Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hazina yaagiza mageuzi Tanoil, Gasco

Muktasari:

  • Ofisi ya Msajili wa Hazina, imeagiza wajumbe wa bodi mpya za kampuni mbili tanzu za Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC), kuwa na ubunifu wenye matokeo chanya ya kibiashara pamoja na ufanisi wa huduma kwa umma.

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imeagiza usimamizi wa matokeo chanya kwa wajumbe wa bodi mpya mbili zilizoanza rasmi kusimamia utendaji wa kampuni tanzu za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 31, 2023 jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa bodi hizo zenye wajumbe watano kila kampuni.

Katika tukio hilo, TPDC imetambulisha wajumbe 10, kati yao wajumbe watano ni wa bodi ya kampuni ya mafuta ya TanOil na wengine ni wa kampuni ya gesi ya Gasco.

Akitoa maelekezo mbele ya wajumbe hao, Mkurugenzi wa Huduma za kimenejimenti kutoka ofisi ya hazina, Neema Musomba, ameagiza bodi hizo kuhakikisha zinasimamia maono ya Serikali.

Pia Neema ameagiza bodi hizo kuanzisha mifumo imara ya kufuatilia utendaji kazi, kuwa wabunifu na kutengeneza faida ili ziweze kujitegemea.

“Lakini pia kuhakikisha mnazingatia mahusiano ya kisekta kupitia utekelezaji wa sheria na miongozo, mnaweza kushauri mahali penye vikwazo vya kisheria ili kuboresha,” amesema Neema.

Akizundua bodi hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPDC, Balozi Ombeni Sefue amesema bodi hiyo haitakubali kuona bodi hizo zikikosa ufanisi kutokana na mchujo wa kuwapata.

“Tulipokea jumla ya maombi 248, kati ya hayo, maombi 104 yalikuwa kwaajili ya bodi ya Tanoil, 73 hawakueleza wanataka upande gani, Mei mwaka huu tukawafanyia usaili na kujiridhisha nyie mnaweza kusaidia mageuzi ndani ya kampuni hizo tanzu?” amesema Balozi Sefue, na kuongeza;

“Kwa hiyo hatutawaonea muhali wakati tumeshapewa uhuru wa kujitegemea, naomba muweke mifumo imara, muandae mipango mikakati, muwe wabunifu, wajasiriamali na wathubutu.”

Akitoa mwelekeo mpya katika usimamizi, Mwenyekiti wa bodi hizo mbili, William Chiume ameahidi kujikita kwenye ubunifu wa kibiashara wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Kwa Gasco tutaangalia uwezekano wa kuwa na CNG (pampu ya kujaza gesi kwenye gari), katika vituo vya mafuta. Kwa TanOil, tutashughulikia madeni, mifumo ya kiutendaji na akiba ya mafuta kwa ajili ya kusaidia changamoto zinazojitokeza,” amesema.

Gasco iliyoanzishwa mwaka 1985, ilifufuliwa tena mwaka 2014 kusaidia miradi na miundombinu ya gesi asilia huku TanOil iliyoanzishwa mwaka 2017, ikihusika na biashara ya mafuta.