Dk Mwinyi ataka wajiolojia kuisaida Zanzibar kutafiti maji ardhini

New Content Item (2)

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema uhitaji wa maji bado ni mkubwa kisiwani hapo hivyo zinahitajika jitihada za makusudi kufanya tafiti kubaini maji ya ardhini kusaidia upatikanaji maji safi na salama na kupunguza pengo lililopo.

Pia ameitaka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kuendeleza juhudi za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi wakishirikiana na wanajiosayansi kubaini sekta hiyo ambayo tayari taarifa za awali zinaonyesha uwapo rasilimali hiyo katika visiwa hivyo.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Novemba 9, 2023 kupitia hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shaibu Hassan Kaduara wakati wa kufungua mkutano wa Taasisi ya Jumuiya ya Wajiolejia Tanzania (TGS) ambao kwa mara ya kwanza ulifanyika Zanzibar.

“Hivyo basi Serikali inategemea Wananchi waweze kupata huduma hiyo kwa asilimia 85 kabla ya kufikia mwaka 2025, bado tunahitaji kuwatumia wanasayansi katika tafiti hizo na kubaini maji ya ardhini,” amesema Dk Mwinyi

Dk Mwinyi amesema mahitaji ya maji yanaendelea kukua kila mara na kwamba hadi kufikia Machi 2023, mahitaji ya maji yalikuwa ni lita 142 milioni kwa siku huku uzalishaji ni lita 116 milioni kukiwa na upungufu mkubwa wa maji.

“Katika hili niendelee kuagiza mamlaka ya maji Zanzibar kuwatumia wataalamu wa jiosayansi kubaini uhitaji wa maji ardhini ili kumaliza tatizo la upungufu wa maji kisiwani hapo,” amesema.

Rais Mwinyi amesema kufikia dira ya maendeleo ya mwaka 2050 ni vyema kuwashirikisha wataalamu hao na ndio maana serikali inajenga mazingira wezeshi ili kutekeleza kazi kwa weledi kufikia malengo hayo.

Amesema tafiti za awali zinaonyesha Zanzibar inarasilimali hizo katika kisiwa hicho kuwa na mafuta na gesi hivyo wizara ya Uchumi wa Buluu ni vyema kuwashirikisha wataalamu hao kusaidia upatikanaji wake.

Rais wa TGS, Dk Elisante Mshiu amesema kuna timu ya wataalamu wa jiolojia kutoka Tanzania Bara watakaokwenda kisiwani hapo kwa ajili ya kuchora ramani upya kubaini maneo yenye rasilimali zinazotokana na utafiti wa jiolojia.

“Zanzibar inaonekana kuwa na maeneo mengi ya rasilimali za gesi asilia na maji, sasa jambo la kubaini yapo maeneo gani kwasasa timu ya wajiolojia hivi karibuni itaanza kutafiti,” alisema Dk Mshiu

Amesema ipo haja katika maeneo mengi yanayohitaji wataalamu wa wajiolojia wapewe nafasi kutoa ushauri wao ili kusaidia kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza na kuvutia wawekezaji wengi nchini.

“Msisitizo wetu kila mmoja akumbuke utaalamu pale yanapotakiwa kufanyika kutoa uwezo wake itasaidia kuepusha hasara na kusaidia kuvutia uwekezaji,” amesema Dk Mshiu

Mwenyekiti wa bodi ya washauri wa TGS, Profesa Abdulkarim Mruma alisema Zanzibar kuna maeneo mengi yenye mwelekeo wa kuwa na rasimali hizo radhini na baharini kwahiyo ni vyema tafiti hizo zikafanyika kubaini kwa kiasi gani rasilimali hiyo inaweza kuwa mkombozi kwa taifa.

Nao baadhi ya washiriki akiwemo mwenyekiti wa chama cha wanafunzi wa wajiolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Janeth Kimario alisema wanawake hawana budi kusoma masomo hayo ili kupata fursa zilizomo.