Hayati Karume unayajua haya? Nisikilize...

New Content Item (1)

Hisia zangu zipo Kisiwandui, Zanzibar, ilipo Ofisi Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Naitazama sanamu iliyosanifiwa vema. Imebeba taswira ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume.

Naitazama sanamu kwa mbele, nyuma yake ndiyo Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar. Pembeni ya jengo la ofisi, kuna kaburi la Karume.

Kalenda ya Gregory inasema leo ni Aprili 7, 2024. Imetimia miaka 52 kamili tangu Karume alipouawa.

Miaka 52 ni siku 18,993. Mengi yametokea ndani ya siku hizo. Angalau jambo moja ambalo linatosha kuthamini, kushukuru na kutambua dhamira njema ya Karume ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kisha ikazaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ananisikia? Imani ya maisha baada ya kifo inanipa uhakika kuwa Sheikh Karume ananipata vema. Na ujumbe wake ni huu; yapo mengi ya kusahau lakini siyo kuimarishwa kwa undugu wa Watanganyika na Wazanzibari, baada ya kuzaliwa Tanzania.

Siwezi kuchelewa kumhakikishia Karume kuwa ndoto yao ya kujenga undugu imara baina ya Watanganyika na Wazanzibari bado ipo hai. Tanzania imeendelea kuwa moja. Changamoto ni nyingi chini ya jina la “Kero za Muungano”, ila zinatatuliwa taratibu na zingine mpya zinaibuka kwa sababu maisha yanaendelea na mahitaji ya wakati ni tofauti. Angalau hilo ni uhakika.

Sheikh Karume, kifo chako bado ni utata wa kuendelea. Sababu ya wewe kuuawa ilikuwa nini? Nadharia kuwa Luteni wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Humud Mohamed Humud, alihusika na mchoro wote ili kulipiza kisasi cha baba yake, imebaki inaelea.

Ni kweli, baba wa Humud aliwekwa kizuizini baada ya Mapinduzi ya Zanzibar. Inaelezwa ni kwa agizo lako wewe Sheikh Karume. Kwamba baba wa Hamud alifia gerezani. Hamud aliapa kulipa kisasi. Ndipo uliuawa. Ni nadharia.

Ipo nadharia ya kimapinduzi. Eti, waliokuua walitaka kupindua Serikali. Hii inaelea pia. Zanzibar tayari ilishakuwa sehemu ya Tanzania, ingewezekana vipi kufanikisha mapinduzi ya aina hiyo ikiwa Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu na mkuu wa dola zote za Tanganyika na Zanzibar pamoja na mipaka yake?

Pengine ungebaki hai kwa siku kadhaa, ungefunua kinywa kuelezea kiini na asili ya shambulio la risasi dhidi yako. Bahati mbaya, yale mapigo nane ya risasi yalisimamisha moyo wako palepale, mbele ya bao ulilokuwa unacheza. Dua njema ni nyingi kwa ajili yako. Uondolewe adhabu za kaburi. Upate hifadhi njema kwa Mwenyezi Mungu.

Sheikh Karume, najua unafahamu, ila siyo vibaya kukujulisha tena kuwa baada ya kifo chako, aliyeingia madarakani ni Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi. Uongozi wake ulidumu kwa miaka 12, kabla ya mwaka 1984, kulazimishwa kujiuzulu. Jumbe alitaka Muungano uwe wa Serikali tatu. Akaonekana alitaka kuwagawa Watanzania.

Msimamo wako ni upi Sheikh Karume? Je, Jumbe alikuwa sahihi au alikwenda kinyume na maono yako kuhusu Muungano? Unadhani agenda ya Jumbe ingefanikiwa Muungano ungekuwa bora zaidi au ulivyo sasa ndivyo unapenda uwe? Tafadhali Sheikh Karume, nitembelee hata usingizini, uniambie hisia zako.

Baada ya kifo chako, ilipita miaka 27, mshirika wako mkuu wa Muungano, Mwalim Nyerere, alifariki dunia. Hakikuwa kifo cha risasi kama chako, bali mauti asilia.

