Chimbuko na maisha ya Karume nje ya urais

Katika mfululizo wa hadithi zihusuzo miaka ya 60 ya mapinduzi Zanzibar, kuanzia Novemba 13 tulifanya uchambuzi kuhusu Zanzibar na historia yake pamoja na dondoo za marais waliowahi kuviongoza visiwa hivyo.

Kuelekea Januari 12, 2024 siku ambayo Mapinduzi yatatimiza miaka 60, tutakuletea uchambuzi wa kila awamu ya utawala wa kisiwa hivyo na kwa kuanza tutaangazia historia ya Rais Abeid Karume, chimbuko lake na maisha yake nje ya urais

Ukimzungumzia Rais Abeid Karume, simulizi za maisha yake zina utata. Kwa mfano, wapo waliosema alizaliwa Kiongoni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar na mama yake ni Amina Kadir (Kadudu) na kuwa ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watano ya Bwana Amani Karume.

Lakini wapo waliodai alitokea Malawi na kufika Zanzibar akiwa mdogo na wengine wakidai wazazi wake walitokea ile iliokuwa ikiitwa Rwanda-Urundi (sasa ni nchi za Rwanda na Burundi).

Hata hivyo, taarifa hizo zilizowahi kuandikwa na vyombo vya habari likiwemo gazeti hili, hazijawahi kuthibitishwa, yamebakia kuwa maneno tu ya watu.

Katika moja ya makala zilizoandikwa juu yake, Mwandishi mkongwe, Salim Said Salim anasimulia: “Mke wa mwanzo wa Mzee Karume niliyemjua kwa karibu ni Fatma Gulamhuseein (mama Fatma Karume) tokea nilipoanza kupata fahamu zangu mwanzoni mwa miaka ya 1950.

Nilimuona Mzee Karume kuwa ni rafiki wa kila mtu mtaani licha ya tofauti za kisiasa, lakini zaidi kwa watoto ambao walipenda kuazima baiskeli yake (mimi nikiwa mmoja wao).

Kila mtoto wa kiume alimwita ‘shabbab’ na wa kike “mchumba wangu”.

Kwa bahati mbaya, licha ya kukaa naye mara nyingi na hata aliponifundisha kucheza karata na dhumna, sikuwahi kumuuliza juu ya habari za wazee na ndugu zake, ijapokuwa nilipenda kupata habari na kuwa mwandishi tangu nikiwa shule ya msingi.

“Mzee Karume alipendeza kukaa mtaani kwa kuwa mtu wa mikasa. Siku zote jua lilipochomoza alikuwa akipiga soga katika baraza ya kahawa mbele ya nyumba yetu.

Miongoni mwa aliokuwa anazungumza nao alikuwa baba yangu, mjomba wangu Suleiman, Shebe “Madawa”, Rashid Mbarouk, Muhsin na Aboud Maalim, Abeid (muuza vifuu), Abaa aliyekuwa fundi wa baiskeli na mzee mmoja fundi mwashi, Mwinjuma aliyemchukua Ikulu alipokuwa Rais.

Jambo lisilokuwa na ubishi ni kuwa Mzee Karume alizaliwa 1905 na kupata elimu ya msingi kuanzia katikati ya miaka 1910.

Baada ya masomo alikuwa baharia katika meli za mizigo na kila aliporudi safari aliniletea paketi za peremende, chokoleti na biskuti.

Alijiunga na chama cha mabaharia wa Uingereza kilichokuwa na makao yake makuu Liverpool, Uingereza.

Sikushangaa kumfahamu ni mpenzi wa klabu ya Liverpool wakati wazee wengine mtaani walikuwa mashabiki wa Blackpool, Leeds, Everton, Westham na Shefield United.

Vilevile alikuwa mwanachama wa Yanga ya Dar es Salaam na kwake ukumbini zilikuwepo na picha alizopiga na wazee wa Yanga katika miaka ya 1948 na baadaye.

