Hivi ndivyo jinsi ya kusherehekea Valentine yako

Hivi ndivyo jinsi ya kusherehekea Valentine yako

Muktasari:

  • Watu wengi wamekuwa wakisumbuka kupata namna sahihi ya kuwaambia wenzao wao neno nakupenda, kwa wengi linaweza kuwa ni neno la kawaida lakini kwa wanaolitamka wakimaanisha huku wakijua uzito wa neno hilo wamekuwa wakisumbuka kufahamu muda sahihi wa kulitamka.

Watu wengi wamekuwa wakisumbuka kupata namna sahihi ya kuwaambia wenzao wao neno nakupenda, kwa wengi linaweza kuwa ni neno la kawaida lakini kwa wanaolitamka wakimaanisha huku wakijua uzito wa neno hilo wamekuwa wakisumbuka kufahamu muda sahihi wa kulitamka.

Wengi wamesahau kwamba uhusiano si jambo la mazoea bali linahitaji utofauti wa aina yake ili mapenzi yaonekane mapya kila siku na kepusha kuchokana na kumuona mwenza wako ni wa kawaida.


Valentine’S Day ina maana gani?

Siku ya wapendanao (Valentine’ day) si ya kuichukulia poa hata kidogo hasa kwa watu waliopo kwenye mahusiano kwani ina umuhimu wa kipekee na ni maalum kwa ajili ya kuonyesha ni kwa namna gani unampenda na kumthamini mwenza wako.

Kama ilivyo kwa sikukuu nyingine za kidini siku hii ilianzishwa maalumu na Papa Gelasius kama kumbukumbu ya kifo cha mtakatifu Valentine wa Roma ambaye aliuawa Februari 14 baada ya kuhukumiwa kifo kutokana na kuhubiri injili kitendo ambacho hakikuwa kikiruhusiwa kwa wakati huo.

Inasemekana kuwa enzi za uhai wake Valentine alikuwa akifanya matendo mengi ya upendo kwa watu wote ikiwamo kuwafungisha ndoa wanajeshi ambao hawakuwa wakiruhisiwa kufanya hivyo lakini pia alimuombea binti wa mtu aliyemfungwa jela ambaye alikuwa na tatizo la kutokuona lakini baada ya maombezi hayo alifanikiwa kuona.

Kabla ya kuuawa Valentine alimuandikia binti huyo barua ambapo mwishoni aliweka sahihi inayosema “Your Valentine” yaani Valentine wako ili iwe kumbukumbu yake kwake.

Baada ya kifo cha Valentine kwenye karne ya 14 na 15 siku aliyouawa ambayo ni Februari 14 ikaanza kuhusishwa na mapenzi kutokana na matendo yake ya upendo aliyokuwa akiyafanya wakati wa uhai wake.

Kulingana na miaka inavyozidi kwenda siku hii imekuwa ikiendelea kujizolea umaarufu mkubwa kwani wapenzi wamekuwa wakiisheherekea kwa namna tofauti na kuonyeshana ni kwa namna gani wanapendana ikiwamo kupeana zawadi mbalimbali kama ishara ya upendo.


Nini kimebadilika

Hivi sasa dunia nzima ipo katika kipindi kigumu kutokana na janga la virusi vya corona hali iliyosababisha baadhi ya nchi kuweka amri ya karantini kwa raia wake na kufunga baadhi ya maeneo ya starehe ili kuepusha maambukizi ya virusi hivyo.

Hicho ndicho kilichobadilika na hueanda siku ya wapendanao mwaka huu ikasheherekewa tofauti na ilivvyozoeleka kipindi cha nyuma kwani wakati huo watu walikuwa na uhuru wa kufanya chochote katika siku hii muhimu ya ‘ku-show love’.

Hivi sasa wapenzi wanatafuta namna sahihi ya kusheherekea siku hii kwa kubuni mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuifanya iwe nzuri na ya kipekee licha ya changamoto iliyopo, hakuna anayejua itakuaje kilichobaki tusubiri Februari 15 ndiyo tutapata mrejesho kupitia mitandao ya kijamii ambapo tutaona ni kwa namna gani watu wataitumia siku hiyo ‘ku-show love’ kwa wenza wao.