Aliumwa na kulazwa Hospitali ya Mtakatifu Thomas, London, Uingereza. Oktoba 14, 1999, Mwalimu alivuta pumzi ya mwisho.

Watu walikuwa na hofu baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere. Hofu ya kuvurugika umoja wa kutaifa na kusambaratika kwa Muungano. Rais wa Tanzania aliyekuwa madarakani, Benjamin Mkapa, alikutaja wewe (Karume) na Mwalimu Nyerere, kuwa mlishajenga misingi imara ya Utanzania. Nchi ilibaki salama.

Misingi hiyo ndiyo ambayo imewezesha mabadiliko ya marais sita, Tanzania na nane Zanzibar.

Bila shaka hili linakufariji huko ulipo. Nakuhakikishia, utaendelea kuenziwa na vizazi vingi vijavyo vya Zanzibar na Tanzania.

Sheikh Karume, unajua tangu mafanikio ya Mapinduzi hadi kifo chako, Zanzibar haikuwahi kufanya uchaguzi?

Miaka minane tangu kifo chako, yaani mwaka 1989, Zanzibar ilirejea mkondo wa uchaguzi na demokrasia. Japo ulikuwa wa chama kimoja, ila Wazanzibari walipiga kura kuchagua viongozi wao. Jumbe alipolazimishwa kujiuzulu, Ali Hassan Mwinyi, alipitishwa kuwa Rais wa Zanzibar. Unamkumbuka?

Ni yuleyule kijana uliyemteua kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, akitokea kuwa Mkuu wa Chuo cha Ualimu Zanzibar, mara baada ya Mapinduzi, Januari 12, 1964.

Mwinyi aliandika kitabu “Mzee Rukhsa; Safari ya Maisha Yangu.” Ndani yake ameeleza imani kubwa uliyokuwa nayo kwake na kwa vijana wasomi wachache wa wakati huo. Uliwateua kwenye nafasi kubwa serikalini, halafu ukawaambia: “Nendeni mkajifunze humohumo.”

Ni Mwinyi huohuyo uliyemteua kuwa Naibu Mkurugenzi wa Chama cha Wakulima wa Karafuu (CGA), halafu mwaka 1970, ukampendekeza kwa Mwalimu Nyerere, amteue kuwa Waziri kwenye Serikali ya Muungano. Basi baada ya Jumbe, Mwinyi aliongoza Zanzibar.

Halafu Mwinyi akawa Rais wa Pili wa Tanzania, baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka. Kijana wako mwenyewe uliyemkuza kiuongozi na kisiasa, akawa Rais wa Zanzibar, halafu Rais wa Tanzania. Ikupe picha kuwa baada ya kifo chako, nchi haikushikwa na walowezi wala wasiotambulika misingi yao. Matunda yako yameendelea kustawi kwenye Taifa.

Hili pia la kutambua thamani yako; hukuwa mbaguzi. Mwinyi ni uthibitisho. Mtoto kutoka Mkuranga, Pwani, Tanganyika. Aliyekulia na kusomea Zanzibar.

Baada ya Mapinduzi, hukumuuliza asili yake, bali ulimteua akafanye kazi aijenge Zanzibar. Ukampendekeza kuwa waziri. Wewe ni alama njema ya maisha bila ubaguzi.

Mwinyi alipochaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, aliyechukua kijiti Zanzibar ni Idris Abdul Wakil. Huyu haimbwi, ila aliweka rekodi ya kipekee kwa historia ya viongozi Afrika. Wakil, alipomaliza muda wake, aliomba asiongoze ili awaachie vijana.

Afrika ni Wakil na Nelson Mandela, Afrika Kusini, ndiyo waliachia urais baada ya muhula mmoja ili kupisha nguvu mpya. Sheikh Karume, hutasahaulika kwa juhudi za kusomesha Wazanzibari bure. Ulitaka waelimike waje waendeleze nchi yao. Fikiria, ulipofariki dunia, mtoto Hussein alikuwa na umri wa miaka mitano. Huyo Hussein ndiye Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Nane wa Zanzibar.

