Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Kamishna wa utalii asimulia safari ngumu ya utalii Zanzibar

Muktasari:

  • Zikiwa zimebakia siku chache kabla ya Zanzibar kuadhimisha Sherehe za Mapiduzi, muasisi katika sekta ya utalii Zanzibar Walid Fikirini amesimulia mageuzi ya sekta hiyo kisera pamoja na hatua zilizofanyika kuimarisha usalama sekta ya utalii miezi kadhaa baada ya mapinduzi hayo.

Dar es Salaam. Zikiwa zimebakia siku 58 kabla ya Zanzibar kuadhimisha Sherehe za Mapiduzi, muasisi katika sekta ya utalii Zanzibar Walid Fikirini amesimulia mageuzi ya sekta hiyo kisera pamoja na hatua zilizofanyika kuimarisha usalama sekta ya utalii miezi kadhaa baada ya mapinduzi hayo.

 Walid aliyetumikia miaka 37 katika sekta hiyo, alianza kufanya kazi ya mhudumu wa mapokezi katika Hoteli ya Zanzibar chini ya Serikali ya awamu ya kwanza ya rais Sheikh Abeid Aman Karume hadi alipostaafu awamu ya sita chini ya Aman Abeid Aman Karume, mtoto wa mwasisi wa kisiwa hicho.

Akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Shirika la Utangazaji wa Zanzibar (ZBC) leo Novemba 13, 2023, Katibu huyo mtendaji mstaafu wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar amesema wakati sekta hiyo inaanza haikuwa na hoteli zenye vitanda hata 100 vya utalii huku utalii ukiwa na sura ya kidplomasia.

Mahojiano hayo yanayoakisi mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964 yanafanyika wakati Jukwaa la Fikra la Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) likishirikiana na ZBC kueleza changamoto, fursa na mafanikio kutoka miaka 60 ya mapinduzi hayo na ‘Zanzibar tuitakayo miaka 60 ijayo’. 

Ushirikiano huo unaohusisha uandaaji na uchapishaji wa maudhui tofauti yanaendeshwa na kampeni ya pamoja ya siku 60 iliyoanza leo na ukomo wake itakuwa ni kilele cha mapinduzi hayo Januari 12, 2024.

Katika utekelezaji wa kampeni hiyo Walid amezungumza na ZBC kwa kina kuhusu safari ngumu ya ukuaji wa Sekta hiyo iliyoongezeka kutoka kwa kasi katika awamu nane za uongozi wa SMZ.

Walid amesema mwaka 1970, aliteuliwa kuwa meneja wa utalii katika Shirika la Furaha ya Visiwani Hoteli lililohusisha Zanzibar Hoteli, Afrika House Hoteli, Rolf Club na Starehe Club baada ya kutoka kozi fupi iliyotolewa Tanzania bara aliyokwenda mwaka 1969 na wenzake watano.

Mbobezi huyo wa masuala ya utalii amepongeza uhai wa mapinduzi hayo kwa miaka 60 chini ya Dk Hussein Ali Mwinyi, akisema matumaini ni makubwa ya kiuchumi na maendeleo kupitia sekta hiyo.

Akisimulia, Walid amesema mwaka 1964 baada ya mapinduzi, Rais Karume aliunda sera iliyoanzisha mashirika ya umma ikiwamo la utalii ambayo yatakuwa na sura ya kukuza mahusiano ya kimataifa.

Mwaka 1965, Serikali ikaunda Shirika la Utalii kwa majukumu manne: kutoa huduma za utalii, kulinda maliasili za Zanzibar, kukuza uhusiano kimataifa na kulinda na kudumisha utamaduni wa Zanzibar.

Kwa hivyo Shirika la utalii lilikuwa namna hiyo, likapatiwa vyombo vya usafiri na hata awamu ya pili chini ya Rais Aboud Jumbe wakaendeleza kujenga Hoteli ya Bwawani mwaka 1974. Lakini Sera iliendelea kubakia vile vile kwamba utalii itakuwa chombo cha kukuza mahusiano ya kimataifa,” amesema Walid.

