Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haya hapa masharti uombaji mikopo ya elimu ya juu, dirisha likifunguliwa rasmi

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dk Bill Kiwia (katikati), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 19, 2026. Kulia ni Mkurugenzi wa Uchambuzi, Upangaji na Utoaji Mikopo, Dk Peter Mmari na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Elihuruma Lema. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Serikali imetenga Sh1.07 trilioni kwa ajili ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi takribani 280,000 katika mwaka wa masomo 2026/27. HESLB imewataka waombaji kuwasilisha maombi yao kabla ya Agosti 31, 2026.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefungua rasmi dirisha la maombi ya mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/27, huku Serikali ikitenga Sh1.07 trilioni zitakazowanufaisha wanafunzi takribani 280,000.

Akizungumza leo Juni 19, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia, amesema dirisha hilo litakuwa wazi kuanzia Juni 19 hadi Agosti 31, 2026 kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu pamoja na waombaji wa ruzuku ya Samia Scholarship.

“Tunawatangazia vijana, wazazi na walezi kuwa dirisha la maombi ya mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/27 limefunguliwa rasmi leo. Tunawasihi waombaji wote kuwasilisha maombi yao ndani ya muda uliopangwa,” amesema Dk Kiwia.

Amesema kufunguliwa kwa dirisha hilo kumeambatana na kutolewa kwa miongozo minne ya utoaji mikopo na ruzuku ambayo tayari inapatikana kupitia mfumo na tovuti ya HESLB.

Miongozo hiyo inahusu mikopo kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza, stashahada, stashahada ya juu ya mafunzo ya sheria kwa vitendo (Law School) pamoja na mwongozo wa utoaji wa ruzuku ya Samia Scholarship.

Dk Kiwia amewataka waombaji kusoma kwa makini miongozo hiyo kabla ya kuanza kujaza fomu ili kuepuka makosa yanayoweza kuchelewesha au kuathiri upatikanaji wa mikopo.

Amesema baada ya dirisha la maombi kufungwa, bodi itaanza mchakato wa uchambuzi na upangaji wa mikopo kwa waombaji waliokidhi vigezo, huku ugawaji wa mikopo ukitarajiwa kuanza Novemba mwaka huu.


Masharti muhimu kwa waombaji

Dk Kiwia amesema hatua ya kwanza kwa mwombaji ni kutembelea tovuti ya HESLB na kujisajili kwa kutumia namba yake ya mtihani wa kidato cha nne kabla ya kufuata hatua nyingine za mfumo.

Amesisitiza kuwa waombaji wanapaswa kutumia namba ileile ya mtihani wa kidato cha nne waliyoitumia wakati wa kuomba udahili katika taasisi za elimu ya juu.

Aidha, amesema vyeti vya kuzaliwa au vyeti vya vifo kwa waombaji wenye wazazi waliofariki dunia vinapaswa kuwa vimehakikiwa na kupata namba maalumu za uhakiki kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kwa Tanzania Bara au taasisi husika Zanzibar.

Kwa upande wa utambulisho wa taifa, amesema waombaji wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wanatakiwa kuwasilisha Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) wakati wa kufanya maombi.

“Waombaji ambao bado hawajafikisha umri wa miaka 18 wanaweza kuendelea na maombi hata kama hawana NIN, lakini wanashauriwa kuanza mapema mchakato wa kuipata,” amesema.

Pia, amewatahadharisha wanafunzi dhidi ya kutegemea ushauri kutoka kwa watu wasiohusika au vyanzo visivyo rasmi wakati wa kujaza maombi yao.

“Tunawaomba watumie taarifa na miongozo rasmi inayotolewa na HESLB pekee ili kuepuka makosa yanayoweza kuathiri maombi yao,” amesema.


HESLB yatumia teknolojia kurahisisha huduma

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchambuzi, Upangaji na Utoaji wa Mikopo wa HESLB, Dk Peter Mmari, amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali yameendelea kuongeza uwazi, ufanisi na kasi ya utoaji wa huduma kwa wanafunzi.

Amesema bodi imeunganisha mifumo yake na taasisi mbalimbali za Serikali ili kurahisisha uhakiki wa taarifa za waombaji na kupunguza muda uliokuwa ukitumika kuthibitisha nyaraka mbalimbali.

“Tunaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali ili kuhakikisha taarifa za waombaji zinathibitishwa kwa haraka na kwa usahihi zaidi,” amesema.

Hata hivyo, amesema baadhi ya wanafunzi, hasa wa maeneo ya vijijini, bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za intaneti.

Kutokana na hali hiyo, HESLB imeingia ushirikiano na Shirika la Posta Tanzania ili kuwawezesha wanafunzi kupata huduma za maombi ya mikopo katika ofisi za posta zilizopo katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini.

“Posta ina mtandao mpana unaofika karibu kila eneo la nchi. Ushirikiano huu utawasaidia wanafunzi wengi kupata huduma za maombi bila kulazimika kutafuta huduma za ‘internet cafe’ au vituo binafsi,” amesema Dk Mmari.