Alipokuwa Rais alitoa fedha kusaidia ujenzi wa Klabu ya Yanga iliyopo Jangwani na mke wake (mama Fatma) mpaka leo hafichi mapenzi yake kwa klabu hii.

Siku moja tulipokuwa uwanjani kuangalia mpira, nilimuona akisherehekea goli maridadi lilioizamisha timu yake ya Kisimamajongoo.

Aliipenda klabu ya Liverpool kwa sababu alipokuwa baharia meli yake ilifika sana katika bandari hiyo ambayo mji wake una historia ndefu ya Waafrika kuishi hapo zaidi ya karne nne ziliopita.

Mzee Karume aliiona Liverpool ni timu ya mabaharia wenzake.

Mapenzi yake ya mchezo ndio yaliyomfanya mara baada ya Mapinduzi kuipatia Zanzibar uwanja wa Amani uliojengwa ukiwa ndio bora zaidi Afrika Mashariki na Kati.

Alisisitiza amani katika michezo wakati wote na kusema hapana haja ya uhasama na labda ndio maana alifurahia hata timu aliyoipenda ilipofungwa bao safi.

Watu wanaomfahamu marehemu hawakushangazwa siku moja katika mwaka 1969 au 1970 alipokuwa jukwaa kuu kuangalia mchezo kati ya Mwadui na Miembeni ya Zanzibar alipoamuru uvunjwe kabla ya muda kwa vile aliona Mwadui walikuwa wanacheza rafu.

Alitoa amri kwa timu ya Mwadui kuchukuliwa uwanjani na polisi kupelekwa moja kwa moja uwanja wa ndege na kuondoka Zanzibar.

Aliipiga marufuku timu hiyo kutembelea Zanzibar na haikufika Visiwani tena wakati wa uhai wake.

Alikuwa akisema “soka ni mchezo wa waungwana na ni watwana ndio wanaocheza rafu”.

Kutokana na kutopenda watu kuumizana katika michezo alipiga marufuku ndondi Zanzibar na amri hii imeondolewa Agosti mwaka 2023 baada ya Rais wa sasa, Dk Hussein Mwinyi kuruhusiwa mchezo huo baada ya kuzuiwa kwa zaidi ya miaka 50.

Siku moja, nikiwa na mwandishi mwenzangu maarufu hapo zamani, Mohamed Karim (baba wa mtangazaji Farouk Karim wa ITV), nilimuuliza kwa nini hapendi ndondi. Jibu yake lilikuwa fupi, lakini la kukata na shoka.

“Eboo! Wee Shtobe (jina langu la utani nilipokuwa mdogo kwa vile nilipenda kupigana bila ya sababu) unapigana na mwenzako ili iwe nini. Ukitaka kupigana pigana na tumbo lako na sio na mwenzako”.

Wakati timu ya Zanzibar ilipopiga kambi kwa michuano ya mwisho ya Kombe la Gossage 1966 (sasa Chelenji) ilipofanyika Zanzibar, nilimuona Mzee Karume akiitembelea timu hiyo asubuhi na jioni.

Aliangalia hali ya malazi na chakula na kutazama mazoezi na hata kutoa maelekezo kwa wachezaji.

Pia, alikuwa hodari wa kucheza dhumna, bao na karata na tulipokuwa tukirusha kishada, hakupenda kile kilichokuwa na mkia kwa vile hali hiyo ilionyesha kukosekana ustadi katika kukitengeneza.

Mara nyingi alifika kuangalia mpira bila ya taarifa mapema, hata timu ndogo zilipocheza uwanja wa Mao Dzedung.

Baadhi ya wakati alikuta jukwaa kuu na kukuta wamekaa watoto. Alichofanya ni kukaa nao kuangalia mchezo kama na yeye ni mtu wa kawaida.


Kesho usikose kufuatilia mwendelezo wa hadithi za Abeid Karume, tukiangazia zaidi utawala wake wa Zanzibar katika siku za mwanzoni sanjari na matukio makubwa yaliyojiri.