HESLB waitwa bungeni kujieleza

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akizungumza wakati wa mkutano wa tisa wa bunge jijini Dodoma, Novemba 1, 2022.

Muktasari:

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameitaka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), kufika katika Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Ijumaa Novemba 4, 2022, ili kujieleza kwanini hawataki kusikiliza maelekezo ya Serikali. 

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameitaka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), kufika katika Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Ijumaa Novemba 4, 2022, ili kujieleza kwanini hawataki kusikiliza maelekezo ya Serikali. 

Agizo hilo limefuatia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda na baadhi ya wabunge kulalamikia kuwa kamati aliyoiunda na (Profesa Mkenda), kuchunguza utoaji wa mikopo ya elimu ya juu imeshindwa kupata ushirikiano.

Dk Tulia ametoa uamuzi huo baada ya Bunge kujadili hoja ya uwepo wa wanafunzi wenye vigezo kukosa mikopo ya elimu ya juu, hoja iliyotolewa na Mbunge wa Biharamulo (CCM), Ezra Chiwelesa

“Naamini kwamba Waziri hawakusikilizi kwenye mambo mengine lakini kwenye hili watakusikiliza wao wataitwa katika Kamati yetu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii…Siku ya Ijumaa saa 7.00 wajikute kwenye hiyo kamati,”amesema.

Tutatoa fursa tujue kama ni kiburi ama kitu kingine tofauti kwa ngazi hii. Kwa maana ya kuichunguza kama inatoa mikopo sawa sawa sio hoja wanazoitiwa ndani ya kamati, sasa hivi tunataka kuelewa kama Bunge kwa nini hiyo bodi haisikilizi hayo maelekezo,”amesema.

Amesema kuhusu hoja kama HESLB inatoa mikopo sawa sawa itajadiliwa Februari mwakani wakati kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii itakapokuwa inatoa taarifa yake bungeni na hivyo kuona kama kuna haja ya Bunge kuunda tume ya kuchunguza bodi hiyo ama la.

Amesema wabunge watapewa taarifa kuhusu kama kinachofanywa na bodi hiyo kama ni kiburi ama la, wiki ijayo baada ya kuwasilikiliza HESLB.