Prime
Hatari za kumtuliza mtoto kwa simu
Muktasari:
- Wataalamu waeleza kuwa tabia hiyo humfanya mtoto, badala ya kufikiri na kubuni, kujikuta akitumia muda mwingi kutazama video na katuni, hali inayoufanya ubongo wake kuwa mpokeaji wa taarifa pekee badala ya kuzalisha mawazo mapya.
Dar es Salaam. Kilio cha mtoto kilipoanza kusikika ndani ya daladala iliyokuwa ikitokea Mbagala kwenda Gerezani, jijini Dar es Salaam, mama aliyekuwa amembeba hakumbembeleza. Badala yake, alitoa simu yake ya mkononi, akafungua video za katuni na kumpa.
Baada ya sekunde chache, mtoto alinyamaza. Akili na mawazo yake yote yakawa kwenye simu hiyo, hakusikika tena akilia. Abiria waliona mama huyo amepata suluhisho la haraka.
Miaka ya karibuni, simu za mkononi zimekuwa sehemu ya malezi katika familia nyingi. Watoto hupewa simu wanapolia, wanapokataa kula, wanaposafiri, wazazi wanapokuwa na shughuli za nyumbani au wanapotaka kupata utulivu wa muda mfupi.
Hata hivyo, wataalamu wa ukuaji wa mtoto wanaonya kuwa huo ndio mwanzo wa tatizo linaloweza kumgharimu mtoto kwa miaka mingi baadaye, kuanzia kupungua kwa ubunifu, kushindwa kudhibiti hisia hadi kuchelewa kukuza uwezo wa kujifunza.
Ingawa hali hiyo huwapa wazazi nafasi ya kuendelea na shughuli zao, wataalamu wa afya ya watoto na saikolojia wanaonya kuwa matumizi ya simu kama njia ya kumtuliza mtoto yanaweza kuathiri ukuaji wa ubongo, lugha, hisia na ubunifu.
Onyo hilo linaungwa mkono na mwongozo mpya wa American Academy of Pediatrics (AAP) wa mwaka 2025 unaosisitiza kuwa kutumia vifaa vya kidijitali kama njia ya kumtuliza mtoto kunaweza kumzuia kujifunza namna ya kudhibiti hisia zake na kusababisha maendeleo duni ya kujifunza na ukuaji.
Matokeo hayo yanafanana na utafiti uliochapishwa katika jarida la Jama Pediatrics la Marekani, uliofanywa na Dk Jenny Radesky na wenzake, uliowafuatilia watoto 422 wenye umri wa miaka mitatu hadi mitano kwa kipindi cha miezi sita.
Utafiti huo ulibaini kuwa watoto waliotulizwa mara kwa mara kwa kupewa simu walikuwa na uwezekano mkubwa wa kupata changamoto za kudhibiti hisia kadri walivyokuwa wakikua, kwa sababu walikosa nafasi ya kujifunza mbinu za kawaida za kujituliza.
Wasemavyo wataalamu
Mwanasaikolojia wa watoto, Stella Mligo, anasema ubongo wa mtoto hukua kwa kasi kupitia mawasiliano ya ana kwa ana, kucheza, kuuliza maswali na kugundua mazingira yanayomzunguka.
Anasema mtoto anapopewa simu kila anapolia au anapochoshwa, ubongo wake haupati nafasi ya kutafuta mbinu nyingine za kujituliza.
"Mtoto anaanza kuamini kuwa kila hisia ngumu zinaondolewa na skrini. Hilo linamnyima nafasi ya kujifunza uvumilivu, kujidhibiti na hata kufikiri mwenyewe. Mtoto anayekuzwa kwa mazungumzo na ushiriki wa mzazi hujifunza namna ya kutambua hisia zake na kuzisimamia, tofauti na anayezibwa hisia kwa video kila anapolia," anasema.
Kwa upande wake, Dk Selestin Mpiri anasema moja ya zawadi kubwa ambayo mzazi anaweza kumpa mtoto si simu ya mkononi, bali ni nafasi ya kuchoka na kujitafutia shughuli za kufanya.
Anasema mtoto anapopata muda wa kuchoka, ubongo wake huanza kutafuta njia za kujiburudisha kwa kubuni michezo, kutengeneza vitu au kufikiri mbinu mpya, hali inayochochea ukuaji wa ubunifu.
"Moja ya zawadi kubwa sana ambayo unaweza kumpa mtoto si simu. Ni kumruhusu achoke. Mtoto akichoka ataanza kuwa mbunifu. Atajibunia michezo yake mwenyewe, na hiyo ndiyo inakuza sehemu ya ubongo inayohusika na ubunifu," anasema Dk Mpiri.
Anasema uwezo huo wa ubunifu ni msingi wa mafanikio katika taaluma nyingi, kuanzia sanaa, muziki hadi taaluma zinazohitaji watu wenye uwezo wa kutatua changamoto kwa njia mpya.
"Baadaye akiwa msanii atahitaji ubunifu, akiwa mwanamuziki atahitaji ubunifu, hata katika kazi za ofisini uwezo wa kufikiri kwa ubunifu unahitajika. Tunaupunguza uwezo huo kila tunapomkabidhi mtoto simu kila anapokuwa hana shughuli," anasema.
