Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Simulizi ya mtoto aliyefanya mitihani darasa la saba gerezani

Mtoto aliyefanya mitihani la saba gerezani afunguka

Muktasari:

  • Licha ya changamoto zinazomkabili mtoto huyo, uongozi wa gereza wafurahia kufanikisha ndoto zake

Bariadi. Licha ya kushikiliwa gerezani kwa tuhuma zinazomkabili, Kunde Gambija Kilulu (15) alikuwa miongoni mwa zaidi ya watahiniwa milioni 1.1 waliofanya mitihani ya darasa la saba na hatimaye kufaulu kwa daraja B.

Wakati wanafunzi wenzake wakifanya mitihani hiyo wakiwa katika mazingira ya kawaida shuleni, kwake ilikuwa tofauti kwa sababu aliifanyia siyo tu akiwa chini ya ulinzi, bali katikati ya kuta za Gereza la Bariadi mkoani Simiyu alikowekwa mahabusu kutokana na tuhuma za mauaji zinazomkabili yeye na baba yake mzazi.

Akizungumza na Mwananchi akiwa chini ya usimamizi wa uongozi wa gereza hilo, Kunde, anayeshikiliwa tangu Julai 16, alisema ufaulu alioupata siyo tu umemtia faraja, bali umerejesha ndoto zake za kielimu zilizoanza kuyeyuka baada ya kushtakiwa na kutupwa mahabusu.

Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwa mkuu wa gereza, mwanafunzi huyo alisema matumaini yalianza siku uongozi wa gereza ulipomwombea kibali cha kuendelea kujisomea na kufanya mitihani.

“Siku napelekwa mahabusu nilianza kukata tamaa ya kuendelea kusoma. Lakini matumaini yangu yalirejea siku mkuu wa gereza alipofanya ziara ya kuwatembelea wafungwa na mahabusu, ambapo nilimwomba anisaidie niweze kufanya mitihani, ombi lililokubaliwa,” alisema Kunde akitabasamu.

“Siku nawasilisha ombi la kusaidiwa kufanya mitihani, zilikuwa zimesalia wiki mbili kabla ya siku ya mitihani ya kitaifa. Namshukuru Mungu kwa kila kinachotokea kwenye maisha yangu,” alisema.

Siku chache baada ya kuwasilishaombi lake, anasema ofisa elimu kata wa eneo lilipo gereza, alimpelekea zana na vifaa vya kujisomea pamoja na mwalimu aliyekuwa akimfundisha na kumwelekeza mbinu za kufanya na kufaulu mitihani.

“Chumba changu cha mitihani kilikuwa humuhumu gerezani na nilikuwa mtahiniwa pekee, namshukuru mwalimu wangu wa hapa gerezani kwa jinsi alivyonitia moyo wa kujiamini na matumaini yaliyoniwezesha kufanya bila hofu hadi kufaulu,” alisema.

Alisema furaha yake iliongezeka maradufu siku alipoitwa na mkuu wa gereza na kusomewa matokeo ya mitihani yakionyesha amefaulu, jambo linalomwongezea ari na nia ya kusoma kwa bidi masomo ya sekondari bila kujali mazingira anayoishi kwa sasa.

Akiwa anajiandaa kwa hatua inayofuata kuyakabili masomo ya sekondari, mtoto huyo aliiomba Serikali kumsaidia kutimiza ndoto zake wakati akiendelea kusubiri hatima ya tuhuma zinazomkabili.

“Naamini iko siku kesi hii itaisha. Naomba kwa jamii na wote wenye mapenzi mema kunisaidia kupata mwanasheria wa kusimamia kesi yangu imalizike kwa haki,” alisema Kilulu.


Uongozi wa gereza

Bwanajela wa Gereza Kuu Bariadi, Abel Gwambasa aliyempokea, alisema japo ni jukumu lake kuwasaidia wafungwa na mahabusu kupata haki na stahiki zao za msingi, ombi la mtoto huyo kuhusu kufanya mitihani lilikuwa miongoni mwa mambo yaliyougusa moyo wake baada ya kuona dhamira na matumaini yake kielimu.

