Hisham Hendi aagwa rasmi, mrithi wake afunguka

Hisham Hendi aagwa rasmi, mrithi wake afunguka

Muktasari:

  • Aliyekuwa Ofisa mtendaji mkuu wa Kampuni ya Vodacom, Hisham Hendi ameagwa jana huku akieleza jinsi kampuni hiyo ilivyofanya mageuzi makubwa kwenye teknlojia ya mawasiliano.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Ofisa mtendaji mkuu wa Kampuni ya Vodacom, Hisham Hendi ameagwa jana huku akieleza jinsi kampuni hiyo ilivyofanya mageuzi makubwa kwenye teknlojia ya mawasiliano.

Pia, ameweka wazi kuwa katika hatua za mwisho za uongozi wake kiwango cha ujumuishaji wa kifedha nchini uliathiriwa na tozo mpya za miamala ya simu za mkononi.

Hendi alisema hayo wakati wa hafla ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake aliyohudumu kwa miaka mitatu akiwa mtendaji mkuu. Katika kipindi hicho Hendi aliipandisha kampuni zaidi katika tasnia ya mawasiliano nchini.

“...ninaondoka nikiwa najivunia kwa yote niliyofanya na kufanikiwa. Pia, ninaondoka na imani kwamba Vodacom Tanzania iko katika mikono salama. Ninajua Sitholizwe (mkurugenzi mpya wa Vodacom); Nimefanya kazi naye kwa zaidi ya miaka mitatu nchini Afrika Kusini,” alisema.

Hendi alisema ana matumaini makubwa kuwa Vodacom Tanzania itazingatia ulimwengu wa kidijitali kama fursa za ukuaji inapoendelea kusonga mbele.

“Tumehamia kwenye ulimwengu wa digitali na kupitia hii, tutaendelea na juhudi zetu kukuza ujumuishaji wa kifedha,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Sitholizwe Mdlalose alisema ataendeleza pale Hendi alipoishia kwa kufanya kazi kwa karibu na wadau wote, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na watunga sera (Serikali) ili kuhakikisha uendeshaji mzuri wa kampuni.

Pia, alisema ataendeleza alipoishia mtangulizi wake katika kuhakikisha uwepo wa Vodacom nchini unakuwa na tija kwa maendeleo ya Watanzania.