Haya hapa mashtaka yanayomkabili Padri

 Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Sostenes Bahati Soka akifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Sostenes Bahati Soka, Padri wa Kanisa Katoliki, Parokia Teule ya Mtakatifu Deonis Aropagita, Jimbo la Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro amesomeshwa mashtaka matatu katika Mahakama mbili tofauti.

Moshi. Sostenes Bahati Soka, Padri wa Kanisa Katoliki, Parokia Teule ya Mtakatifu Deonis Aropagita, Jimbo la Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro amesomeshwa mashtaka matatu katika Mahakama mbili tofauti.

Padri huyo mwenye miaka 41, amesomeshwa mashataka hayo leo Jumatatu, Septemba 26, 2022 kwa nyakati tofauti akianza na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kisha Mahakama ya Wilaya ya Moshi.

Kesi ya kwanza ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Salome Mshasha ambapo Padri huyo anakabiliwa na shtaka moja la kumbaka mtoto wa miaka 12.

Wakili wa Serikali, Kasimu Nasiri amesema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika

Mshtakiwa huyo amekana shtaka hilo huku Wakili wa Serikali, Kasimu Nasiri akisema upelelezi umekamilika na Hakimu Salome ameiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 10, 2022 ambapo atafikishwa kusomewa maelezo ya awali.

Mshtakiwa huyo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wakazi wa Kilimanjaro ambao wawe na uwezo wakuweka bondi ya Sh10 milioni, kika mmoja.

Padri Soka amekosa dhamana kutokana na wadhamini kutokidhi vigezo.

Katika kesi nyingine, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya, Erasto Phily mshtakiwa huyo amesomewa shtaka moja la ubakaji wa mtoto.

Kesi hiyo namba 349 ya mwaka 2022, mwendesha mastaka wa Serikali, Verediana Mlenza na Nitike Immanuel wamesema upelelezi umekamilika.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo amepata dhamana na kesi hiyo itakuja tena Oktoba 12, 2022 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Aidha, katika kesi ya tatu, padri huyo ameshtakiwa kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka 12, eneo la kanisa alilokuwa anahudumu.

Kesi hiyo ya Jinai namba 44 ya 2022, imetajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Jenipha Edward ambapo padri huyo nadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 2022.

Waendesha mashtaka wa Serikali, Kambarage Samson na Veridiana Mlenza wameieleza Mahakama hiyo upelelezi umekamilik.

Mshtakiwa ameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuweka bondi ya Sh2 milioni

Kesi hiyo imehairishwa hadi Oktoba 18, 2022 ambapo kesi itakuja kwaajili ya kusomewa maelezo ya awali