Itasheherekewa ndani au nje ya nyumbani

Chris Mauki, Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye pia ni mwanasaikolojia, mtoa ushauri na mtaalamu wa masuala ya mahusiano amegusia kwa undani kuhusiana na umuhimu wa siku hii na namna sahihi ambavyo inaweza ikasheherekewa katika kipindi hiki cha janga la corona.

Mwanasaikolojia huyu anasema tofauti na watu wengi wanavyopendelea kusheherekea siku hii peke yao yeye na mke wake, Miriam Mauki hufanya tofauti kwani wamejiwekea utaratibu wa kualika watu walioko kwenye mahusiano na kusheherekea nao pamoja.

Aliongeza kuwa yeye na mkewe neno ‘Nakupenda’ kwao ni la kila siku na siyo kwa Valentine peke yake na kwamba wamezoea kufanya kila kitu pamoja hata linapotekea suala la kazi huwa wanasafiri pamoja kila mara na wataeja wake wanalifahamu hilo hivyo wakihitaji huduma yake huwa waamjumuisha na mkewe katika gharama za safari.

Kulingana na hali ilivyo Chris anashauri kufanya baadhi ya mambo ili siku hii iweze kuwa maalumu kwa wapendanao hasa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam ambalo lina maeneo mbalimbali ya kuvutia ambayo watu wanaweza kukaa kwa kupeana nafasi ya kutosha ili kuepusha maambukizi ya corona na siku yao ikawa nzuri.

“Suala la kutoka nje au kusheherekea siku hii ndani ni maamuzi ya mtu binafsi lakini vyovyote vile unaweza ukaifanya kuwa ya kipekee kutokana na namna ulivyodhamiria wewe mwenyewe.

“Hata kama msipoweza kutoka jitahidini mfanye vitu vya kufurahisha kama vile kupika pamoja, kusoma vitabu, kuangalia television na mambo mengine mengi ambayo hayataifanya siku yenu isiwe ya kuboa, jitahidini mfanye mambo ambayo yatawafurahisha wote na kuwafanya muwe mnazungumza lugha moja ya mapenzi,” amesema Chris.

Sote tuliona namna mwaka 2020 ulivyobadilisha baadhi ya mambo hali iliyosababisha watu kusheherekea shughuli mbalimbali nyumbani kwao bila kwenda sehemu yoyote lakini wapo baadhi waliokodisha kumbi za sinema kwa ajili ya kusheherekea sikukuu za kuzaliwa za wapenzi wao ili kuepusha misongamano ya watu, hii inaonyesha kuwa watu wanapaswa kutumia ubunifu katika kufanikisha furaha za wenza wao na familia zao.

Hivi sasa mambo yamebadilika unaweza kuagiza chakula ukaletewa popote pale ulipo lakini iwapo utatenga muda na kumuandalia mpenzi wako chakula kwa kukipika wewe mwenyewe hii huvutia zaidi kwani atajiona kuwa ana umuhimu mkubwa tofauti na ukiagiza chakula hotelini.

Pia, unaweza kutuma zawadi au kubadilisha muonekano wa nyumba yako kuwa wa tofauti utakaoakisi siku hii muhimu kwao wewe na mpenzi wako, unaweza ukaitumia siku hiyo kufanya mambo mengi ukiwa hapohapo nyumbani kwa kufanya mazoezi, massage, kuangalia movie pamoja na kupika, kucheza muziki pia jitahidi uifanye siku hii kuwa ya tofauti zaidi.

Wapo watakaotafuta visingizio kwamba wana majukumu mengi ikiwamo kulea watoto, jitahidi utafute mtu atakayekusaidia kuangalia watoto kwa siku hii moja ili upate muda na mweza wako, katika siku hii mtaweza kujadili mambo mengi na kufaamu ni yapi hayapendi kutoka kwako nawe utamweleza pia na kwa kufanya hivyo mtafanikiwa kujenga ndoa imara na yenye mshikamano.

Hatuwezi kupingana na ukweli kuwa changamoto zitakuwepo katikati ya safari, lakini mwisho wa siku mwenye maamuzi na uwezo wa kuifanya siku hii iwe ya tofauti ni wewe mwenyewe, iwe mtaamua kusheherekea Valentine’s Day nyumbani au mtatoka jitahidini sana muitumie ipasavyo huku mkiwa makini kwa kujali afya zenu hasa mnapokuwa katika mikusanyiko ya watu wengi.

Maandalizi mema ya kuelekea siku ya wapendanao, ifanye iwe ya utofauti, dumisha upendo na amani