“Mpaka 1984/85 chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, akaomba ushauri nikashauri sera ibadilike kutoka kujenga mahusiano na kiwe chombo cha biashara na uchumi. Akakubali na sera ikabadilishwa 1984, shirika la utalii likabadilishwa pia majukumu yake na kuwa Zanzibar Tourist Corporation.”

Katika awamu hiyo, Walid amesema Rais Mwinyi akawekeza nguvu na miundombinu ikiwamo kununua mabasi 12 ya shirika la utalii kutoa huduma kwa utalii na wananchi kabla ya kuingia uchaguzi mkuu 1985 na kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa awamu ya pili huku Zanzibar ikipata Sheikh Idrisa Abdulwakil.

Alipoingia Sheikh Indris katika awamu hiyo ya nne 1985/1990 aliamua kuwekeza zaidi, huku Wazanzibari wakiwa na hawana uwezo wa kununua magari binafsi. “Kwa hiyo mabasi ya shirika yalitoa huduma ya usafiri wa umma,”amesema akifafanua: 

“Kila basi tulipewa kwa mkopo wa Sh150,000 pesa hizo zililipwa na PBZ (Benki ya Watu wa Zanzibar) ili sisi tuhesabike tumechukua mkopo PBZ, baada ya miezi sita tukalipa pesa zote.”

Baada ya kuingia awamu ya tano chini ya Dk Salmin Amour Juma 1990/2000, Walid amesema matumaini ya kukuza sekta hiyo yalianza kuonekana zaidi baada ya kuunda rasmi Kamisheni ya Utalii akiwa Katibu Mtendaji wa kwanza huku akiwezeshwa mahitaji yote waliyohitaji ili kuanza biashara ya utalii.

“Alipotuteua tukaenda kumuuliza Ikulu madhumuni ya kamisheni ni nini? Akatuambia sisi ndiyo tumwambie kamisheni itafanyaje kazi, tukampelekea taarifa ya muundo wa kamisheni na tukamuomba ofisi, vitendea kazi, nguvu kazi na vyombo vya usafiri,”amesema akifafanua:

“Kuhusu ofisi, akatuambia tuchague jengo lolote la Serikali. Kuhusu gari akatuambia ameagiza gari na zikifika tuchague sisi kabla ya kuzigawa kwa wengine.”

“Kuhusu nguvu kazi, akavunja Idara ya Utalii na wengine watakaohitajika mtauliza Idara ya utumishi. Kuhusu vifaa vingine, akatuambia tuombe Wizara ya Fedha ili kuendeleza zaidi. Idara ya Utalii tukawachukua na tukaenda jengo la Hoteli ya Amani na kuanza kazi.”

Kamishna wa utalii asimulia safari ngumu ya utalii Zanzibar

Kazi ilivyoanza

Baada ya kukabidhiwa kila ombi walilohitaji, kazi ikaanza na Walid anasema walianza kuimarisha kwanza eneo la mahusiano ya kidplomasia, ushirikiano na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na safari za nje ili kukuza chapa ya utalii wa Zanzibar.

“Tukaenda Ubalozi wa Ufaransa tukaomba utalii na wakatupatia watalaamu wawili kusaidia promosheni, tukaenda Ubalozi wa Marekani wakatupatia mtalaamu wa kuandaa mpango kabambe wa sekta ya utalii, baadaye tukafanya semina na kazi ikabakia promosheni ya kuleta watalii nchinim,” amesema akifafanua:

“Tukaenda Ujerumani, Uingereza, Itali, Marekani, Afrika Kusini mwezi Juni (1993) ambako tulifukuzwa hotelini kwa kuwa ni waafrika na tulihamia hoteli nyingine, ilikuwa mwaka mmoja kabla ya wao kupata Uhuru.”

Hata hivyo Walid amesema juhudi zilizaa matunda baada ya miezi kadhaa kupokea kundi la watu 20 Ikulu ya Zanzibar walioahidi kushirikiana kukuza sekta ya utalii.

“Kwa hiyo ilikuwa hakuna kukaa, kesho huku, mwingine huko na huku, tukaunda ushirikiano na TTB (Bodi ya Utalii Tanzania), kila walipokwenda tulikuwa naoi li kukuza utalii wa Zanzibar pia,” amesema.

