Bosi Vodacom azungumzia bei ya bando na kodi

Bosi Vodacom azungumzia bei ya bando na kodi

Muktasari:

  • Serikali imeshauriwa kufanya mapitio ya sera na kodi, ili kuhakikisha kunakuwa na ukuaji wa uwekezaji nchini pamoja na kuvutia uwekezaji wa kampuni kubwa kutoka nje ya nchi.

Dar es Salaam. Serikali imeshauriwa kufanya mapitio ya sera na kodi, ili kuhakikisha kunakuwa na ukuaji wa uwekezaji nchini pamoja na kuvutia uwekezaji wa kampuni kubwa kutoka nje ya nchi.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi mkuu wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi na kuongeza kuwa wawekezaji wanazingatia uhakika wa kupata faida, hivyo ni muhimu kuwa na mazingira rafiki yanayokuza uwekezaji.

Alisema Tanzania kuna fursa kubwa kutokana na kuenea kwa matumizi ya intaneti na uwepo wa simu janja, lakini matumizi ya dijitali hapa nchini bado ni madogo, jambo ambalo linaweza kuvutia wawekezaji lakini suala la kupata faida ni jambo muhimu.

“Nikiangalia sekta ya mawasiliano ya simu kwa miaka mitano imekuwa chini ya tarakimu moja tofauti na masoko mengine yanayokua Afrika na Asia ambapo ukuaji ni mpaka tarakimu mbili,” alisema huku akiongeza kuwa Serikali na watunga sera kwa ujumla wanapaswa kuangalia namna ya kukuza teknolojia nchini na sio kuidhoofisha.

Alisema kwa Tanzania tatizo ni kwamba kuna watoa huduma saba ambao kwa kawaida jambo hilo linaleta ushindani katika bei, lakini linaathiri faida na wamiliki wa biashara hawaangalii kukuza biashara pekee bali ni pamoja na faida.

Aliongeza kuwa katika sekta ambayo ina fursa nyingi, lakini hakuna kinachorudi kama faida wawekezaji na wanahisa watakuwa wanafikiri kiasi cha kuwekeza katika eneo hilo, hivyo ni muhimu kuwa na mizania kwa kuwa na mapitio maalumu ya kulinda sekta na kuhakikisha inakuwa na faida.

Kwa mujibu wa ripoti ya fedha ya awali ya kampuni hiyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Machi, 2021 Vodacom ilipata hasara ya Sh30 bilioni tofauti na mwaka uliopita (Machi 2020) ambapo walipata faida ya Sh45.76 bilioni.

Taarifa hiyo ilieleza kampuni hiyo ambayo imekuwa ikidhamini ligi kuu ya soka Tanzania Bara kwa miaka 10 ilipata hasara kutokana na wateja wake zaidi ya milioni 2.9 kufungiwa laini zao kwa kushindwa kukamilisha usajili wa alama za vidole pamoja na sababu nyingine za kikodi.

Hendi alisema mbali na kukosa watu hao, kampuni hiyo ya simu inayoongoza ilitumia fedha nyingi kuhakikisha wateja wake wanatimiza utaratibu huo wa kisheria haraka.

“Mchakato huo mzima uliathiri kukua kwa mapato ya kampuni kwa kuwa uwekezaji ulikuwa unatakiwa mkubwa, kununua vifaa vya kusajili na kuvisambaza, kutoa elimu nakadhalika,” alisema.

Hata hivyo, alisema gharama za huduma zipo chini katika sekta, akitolea mfano gharama ya huduma ya intaneti kwa kusema sekta nzima inauza huduma hiyo kwa hasara.

“Wastani wa bei ya intaneti nchini ni Sh67 kwa MB, lakini inauzwa kwa Sh1.5 hadi 2 kwa MB, jambo ambalo linaashiria kuwa sekta nzima inauza intaneti kwa hasara. Hilo si zuri kwa sekta na wawekezaji wanaliangalia na kujiuliza kwa nini wawekeze katika intaneti wakati inauzwa kwa hasara,” alisema.

Pia alisema katika mwaka huo kodi zilikuwa kubwa na kodi za matangazo ziliongezeka kwa asilimia kubwa, hivyo ongezeko dogo la mapato na ongezeko kubwa la matumizi vilisababisha hasara.

Hata hivyo, katika mahojiano Hendi alisema yajayo huenda yatafurahisha kwa kuwa hivi karibuni wamekuwa na majadiliano mazuri na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Waziri wa Mawasiliano na kamati ya Bunge wakati wa mchakato wa bajeti, hivyo wanatarajia kupata utatuzi wa mambo hayo. “Mwishowe tukifanikiwa kukuza uwekezaji maana yake ni kuwa tutalipa kodi zaidi, wateja watanufaika, lakini kiuchumi tunakuwa mabalozi wa kampuni kubwa Tanzania kwa kuwa tukikua vizuri ni ujumbe mkubwa katika uwanda wa kimataifa na watavutia wawekezaji wengi,” alisema.

Alisema watafanikiwa endapo kutakuwa na mapitio ya gharama za huduma ambayo yatawafanya kuongeza uwekezaji wao nchini na mapitio ya kodi kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye kiwango kikubwa cha kodi katika sekta hiyo kikifikia takribani asilimia 40. Mbali na hilo, Hendi alisema hata kodi ya simu za kisasa nayo ipo juu na endapo ikipunguzwa au kuondolewa kutaongeza idadi ya watu wanaotumia simu hizo na intaneti kwa ujumla, hivyo yajayo yatakuwa chanya.

“Tumekuwa na majadiliano mazuri na Waziri kwa siku zilizopita na tunatumai tutasikia habari njema katika bajeti mpya inayokuja hivi karibuni, ni imani yangu sekta italindwa na kuvutia wawekezaji wengi kutoka nje. Kwa sasa utaona uwekezaji zaidi wa kampuni ya Vodacom huko Kenya na Msumbiji na Congo kwa kuwa ina masoko yanayokua,” alisema.