Hivi hapa vigezo vilivyotumika kupata mabwana harusi 70 wa Shekh Kishk

Mkurugenzi wa taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Nurdin Kishk

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Nurdin Kishki amesema moja ya kigezo walichokizingatia kutoa ufadhili huo ni muoaji kuwa na ajira itakayomuwezesha kuhudumia familia.

Dar es Salaam. Wakati maharusi 70 waliolipiwa mahari kupitia taasisi ya dini ya Kiislamu ya Al- Hikma wakitarajia kufunga ndoa leo Jumapili Agosti 6, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi hiyo Sheikh Nurdin Kishk amesema moja ya kigezo walichokizingatia kutoa ufadhili huo ni muoaji kuwa na ajira itakayomuwezesha kuhudumia familia.

Kishki ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika sherehe ya ndoa hiyo inayofanyika katika ukumbi wa DYCC, Chang'ombe.

Kishki amesema waliweka kigezo hicho ili kuhakikisha kijana anayepata ufadhili huo ana uwezo wa kumuhudumia mkwewe na familia atakayokwenda kuijenga.

"Hatutaki kumuingiza mtu katika ndoa ikiwa yeye mwenyewe hajajipanga, unapooa mke anatakiwa kuhudumia,"amesema

Amesema kingine walichokizingatia ni yule mwenye nia ya dhati ya kuoa lakini amekosa pesa za mkupuo kwa ajili ya kulipa mahari na yule ambaye hana mke.

Kuhusu kuongeza idadi kutoka vijana 50 hadi 70 Kishki amesema walifikia uamuzi huo kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa.

Amesema baada ya taasisi hiyo kutangaza nia ya kutoa ufadhili kwa vijana 50 walipokea maombi ya vijana takribani 1,000 na baada ya kutangazwa utaratibu rasmi vijana zaidi ya 200 walijitokeza kutuma maombi hayo.

"Baada ya usaili tulipata idadi ya vijana tuliokusudia lakini kutokana na uhitaji kuwa mkubwa tukaona ni vyema kuongeza 20 japo tulitamani kufikisha idadi ya vijana 100"amesema.