Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hemed: Mbwembwe zinakitia dosari Kiswahili

Muktasari:

  • Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema wakati Serikali ikiendelea kutafuta fursa mbalimbali kwa wataalamu wa lugha ya Kiswahili, wapo wanaoitia dosari lugha hiyo ama kwa makusudi au kwa kutokujua na hasa pale wanapotia mbwembwe.

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema wakati Serikali ikiendelea kutafuta fursa mbalimbali kwa wataalamu wa lugha ya Kiswahili, wapo wanaoitia dosari lugha hiyo ama kwa makusudi au kwa kutokujua na hasa pale wanapotia mbwembwe.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 4, 2023 wakati akifungua jukwaa la wahariri mjini Zanzibar ambalo linajadili kuhusu nafasi za wahariri wakuu katika kusimamia matumizi ya Kiswahili sanifu katika vyombo vya habari.

Hatua hiyo ni kuelekea siku ya Kiswahili duniani ambayo kilele chake ni Julai 7, 2023.

"Ipo haja kuzingatia matumizi sahihi ya Kiswahili katika kazi zetu kwani ni sehemu ya kukitangaza zaidi duniani, nimefuatilia kwenye vyombo vya habari wengi wenu mnakitumia vizuri lakini hata hivyo wapo wachache wamekuwa wakitia dosari lugha hiyo Kwa kuweka mbwembwe," amesema.

Amewataka kutumia jukwaa hilo kuweka mikakati ambayo itasaidia kuzuia hali hiyo isiendelee kwa lengo la kuitunza lugha hiyo.

Awali Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita amesema wizara zote mbili zina mikakati kuifanya lugha hiyo kuwa bidhaa nje ya nchi na kuwapeleka walimu kufundisha.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema kuna uwezekano wa kukitumia Kiswahili kama bidhaa ya utalii hivyo ipo haja ya kuangalia namna ya kuiendeleza lugha hiyo.

"Wahariri wana nafasi kubwa kusimamia matumizi ya Kiswahili sanifu katika vyombo vya habari," amesema.

Awali akichokoza mada, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Charles Hilary amesema bado wahariri wa vyombo vya habari hususani wa redio na televisheni wanaacha makosa mengi ya kizembe yanapitishwa.

"Wahariri tunaacha mambo yanaenda shaghalabaghala...kule kwenye michezo ndio kubaya zaidi kunachanganywa sana Kiswahili na Kiingereza, bado wahariri hatujafanya kazi yetu," amesema.