika siku tano za wiki. Au fanya kazi za kuushughulisha mwili.

Fanya uchunguzi wa kiafya na hudhuria kampeni za kitaifa. Angalau pima afya mara moja kwa miezi sita. Hudhuria uchunguzi wa saratani ya mlango wa uzazi na matiti wakati wa kampeni.

Shikamana na elimu inayotolewa ikiwamo kujichunguza mwili wako kila unapoamka hasa katika matiti na njia ya uzazi.

Shikamana na ushauri na matibabu. Wenye magonjwa sugu ikiwamo vvu, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na kisukari wasiache kutumia dawa na kuhudhuria kliniki zao.

Epuka matumizi ya dawa na matibabu holela. Ni rahisi kuvutika na matibabu ya mitandaoni na mtaani. Matumizi holela ya dawa, vipodozi na bidhaa zisizothibitishwa usalama wake yanahatarisha afya yako.

Jikinge na magonjwa ya akili. Epuka mifarakano isiyo ya lazima ili kujiepusha na shinikizo la akili, msongo wa mawazo na hofu kali, pia usikae na jambo linaloumiza hisia zako. Kumbuka haya yanachangia magonjwa ya akili na shinikizo la damu.

Waone washauri tiba au wataalam wa afya ya akili, kumbuka kutetereka kwa akili pia husababisha kinga ya mwili kuwa dhaifu hatimaye kupata magonjwa kirahisi.

Kulala, mapumziko na kujiburudisha. Lala kwa saa sita had inane kwa usiku mmoja, hakikisha eneo la kupumzika linakuwa tulivu na lenye hewa safi. Burudika ili upate hisia nzuri, hii inakupa utulivu wa mwili na akili.

Jikinge na magonjwa yanayoenea kwa kujamiana. Kuwa na mwenza mmoja mwaminifu asiyeambukizwa au zingatia njia zote za kujikinga ikiwamo matumizi ya mipira ili kujikinga na virusi vya ukimwi na magonjwa ya (STI/STDs).

Usiyape kisogo magonjwa haya. Kumbuka katika maeneo ya Afrika magonjwa hatari ya kuambukiza ni pamoja na vvu, kifua kikuu na malaria. Hakikisha unashikamana na njia zote kujikinga nayo.

Fika mapema katika huduma za afya. Unapoona dalili na viashiria vya kuumwa wahi kituo kilicho jirani yako.

Mambo haya ndio mienendo na mitindo mizuri ya kimaisha endapo utashikamana nayo inapunguza hatari ya kupata magonjwa hatimaye kuishi maisha marefu ukiwa na afya njema.