Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi Dar yatoa onyo vurugu baada ya ibada KKAM

Muktasari:

  • Juni 29, 2025 baadhi ya waumini waliotoka kwenye ibada katika Kanisa la KKAM lililo jirani na makao makuu ya Kanisa la Ufufuo na Uzima, Ubungo Kibo, Dar es Salaam walitawanywa na polisi walipojaribu kuingia barabarani wakiwa na mabango.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetoa onyo kali kwa kikundi cha watu ambao wamekuwa wakitoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Afrika Mashariki (KKAM) kwa nia ya kuingia barabarani kufanya vurugu.

Onyo hilo limetolewa leo Jumamosi Julai 5, 2025 na Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala ya usalama.

Ingawa Kamanda Muliro hakuwazungumzia, lakini waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima wamekuwa wakitawanywa na polisi mara kadhaa tangu Juni 2, 2025, Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa alipotangaza kulifuta kanisa hilo.

Hatua hiyo ilielezwa ni kutokana na kukiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Tayari kanisa hilo, limefungua kesi Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dodoma kupinga uamuzi huo.

Juni 29, 2025 baadhi ya waumini hao waliotoka kwenye ibada katika Kanisa la KKAM lililo jirani na makao makuu ya Kanisa la Ufufuo na Uzima, Ubungo Kibo, Dar es Salaam walitawanywa na polisi walipojaribu kuingia barabarani wakiwa na mabango. Baadhi yao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.

Kamanda Muliro amesema eneo la Ubungo Kibo kwa wiki mbili zilizopita za Juni, 2025 kumejitokeza kundi la watu ambao wamekuwa wakitoka kwenye Kanisa la KKAM wakiwa na mabango baada ya ibada kumalizika.

“Kundi hilo limekuwa likitoka na mabango baada ya ibada wakati wenzao  wakitawanyika kwa amani kuendelea na kazi zingine, wao huanza kupiga kelele na kutaka kuingia barabarani  kwa nguvu kwa lengo  la kufanya vurugu,” amesema na kuongeza:

“Ieleweke wazi kuwa, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu halikatazi wala kupinga watu kuabudu kwenye maeneo yao yaliyo rasmi kisheria. Lakini pia ikumbukwe, Jeshi la Polisi pia linao wajibu wa kusimamaia haki za watu wengine kwenye maeneo mengine.”

Kwa sababau hiyo, amesema Jeshi la Polisi linawatahadharisha watu hao kutoa onyo kali kuwa halitaruhusu kundi hilo kuendelea na mipango ya vurugu na uvunjifu wa amani kama ambavyo wamekuwa wakijaribu kufanya siku za hivi karibuni.

Amesema aendapo watathubutu au kujaribu kufanya hivyo, watajikuta kwenye msuguano mkali wa usimamaizi wa sheria wa jeshi hilo.

“Narudia tabia ya kundi lile wakimaliza ibada wenzao wakitawanyika kwa amani  wao wakaanza kupiga makelele na kutaka kuingia barabarani kwa nguvu, Jeshi hili la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawatahadharisha na kuwapa onyo kali kwamba watajikuta kwenye  msuguano mkali wa usimamizi wa sheria na jeshi hili,” amesema.

Kamanda Muliro amesema jeshi hilo linawataka wananchi wengine wema kuendelea na ibada katika maeneo yaliyo rasmi kisheria bila kuwa na malengo ya kuvunja sheria za nchi.

Alipoulizwa nini kinaendelea kwa watu waliokamatwa Juni 29, Kamanda Muliro alijibu bado taratibu za kisheria zinaendelea dhidi yao.

Katika tukio la Jumapili Juni 29, waumini hao walitawanywa kwa mabomu ya machozi walipoanza kuingia barabarani wakiwa na mabango.

Kamanda Muliro alisema: “Tumewakamata 33 na tunawahoji ili kujua wana kitu gani kwa sababu kwenye hilo kanisa wamesali vizuri na sisi tunajua haki za kuabudu na ndiyo maana hatukuwafanya chochote.”

Awali, majuma yaliyopita waumini hao walifanya ibada barabarani eneo la katikati ya Ubungo Maji na Kibo, jirani na yalipo makao makuu ya kanisa lao.