Inatisha, padri mbaroni akidaiwa kulawiti watoto 10

Muktasari:

Anatuhumiwa kuwadhalilisha watoto zaidi ya 10 wa mafundisho ya komunio na kipaimara. Huwapa kati ya Sh3,000 hadi Sh5,000.

Moshi/Dar. Vitendo vya udhalilishaji wa kingono kwa watoto vinazidi kuitikisa nchi na sasa padri mmoja wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwabaka na kuwalawiti watoto zaidi ya 10.

 Watoto hao ni wanafunzi wa kuanzia darasa la sita hadi kidato cha kwanza waliokuwa wakihudhuria mafundisho ya komunio ya kwanza na kipaimara.

Inadaiwa kila alipomaliza haja zake, padri huyo humpa kila mmoja kati ya Sh3, 000 na Sh5,000.

Wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, akikataa kuthibitisha au kukanusha kukamatwa kwa padri huyo, Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu amethibitisha uwepo wa tukio hilo alilosema “ni baya linalofedhehesha”.

Tukio hilo ambalo ni la kwanza kusikika likifanywa na kiongozi wa dini mkoani Kilimanjaro, huku likihusisha idadi kubwa ya wanafunzi, limeibua taharuki kwa wazazi na walikuwa wamejipanga kuandamana kwenda kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wananchi hao walikuwa wamepanga kuandamana kwenda kwa Waziri Mkuu aliyekuwa mgeni rasmi katika Siku ya Amani Duniani ambayo kitaifa ilifanyika mjini Moshi, ili kupaza sauti zao kutokana na kigugumizi cha kukamatwa kwa padri huyo.

Baada ya polisi kupata fununu za wazazi kujipanga kuandamana na mabango kwenda kwa Waziri Mkuu, ndipo jioni ya Septemba 20, siku moja kabla ya kiongozi huyo kuwasili mkoani Kilimanjaro, walikwenda kumkamata.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alipotafutwa juzi ofisini kwake kuzungumzia uwepo wa tukio hilo, alikataa kuthibitisha au kukanusha kukamatwa kwa padri huyo zaidi ya kusema wanaendelea kuchunguza tukio hilo.

“Siwezi kusema kama tumemkamata au hatujamkamata, ila suala hili tunaendelea kulichunguza ili kujua ukweli wake, kwa sababu tuhuma hizi zinaelekezwa kwa kiongozi wa dini, hatuwezi kukurupuka kutoa taarifa,” alisema Maigwa.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, zinadai kuwa baada ya wazazi, kubaini watoto wao kufanyiwa vitendo hivyo, walitoa taarifa hizo kwenye vyombo husika ikiwemo uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi na Polisi.

Jina la padri huyo na kituo chake cha kazi tunavihifadhi kwa sasa kwa sababu za kimaadili, hasa kwa kuwa hatujapata upande wake wala vyombo vinavyomshikilia.

Jana, gazeti hili lilimtafuta kwa simu Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Ludovick Minde na baada ya kuulizwa taarifa za padri huyo, alisema wapo katika kipindi cha sala, hivyo asingeweza kuzungumza chochote kwa wakati huo (ilikuwa saa 7:12 mchana).

Ilipofika saa 10 jioni Mwananchi, lilimpigia tena simu Askofu Minde ambapo ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi kuhusu tukio hilo, Mkuu wa mkoa Babu alisema tukio hilo lipo na kwamba ameviagiza vyombo vya usalama kwamba mtu yeyote atakayekamatwa kwa matukio hayo na ushahidi upo, hakuna kurudi nyuma wanapaswa kuchukuliwa hatua kali.

“Katika tabia mbaya zisizo za watu waliostaarabika ni hizo, inaonekana mkoa wetu umezidi kuwa na matukio kama haya. Naviagiza vyombo vya usalama kwamba mtu yeyote atakayekamatwa na ushahidi upo hakuna kurudi nyuma,” alisema RC Babu.

“Kwa sababu haiwezekani kiongozi wa dini kama huyo afanye mambo kama hayo yanayofedhehesha hata waumini wake. Mambo kama haya kwa nchi yetu ni ya kuchafua taswira ya mkoa na nchi na nitaomba mahakama impe adhabu kali,” alisema.


Hali ilivyo kanisani

Mwananchi lilifika katika kanisa analohudumu padri huyo na kukuta ofisi zimefungwa, lakini wahudumu waliokuwepo walidai padri huyo aliongoza ibada Jumapili Septemba 18 na baada ya hapo alienda kwenye mafungo.

