Hatma kesi aliyefanya mtihani darasa la saba gerezani kujulikana leo

Muktasari:

  • Shauri la kesi ya kuua bila kukusudia linalomkabili mtoto Kunde Gambija Kilulu (15) aliyefanya mtihani wa darasa la saba akishikiliwa katika Gereza la Bariadi mkoani Simiyu linatarajiwa kutolewa hukumu leo, Novemba 10 katika Mahakama Kuu ya Shinyanga inayoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.

Bariadi. Shauri la kesi ya kuua bila kukusudia linalomkabili mtoto Kunde Gambija Kilulu (15) aliyefanya mtihani wa darasa la saba akishikiliwa katika Gereza la Bariadi mkoani Simiyu linatarajiwa kutolewa hukumu leo, Novemba 10 katika Mahakama Kuu ya Shinyanga inayoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.

Jaji Seif Mwishehe Kulita tayari amefika katika mahakama hii huku mawakili wa Serikali na wa upande wa utetezi wakiwa mahakamani wakisubiri taarifa ya mtoto kutoka ofisi ya ustawi wa jamii ili kesi iweze kutajwa. Kesi hii itasikilizwa katika mahakama ya ndani kwa sababu za kisheria kutokana na umri wa mtoto huyo anayetuhumiwa.

Kwa mara ya kwanza, shauri la kesi hii ya mauaji namba 66 ya mwaka 2021 inayomkabili mtoto huyu na baba yake mzazi, Sayi Gisabu lilisomwa Novemba 8 likitarajiwa kutolewa hukumu leo.

Baada ya kesi hiyo kusikilizwa, Wakili Samwel Lugundija alizungumza na Mwananchi na kueleza kuwa upande wa utetezi ulitoa hoja kuiomba mahakama kubadilisha hati ya mashitaka kutoka kesi ya mauaji na kuwa kesi ya kuua bila kukusudia na hoja hiyo ilikubaliwa.

Alisema mtoto alikili kosa dogo la kuua bila kukusudia na kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, mahakama ilishindwa kutoa hukumu dhidi ya mtoto kwa sababu ya kisheria ambapo mahakama ilihitaji taarifa kutoka ustawi wa jamii ili iweze kutoa hukumu.

Kunde Gambija Kilulu  ni mhitimu wa darasa la saba aliyefanya mtihani wa Taifa akiwa gerezani na kufaulu kwa kupata daraja B kuwaongoza wenzake kwa ufaulu katika Shule ya Msingi Dasina B wilayani Itilima.