Jambo lingine lililofanyika ilikuwa ni kuunda chombo cha kuhamasisha uwekezaji kuja Zanzibar hatua iliyoshawishi kasi ya ujenzi wa mahoteli.

“Hata wageni tukajua wakija watakaa wapi, baadaye ikafikia wakati Serikali ijiondoe kwenye biashara na iachie sekta binafsi, kwa hiyo shirika la utalii likavunjwa, hoteli ya Zanzibar ikabinafsishwa,”amesema.


Uzoefu wake

Baadaye alihamishiwa Shirika la Utalii na kisha kurejeshwa tena Idara ya utalii kabla ya kuundwa kamishna ya Utalii mwaka 1992 iliyopo chini ya Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kwa sasa.

“Nikachaguliwa kuwa kamishna wa mwanzo na nikatakiwa kuunda hiyo kamishna, nitaandaa muundo wa majukumu yake ikakubaliwa Serikalini ndio tukaanza kazi,”amesema.

“Hatukuwa na ofisi wakati huo, ikabidi tukae Uwanja wa Amani katika jengo lililopo pale baadaye tukahamia ofisi mpya za kukodi kwa kulipia Sh400,000 kila mwezi, muuzaji akatangaza kuiuza ndipo Serikali ikainunua nyumba ile kwa Sh200milioni, hadi sasa ndipo ofisi zilizopo.”

Amesema Shirika la Bima Zanzibar lilikosa leseni ya kimataifa kutoka Benki ya Tanzania (BoT) baada ya kuwa na rasilimali zilizokuwa chini ya vigezo kwa wakati huo.  Jengo hilo ikabidi lihesabike kuwa sehemu ya Shirika la Bima ili kufikia vigezo hivyo licha ya umiliki wake kuwa upande wa kamisheni hiyo ya utalii.


Usalama ulikuwaje?

Akizungumzia kuhusu hali ya usalama baada ya mapinduzi na mwingiliano wa watalii, Walid amesema idadi kubwa ya watalii walikuwa ni wachunguzi na wapelelezi waliotaka kufahamu uendeshaji wa Serikali ya mapinduzi.

“Kulikuwa na mambo ungeshangaa, walikubali kuvaa kanga kwa sababu ya intension (matamanio) yao na sisi tulijua hilo kwamba wengi walitaka kujua Zanzibar inakwendaje, lakini sasa utamvalisha mtalii kanga atakuelezwa?,”amehoji akitoa mfano:

“Kuna mwandishi wa Uingereza alikuja mara mbili hapa kuonana na Rais Karume baada ya mapinduzi, na maswali yake ilikuwa ni lini Zanzibar itaanzisha uchaguzi. Karume alimjibu miaka 50 ijayo, ‘ndenda zako’, ndio wengi ilikuwa hivyo.”

Hata hivyo, Walid amesema baada ya mapinduzi hadi mwaka 1966, watalii wote walisajiliwa na kulala hoteli za Serikali ili kulinda mapinduzi. Amesema mikakati hiyo imechagiza uhai wa mapinduzi hayo yanayofanyika kwa awamu ya 60


Changamoto

Kuhusu changamoto za kimaadili, Walid amesema wakati wanaanza, watalii wote walioingia Zanzibar walipewa vipande vya kanga Uwanja wa ndege, ambao walionekana kutovaa kiheshima. 

“Lakini sasa watalii wanaingia na wengine wanatembea bila nguo, kwa sasa usiende Nungwi na mtu unaemuheshimu hata Paje ukienda wageni ni wengi kuliko wenyeji, ndio ilipokuja mmononyoko wa maadili, kutokana na mwingiliano, vijana wetu wamevutika zaidi na utamaduni wa nje.”

Pili, Walid amesema kabla ya mapinduzi, hoteli kubwa za kitalii zilizofahamika kwa hadhi ya nyota tano ni Hoteli ya Zanzibar, Afrika House pamoja na nyumba chache za wageni zilizokuwa chini ya hadhi za kimataifa.

“Rais Karume aliona mbali sana kwa wakati katika kutengeneza uchumi. Baada ya kufariki, hoteli zikajengwa nyingine Pemba,” amesema.