“Baada ya misa ya Jumapili aliondoka kwenda mafungo na bado hajarudi, lakini Jumapili ijayo (leo) anaweza kuwepo, kama mnamuhitaji mnaweza kuja kumuona,” alisema mmoja wa wahudumu kanisani hapo ambaye hata hivyo hakutaka kutaja jina lake.

Vilevile, Mwananchi lilizungumza na wananchi wa kada mbalimbali wakiwamo madereva bodaboda wa eneo hilo, ambapo walionyesha kulifahamu suala hilo na kueleza kusikitishwa na kitendo kinachodaiwa kufanywa na kiongozi huyo.


Tukio limetuumiza

Mmoja wa wazazi wa watoto wanaodaiwa kufanyiwa kitendo hicho, alisema kitendo hicho kimemuumiza na kimemfanya apoteze imani kwa kuwa kiongozi wao huyo walimuamini na watoto walimchukulia kama baba yao.

Akisimulia namna alivyofahamu tukio hilo, alidai alipigiwa simu na mtu mmoja akimtaka amchunguze mwanaye kwa kuwa wapo watoto wanaodaiwa kubakwa na padri huyo na mwanaye ni miongoni mwa waliotajwa na wenzake.

“Mwanangu anasoma mafundisho kanisani hapo, nilipopata taarifa hizo, nilimbana akanieleza kuwa amekuwa akiingiliwa na padri huyo tangu Januari mwaka huu,” alisema mzazi huyo ambaye aliomba jina lihifadhiwe.

“Aliniambia wanapokwenda mafundisho, huambiwa waingie ofisini kuungama ambapo huingia mmoja mmoja na ndipo huwafanyia ukatili huo na kuwaambia kuwa wasiwe na shida na wamchukulie kama baba yao,” alieleza mama huyo.

“Taarifa hiyo iliniumiza sana, na ndipo nilipoenda kutoa taarifa kanisani na baadaye polisi, ambapo watoto ikiwemo wa kwangu walipelekwa hospitali ya Mawenzi na kubainika ameingiliwa, jambo ambalo mpaka sasa linaniumiza.”

“Kibaya zaidi baada ya kumbana na kunieleza ukweli, aliniambia baada ya kufanyiwa ukatili huo, hupewa Sh3,000 hadi Sh5,000 ambazo huenda nazo shule na sikuwahi kujua haya, mpaka nilipombana baada ya kuambiwa nimchunguze”.

Mzazi mwingine alisema hawezi kuzungumza kwa undani kuhusiana na tukio hilo kwa kuwa limemuumiza moyoni na limemuathiri mwanaye, kutokana na jamii inayomzunguka kufahamu unyama huo.

“Tukio hili limeniumiza sana, maana mwanangu bado ni mdogo amefanyiwa unyama na ukatili huo na aliyefanya ni kiongozi wa dini tuliyemuamini na hata watoto walipokwenda kanisani hatukupata shaka.”

Baadhi ya wananchi katika eneo hilo, walieleza tukio hilo limeibua taharuki kubwa na kuchafua hali ya hewa, kutokana na kudaiwa kufanywa na kiongozi wa kiroho ambaye wanasema ukimtazama ni mtu mnyenyekevu na asiyedhaniwa kufanya unyama huo.

“Watoto waliofanyiwa ukatili huu wameathirika sana, kwani wapo wanaosoma shule za hapa jirani na wanafahamika na baada ya tukio hili hawawezi kwenda shule kwa sababu ya kunyooshewa vidole na wenzao,” alisema.

Mkazi mwingine wa eneo lilipo kanisa hilo, alisema, “jambo hili limetushtua sana wananchi na baadhi ya wazazi tunaambiwa tayari wamewasitisha watoto wao kwenda mafundisho. Tunaiomba Serikali ilifanyie uchunguzi wa kina suala hilo ili kubaini ukweli wake,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti mmoja wa kitongoji jirani na wananchi hao, alikiri kupata taarifa za watoto hao kufanyiwa ukatili huo na kwamba vyombo vya dola likiamo Jeshi la Polisi vinaendelea kulichunguza, hivyo viachwe vifanye kazi.

“Nikiwa mtaani hapa, nilipata taarifa za watoto 10 kufanyiwa ukatili na kiongozi huyo wa dini, naambiwa wazazi tayari walitoa taarifa kwa uongozi wa kanisa na polisi na tayari vyombo husika vimeanza kulichunguza,” alisema.

Matukio ya udhalilishaji wa kingono kwa watoto yanazidi kushika kasi na uchunguzi unaonyesha ndugu, walimu na viongozi wa dini hushiriki.