Anasema badala ya kutumia muda kufikiri na kubuni, watoto wengi hujikuta wakitumia saa nyingi kutazama video na katuni, hali inayoufanya ubongo wao kuwa mpokeaji wa taarifa pekee badala ya kuzalisha mawazo mapya.
Dk Mpiri anasema matumizi ya simu pia huwanyima watoto nafasi ya kujifunza kupitia mazingira yanayowazunguka.
Anatoa mfano wa mzazi anayempeleka mtoto hospitalini, lakini badala ya mtoto kutazama mazingira, kuona jinsi madaktari wanavyofanya kazi au kujifunza namna wagonjwa wanavyohudumiwa, anakabidhiwa simu na kujitenga na kila kinachoendelea.
"Mtoto akiwa hospitalini angeweza kuona daktari anavyoongea na wagonjwa, akajifunza hata labda siku moja angependa kuwa daktari, lakini akiwa ameshika simu muda wote, anakosa uhusiano huo na mazingira yanayomzunguka," anasema.
Anasema wazazi wengi hutafuta njia ya haraka ya kumtuliza mtoto kwa kumpa simu, bila kutambua kuwa wanajenga utegemezi ambao baadaye huwa mgumu kuuvunja.
"Tuchukulie kama utegemezi mwingine wowote. Si rahisi kuuacha. Ukijaribu kumnyang'anya mtoto simu, analia kwa sababu tayari ameizoea," amesema.
Mtaalamu wa saikolojia ya elimu, Dk Asha Komba, anasema ubunifu haujengwi kwa kutazama video, bali kwa mtoto kutumia mawazo yake kutengeneza ulimwengu wake.
Anasema mtoto anapocheza na mawe, vijiti au vifuniko vya chupa, huweza kuvigeuza kuwa magari, nyumba, ndege au watu.
"Hapo ndipo ubunifu unapozaliwa, lakini kwenye simu kila kitu tayari kimechorwa, kimeimbwa na kimeamuliwa. Mtoto hubaki kuwa mtazamaji badala ya mbunifu," anasema Dk Asha.
Mambo ni mabaya hata darasani
Mtaalamu wa elimu ya awali, Dk Rehema Mshana, anasema athari za watoto kutumia simu huonekana mapema wanapoanza shule.
Anasema watoto waliokulia kwenye matumizi makubwa ya simu mara nyingi hupata ugumu wa kushiriki michezo ya kubuni, kuchora au kuelezea mawazo yao.
"Ukimpa mtoto karatasi na rangi achore alichokiona, wengine hushindwa kabisa kwa sababu wamezoea kupokea picha zilizokamilika kutoka kwenye skrini. Simu humpa mtoto majibu ya haraka badala ya kumfundisha kufikiri, kujaribu na kukosea, hatua ambazo ndizo msingi wa kujifunza," anasema Dk Rehema.
Mbali na ubunifu, mtoto anayekaa muda mwingi kwenye simu hupoteza nafasi muhimu ya kujifunza lugha.
"Lugha hukua kupitia mazungumzo kati ya mtoto na mzazi, kusikiliza hadithi, kuimba na kuuliza maswali. Simu haiwezi kuchukua nafasi ya mazungumzo. Mtoto anayezungumza na wazazi wake hujifunza maneno mapya, namna ya kueleza hisia na kujenga uhusiano," anasema.
Mwanasaikolojia tiba, Dk Joseph Mrema, anasema kosa kubwa ambalo wazazi wengi hulifanya ni kuchukulia kilio cha mtoto kama tatizo linalopaswa kuzimwa haraka.
"Kulia ni lugha ya mtoto. Anapopewa simu na kunyamaza, haimaanishi ameeleweka. Mara nyingi amenyamazishwa tu."
Anasema mtoto anayekumbatiwa, kusikilizwa na kupewa nafasi ya kueleza hisia zake hukua akiwa na uwezo mzuri wa kukabiliana na changamoto za maisha.
Wazazi wakiri tatizo ni kubwa
Wazazi waliozungumza na Mwananchi wanaeleza kuwa simu zimekuwa msaada wa muda mfupi, lakini baadaye zimeleta changamoto.
Grace Mushi, mama wa watoto wawili, anasema zamani alikuwa akimpa mwanawe simu kila alipokuwa akifanya kazi za nyumbani.
"Niliona ni njia rahisi kwa sababu alikuwa anakaa kimya, lakini baadaye alianza kulia kila nilipoichukua simu. Hapo sasa ikawa changamoto. Wakati mwingine nilikuwa nalazimika kumchapa ili anyamaze," anasema.
Kwa upande wake, Juma Salum, baba wa mtoto wa miaka minne, anasema mazingira ya maisha ya sasa ndiyo yanayowasukuma wazazi wengi kufanya hivyo.
"Unatoka kazini umechoka, mtoto analia, simu inaonekana suluhisho la haraka. Lakini baadaye unagundua hawezi kula wala kusafiri bila kushika simu," amesema Salum.