Siku ile unauawa Kisiwandui, kuna binti alikuwa na umri wa miaka 12, akimaliza mwaka wa mwisho, Shule ya Msingi Mahonda, Zanzibar.

Huyo uliyemwacha akiwa binti, hivi sasa siyo tu ni mama na bibi, bali ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ameweka rekodi ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke Afrika Mashariki. Jina lake ni Samia Suluhu Hassan.

Bila shaka sasa unanielewa nilipokwambia mambo mengi yametokea ndani ya siku 18,993, ambazo umeipa kisogo dunia.

Vita ya Kagera na Uganda, Tanzania ilikomesha uchokozi wa kiuvamizi wa Idi Amin Dada, ikamwondoa madarakani. Ajali za ndege na magari barabarani, meli baharini na ziwani, mafuriko na matetemeko ya ardhi, yametokea Tanzania kwa nyakati tofauti.

Taifa linafuta machozi na kuganga yajayo. Watanzania husimama pamoja palipo na misiba.

Sheikh Karume, umoja huo wa Watanzania kwenye misiba, hauhusu madhila ya mauaji Januari 26 na 27, Zanzibar, hususan Pemba. Kovu kubwa lilitengenezwa kwa matukio hayo. Wazanzibari wakageuka wakimbizi. Walikimbia nchi kuokoa maisha yao. Sababu ni siasa. Julai Mosi 1992, Tanzania iliingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa. Mwaka 2000, mwanao Amani, alichaguliwa kuwa Rais wa sita wa Zanzibar.

Amani na kijana uliyemwacha akiwa mwalimu, Seif Sharif Hamad, walichagiza mabadiliko makubwa, ikiwemo kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Walitaka Zanzibar ibaki pamoja, licha ya tofauti na itikadi za kisiasa.

Pamoja na hivyo, ukikaribia uchaguzi Wazanzibari hawazikani. Hili bila shaka halikupendezi. Wakati wako ulikuwa na sera ya mgawo sawa wa fursa kwa Pemba na Unguja. Sera yako ilikuwa kila kilichofanyika Unguja, kitekelezwe Pemba kwa ubora na ukubwa au idadi sawa.

Hivi sasa, Pemba na Unguja ni visiwa pacha visivyo na mfanano wowote. Pemba haiperembi tena. Imechoka. Japokuwa maghorofa ya Kengeja, Chakechake, Machomane, Wete, Micheweni na Konde, yapo Pemba, kama ilivyo kwa Michenzani, Unguja.

Ulitaka maghorofa ya Michenzani na yale ya Pemba yakaliwe na Wazanzibari masikini, hivi sasa hakuna hohehae anaweza kumiliki nyumba (apartment) Michenzani.

Ulipokufa huduma nyingi za kijamii zilikuwa bure, sasa kila kitu fedha. Sheikh Karume, jinsi ulivyo ungeshangaa leo Wazanzibari wanatibiwa kwa fedha na maji wanauziwa.

Ungefurahi utalii unavyoongezeka na mwingiliano wa Wazanzibari na Watanganyika ulivyo mkubwa. Hakuna hati ya kusafiria kwa Mtanganyika kuzuru Zanzibar. Pumzika kwa amani huko uliko, huku maisha yanaendelea na Muungano mwaka huu utatimiza miaka 60.


Huyu ndio Karume

Sheikh Abeid Amani Karume alizaliwa Unguja Agosti 4, 1905 akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watano ya Amani Karume na Bibi Amina binti Kadir (Amina Kadudu).

Miongoni mwa watoto wote watano, ni Abeid Karume pekee aliyebaki hai baada ya nduguze kufariki dunia kutokana na maradhi mbalimbali na hivyo kubaki yeye peke yake. Baba yake Abeid alifariki dunia mwaka 1909 wakati huo yeye akiwa na umri wa miaka minne.

