Hofu sasa yatanda Ziwa Tanganyika kufungwa

Kigoma. Zikiwa zimebaki siku 11 kabla ya Tanzania kuanza kutekeleza makubaliano ya rasimu ya kusimamisha shughuli za uvuvi wa Ziwa Tanganyika kwa kipindi cha miezi mitatu, wavuvi, wasafirishaji wa mazao hayo na wabunge wamebaki njiapanda wakiomba Serikali itazame upya uamuzi huo.

Makubaliano ya kusimamisha shughuli hizo yalifanyika katika kikao kilichofanyika mwaka jana kikihusisha nchi zinazozunguka ziwa hilo ambazo ni Zambia, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Nchi hizo zilikubaliana kanuni moja ya kutambua zana haramu za uvuvi ili kuruhusu mazalia ya samaki kwa wingi na kudhibiti uvuvi haramu, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Hata hivyo, alipoulizwa jana kwa simu, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema leo atakuwa na mkutano na viongozi wa mikoa na wilaya husika, wakiwamo wabunge kujadili utekelezaji wa suala hilo.

“Tunakwenda kujadiliana namna ya utekelezaji au vinginevyo. Tutapata uelekeo kesho (leo),” alisema Ulega.


Kujengewa uwezo

Awali, katika kikao kingine cha kuwajengea uwezo maofisa wanaoshughulika na usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa nchi zote nne, kilichofanyika mjini Kigoma Februari 12, 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya ziwa Tanganyika, Tusanga Sylvain alisema makubaliano ya kufunga ziwa hilo yalikuja mara baada ya kupokea malalamiko ya wavuvi ya kupungua kwa mazao ya uvuvi kutokana na uvuvi haramu.

Sylvain alisema nchi zote zimesaini makubaliano hayo na kwamba ikifika tarehe husika iliyokuwa imepangwa nchi hizo zitaweza kutekeleza na kuchukua hatua za kusitisha shughuli za uvuvi katika ziwa hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu.


Kilio cha wavuvi

Akizungumzia hatua hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Wavuvi Tanzania, Francis John alisema kabla ya kusitishwa kwa shughuli za uvuvi Serikali ingewapa mikopo na elimu ya ufugaji wa vizimba vya samaki ili wakati wakisitisha shughuli wao wanaendelea na maisha ya uvuvi.

John ambaye pia ni Mwenyekiti wa vyama vya ushirika wa wavuvi Mkoa wa Kigoma, alisema ilipaswa wapate mikopo ya riba nafuu ili wafuge na kuendelea kuvua na kula samaki.

Alisema uvuvi haramu ni hali ya kutumia zana za uvuvi zisizoruhusiwa kisheria kuhatarisha mazalia ya viumbe hai vinavyoishi majini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wavuvi na wadau wa uvuvi mkoani Kigoma, wamesema kufungwa kwa ziwa hilo kutazorotesha hali zao kiuchumi kutokana na asilimia kubwa ya wakazi wa mkoa huo kutegemea ziwa hilo kimapato.

Mchuuzi wa samaki, Beatrice Simon alisema miaka mitano iliyopita alifiwa na mume wake lakini kupitia ziwa hilo amekuwa akipata mahitaji ya familia yake na kwamba endapo wataamua kusitisha shughuli ndani ya ziwa hilo kwa kipindi cha miaka mitatu hali ya maisha itakuwa mbaya kwao.

Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa kampuni ya Mkungu Fish Export, Jamilu Alfan alisema walipopokea taarifa hizo waliambiwa na Serikali kuanzia Januari, 2023 watapewa mafunzo maalumu yatakayowasaidia wakati ziwa hilo litakapositishwa shughuli zake kwa miezi mitatu.

Alfan alisema Mei imeshaanza na kwamba hadi sasa hakuna kilichofanyika na hata wao hawajui hatima yao na kama wangearifiwa mapema wangeweza kuweka hata akiba ya mazao hayo.

Naye Meneja wa kampuni ya Lambati Fish Export, Asha Ibrahim alisema zaidi ya kampuni 20 za usafirishaji zitapoteza nguvu kazi za vijana endapo shughuli za ziwa hilo zitasitishwa na kuna uwezekano mkubwa wa matukio ya kiuhalifu kuongezeka katika mji wao kutokana na vijana wengi kupoteza ajira.

Wafanyabiashara wa samaki katika soko la Kibirizi kwenye Manispaa ya Kigoma Ujiji, Amina Sadiki (kushoto) na Halima Ramadhani (kulia) wakipaa samaki kabla ya kwenda kuwauza sokoni hapo, Februari 15, 2019. Picha na Maktaba

Wabunge wang’aka

Suala hilo liliibuka bungeni jijini Dodoma jana, wakati wabunge wanaotoka mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2023/24, wakiitaka Serikali kuwa makini na jambo hilo.

"Mkoani Kigoma kuna taharuki sana kuhusu kufungwa kwa ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu kuanzi Mei 15. Ni jambo jema nikiwa kama mwakilishi wa wananchi sikusudii kupinga nalo isipokuwa ushirikishwaji wa wananchi unahitajika,” alisema Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda.

Aliendelea, “kama hakuna ushirikishaji wa wananchi kunakuwa na ubatili, turudi kushirikisha wananchi."

Kwa upande wake, Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenan aliunga mkono hoja ya Kilumbe Ng’enda akisema mikoa hiyo inasubiri tamko la Serikali.

“Ziwa Tanganyika tuna share nchi nne, DRC inatumia 45, Tanzania asilimia 41, hizo nchi mbili asilimia inayobaki ndiyo wanatumia.

“Unapoingia makubaliano ya kufunga na nchi zenye asilimia ndogo, lengo ni nini? Unakwenda kumnufaisha nani? Kama wengine wanaweza kuzungumzia korosho ndio uchumi wao, madini ndio uchumi wao, uchumi wetu ni Ziwa Tanganyika, ndio duka letu,” alisema.

Alishauri Serikali kupambana na uvuvi haramu badala ya kukimbilia kusema kufunga ziwa.

Naye Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM), Nashon Bijanguze, mbali na kulalamikia kutoshirikishwa, alisema hadi sasa Serikali haijatoa ajira mbadala kwa wavuvi.

“Nimekwenda kufanya ziara kwenye kata mbili, Sigunga na Mgambo, Sigunga wameniambia, mbunge tunaomba kama ziwa linakwenda kufungwa tuandalie makaburi, hatuna kazi nyingine ya kufanya kazi yetu ni hapo ziwani. Hiyo kauli ni nzuri kwa wananchi ambao ni wapiga kura?

Suala la kutoshirikishwa pia limelalamikiwa na Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Kigoma (CCM), Sylvia Sigula akisema,“haiwezekani leo bado siku nane, sisi wawakilishi hatuna taarifa rasmi kuhusu kufungwa kwa ziwa.”

Wakati mbunge huyo akiendelea kuzungumza, Mbunge Ng’enda alitoa taarifa akisema Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekataa hoja ya kufunga ziwa Tanganyika, “kwa maana hiyo, leo (jana) tuko kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano na sisi tunakataa.”


Majibu ya Waziri Ulega

Kuhusu ziwa Tanganyika Ulega alisema “limesemwa kwa kirefu sana kuhusu Ziwa Tanganyika kufungwa na wabunge wa Kigoma, Rukwa, Katavi, wamesema kwa mapana na wananchi wamewasikia na sisi tumewasikia,” alisema Ulega.

Alisema wa suala hilo ulikuwa na lengo jema lakini haikulazimisha nchi wanachama namna ya kutekeleza itifaki kwa kufanana.