“Ilikuwa ni wiki ya kwanza tangu mtoto huyo alipoingia mahabusu nilipofanya ukaguzi na kupokea ombi lake la kusaidiwa kufanya mitihani ya darasa la saba. Niliwasilisha taarifa kwa mkuu wa magereza mkoa kwa taratibu za kiutawala zilizowezesha kupatikana kwa zana na vifaa vya kumwezesha kujisomea,” alisema Gwambasa.

Baadaye, alisema uongozi wa gereza ulitangaza kumtafuta mfungwa au mahabusu mwenye taaluma ya elimu kwa ajili ya kumsaidia mwanafunzi huyo aliyeonyesha kutokata tamaa kimasomo licha ya kukabiliwa na kesi.

“Tulimpata mwalimu wa masomo ya sayansi, hasa hisabati ambaye alimsaidia na matokeo yake sote tunayafurahia kwa sababu amefaulu vizuri,” alisema

Alisema hata historia ya mwanafunzi huyo kutoka kwa walimu wake inaonyesha alikuwa miongoni mwa wanafunzi wenye juhudi kimasomo na kuahidi kuwa uongozi wa gereza utafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuhakikisa anaendelea kusoma.

“Hata sasa tayari ameanza maandalizi ya kujisomea masomo ya kidato cha kwanza, ni mtoto mwenye bidii, juhudi na malengo,” alisema bwanajela huyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Simiyu, Huruma Mwalyaje alisema wamefarijika kuona jitihada za kumsaidia Kunde zimezaa matunda.

“Tulipopokea taarifa za yeye kujisajili kufanya mitihani na ombi lake, mara moja tulilifikisha suala hilo kwenye mamlaka za Serikali akiwamo Mkuu wa Mkoa, David Kafulila aliyeguswa na kufika yeye mwenyewe gerezani kumwona na kuzungumza naye kumtia moyo,” alisema Mwalyaje.

Baada ya ziara ya mkuu wa mkoa, alisema taratibu za kufanikisha ombi la mwanafunzi huyo zilianza kuchukuliwa kwa kulishirikisha Jeshi la Magereza, Mahakama na Baraza la Mitihani ya Tanzania (Necta) kwa kuunda kikosi kazi kulifanikisha.

“Kufanikisha jambo hilo haikuwa rahisi, lakini tunashukuru mkuu wa magereza nchini, Jeshi la Polisi na Necta pamoja na mamlaka nyingine kumwezesha mtoto huyu kufanya mitihani yake na kufaulu,” alisema.

Kutokana na taratibu za kiusalama, mtoto huyo aliandaliwa chumba na mazingira maalumu kufanya mitihani akiwa eneo la gereza. Kutokana na tukio hilo ambalo kwao ni la kihistoria, alisema ufanyike utafiti wa kutosha kubaini watoto waliopo mahabusu na kupoteza haki zao kwa kutozijua, kuziomba au kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili waweze kupata haki zao, ikiwemo ya kuendelea na masomo.

Mkuu huyo wa magereza pia aliwaomba Watanzania wenye tatizo la kisheria kuiga mfano wa Kunde kwa kuomba haki zao wanapokuwa chini ya ulinzi.


Idara ya elimu yammwagia sifa

Akimzungumzia mwanafunzi huyo, Ofisa elimu wa Wilaya ya Itilima, Marry Maka alisema ofisi yake inajivunia mafanikio yake, huku akieleza kuwa rekodi zake zinaonyesha kuwa ni miongoni mwa wanafunzi wenye juhudi.

“Kunde ni miongoni mwa wanafunzi waliokuwa kwenye kambi za kitaaluma zinazoandaliwa kwa wanafunzi wa madarasa ya mitihani, siku ya tukio lililosababisha ashtakiwe na kuwekwa mahabusu alirejea nyumbani kufuata mahitaji,” alisema Mary.

Alisema idara ya elimu kwa kushirikiana na ustawi wa jamii zitamsaidia mwanafunzi huyo kuendelea na masomo ya sekondari bila kujali kama ataachiwa huru au kutiwa hatiani katika kesi inayomkabili.

“Kusoma ni haki yake ya msingi, bila kujali mazingira anayoishi kwa sasa, kwa sababu ameonyesha nia na bidii, tutaendelea kumwezesha kutimiza ndoto zake,” alisema Mary.