Mwaka 1913 alikwenda kuishi na mjomba wake mjini Unguja aliyekuwa Sajenti katika Jeshi la Polisi la King African Rifle (KAR). Kwa bahati mbaya muda wake wote wa masomo ulikuwa miaka mitatu. Akiwa mjini Zanzibar Abeid Karume alipata marafiki kadhaa na kuvutiwa mno na harakati za bandari ya Zanzibar.

Kwa wakati huo bandari ya Zanzibar ilikuwa kubwa Afrika Mashariki na kituo kikuu cha biashara katika Afrika Mashariki kwa sababu meli za mataifa ya nje hasa Marekani, Uingereza, Ufaransa na Italia zilitia nanga bandarini hapo kupakia na kupakua bidhaaa.

Kwa kuwa alipenda kazi ya ubaharia, Abeid alijumuika na watoto kadhaa waliofuata ajira ya muda bandarini. Kama walivyokuwa watoto wengine kama hao, naye alipata ajira ya muda. Ingawa mwaka 1919 alituma barua ya maombi ya kazi, alikataliwa kutokana na umri mdogo.

Karume alijiunga na timu ya soka ya New Generation ambayo aliichezea na baadaye kuwa nahodha wake. Mwaka 1920 alikubaliwa kuwa baharia katika meli ya Golden Crown iliyobeba abiria na mizigo kati ya bandari ya Zanzibar, Dar es Salaam, Pemba, Tanga, Mombasa na Mikindani Kilwa.

Baadaye alishuka katika meli hiyo na kufanya kazi katika meli nyingine iliyoitwa Cheko. Kwa bahati mbaya, meli hiyo iligonga mwamba na kuvunjika huko Kimbiji, nje kidogo ya Dar es Salaam lakini watu wote walinusurika.

Kazi ya ubaharia ilimpa tija Karume, kwani alinunua nyumba na viwanja kila alipopata nafasi ya kwenda nyumbani. Kwa muda wote huo Karume alifanya kazi katika meli zilizopata leseni ya kufanya kazi katika mwambao wa Afrika Mashariki.

Akifanya kazi katika meli ya kampuni ya British Indian Steam Navigation Company ya Uingereza, alikaa nje kwa miaka mitatu, 1922—1925. Hadi wakati huo alikuwa ameshatembelea nchi kadhaa kama Japan, Comoro, Madagascar, China, Singapore, New Zealand, Uingereza, Marekani, Canada, Ufaransa, Ubelgiji, India, Ureno, Hispania, Arabuni, Italia na Ugiriki, na huko ndiko alijifunza mengi.

Mbali ya kuanzisha chama cha mabaharia, pia Abeid alikuwa muasisi wa Jumuiya ya Waafrika iliyoitwa African Dancing Club katika miaka ya 1940 na baadaye Afro-Shirazi Union Februari 5, 1957 baada ya kuunganishwa vyama vya Shirazi Association na African Association ambacho baadaye kilikuja kujulikana kama Afro-Shirazi Party.

Miongoni mwa wapigania uhuru waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa TANU, Mwalimu Julius Nyerere. Karume alichaguliwa tena kuwa mjumbe wa baraza la kutunga sheria katika uchaguzi wa pili wa Januari, 1961, katika jimbo la Jang'ombe kwa tiketi ya ASP.

Baada ya kuundwa Serikali ya Waziri Mkuu Muhammed Shamte kufuatia uchaguzi wa 1963, Karume aliteuliwa kuwa kiongozi wa upinzani katika baraza la kutunga sheria.

Wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964, Karume alikuwa mwenyekiti wa kamati ya watu 14 waliotayarisha Mapinduzi hayo kwa siri. Na baada ya mapinduzi kufanikiwa, Zanzibar na Tanganyika ziliungana Aprili 26, 1964 kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yeye akawa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Aprili 7, 1972 Karume aliuawa kwa kupigwa risasi katika mazingira na sababu za kutatanisha. Kutokana na umaarufu wa Karume katika visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, ni jambo lisilowezeka kuandika historia ya Zanzibar bila kumtaja Abeid Amani Karume. Na ndio sababu Aprili 7 ya kila mwaka, siku kama ya leo tunaadhimisha kumbukumbu yake kumuenzi.