Hoja kukosekana mkalimani wa Kisukuma yashindwa kumnusuru kifungo cha miaka 30
Muktasari:
- Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Musoma, imetupilia mbali rufaa ya Komanya Makoye, ikiwemo hoja yake kuwa hakuelewa lugha ya Kiswahili wakati wa kesi yake na hivyo alipaswa kupewa mkalimani wa Kisukuma, huku ikibainisha kuwa alijibu mashtaka, aliwahoji mashahidi na kujitetea kwa Kiswahili.
Arusha. Komanya Makoye, aliyekuwa akipinga kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji akidai Mahakama ya Wilaya ya Musoma ilimnyima mkalimani wa lugha ya Kisukuma kwa kuwa hakuelewa Kiswahili, ameshindwa katika hoja hiyo baada ya Mahakama Kuu kubaini kumbukumbu za kesi zinaonyesha alijibu mashtaka yote kwa Kiswahili bila kuonyesha kuwa alikuwa na tatizo la kuelewa mwenendo wa kesi.
Mahakama ilibaini kuwa Makoye aliwauliza mashahidi maswali kwa Kiswahili na alijitetea na kujibu maswali yote bila kuonyesha kuwa hakuelewa kilichokuwa kinaendelea mahakamani.
Aidha, Mahakama ilitupilia mbali madai ya Makoye kuwa kesi hiyo ilitokana na mgogoro wa deni la Sh milioni mbili kati yake na baba wa mwathiriwa, ikieleza kuwa utetezi huo ulizingatiwa na Mahakama ya Wilaya, lakini haukuibua shaka yoyote dhidi ya ushahidi wa upande wa mashtaka uliomhusisha na kosa la ubakaji.
Uamuzi huo ulitolewa Julai 13, 2026 na Jaji Kamazima Kafanabo wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Musoma, wakati akiamua rufaa ya Makoye, akipinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Musoma.
Katika uamuzi huo, Jaji alithibitisha hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji, lakini akafuta hatia na adhabu ya miaka mitano kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi baada ya kubaini shtaka hilo halikuthibitishwa bila kuacha shaka.
Kesi ya msingi
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani katika Mahakama ya Wilaya, ilidaiwa kuwa kati ya Januari na Septemba 2025 katika Kijiji cha Kwibara, Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Makoye alifanya ngono mara kadhaa na mwanafunzi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 16, ambaye baadaye aligundulika kuwa na ujauzito.
Baada ya kutiwa hatiani, Mahakama ya Wilaya ilimhukumu kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji na miaka mitano jela kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi, huku adhabu hizo zikienda kwa pamoja.
Rufaa
Makoye hakuridhika na hukumu hiyo na kukata rufaa akitoa sababu saba, zikiwemo madai kuwa alihukumiwa kwa kutegemea ushahidi usiothibitishwa wa mwathiriwa, kulikuwa na utata katika ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, kesi ilitokana na mgogoro wa deni la Sh milioni mbili, hakukuwa na ushahidi wa DNA unaomhusisha na ujauzito, na kwamba alinyimwa mkalimani wa Kisukuma.
Uamuzi wa Mahakama
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, kupitia mwenendo wa kesi, Jaji Kafanabo amesema Mahakama ya kwanza ya rufaa ina wajibu wa kupitia upya ushahidi wote na kufikia hitimisho lake, huku akisisitiza kuwa katika kesi za jinai upande wa mashtaka unatakiwa kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka yoyote.
Mahakama imesema ushahidi wa mwathiriwa ulikuwa wa kuaminika na uliungwa mkono na ushahidi wa daktari aliyemfanyia uchunguzi na kuwasilisha Fomu ya Polisi Namba Tatu (PF3).
Jaji amesema ushahidi wa baba wa mwathiriwa pamoja na maelezo ya mwathiriwa mwenyewe ulithibitisha kuwa alikuwa na umri wa miaka 16 wakati matukio hayo yalipotokea, hivyo kukidhi moja ya vipengele muhimu vya kosa la ubakaji wa mtoto chini ya miaka 18.
Mahakama imesema sheria inaruhusu ushahidi wa mwathiriwa wa kosa la kingono kutegemewa hata bila uthibitisho mwingine endapo mahakama itajiridhisha kuwa ushahidi huo ni wa kweli na unaaminika.
Jaji Kafanabo ameeleza kuwa mwathiriwa alitoa maelezo ya kina kuhusu namna alivyoshawishiwa kuingia katika uhusiano huo, maeneo walikokuwa wakikutana na nyakati walizokuwa wakifanya ngono, huku Makoye akishindwa kupinga ushahidi huo kwa kumuhoji wakati wa usikilizwaji wa kesi.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama iliridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kosa la ubakaji bila kuacha shaka yoyote na hivyo hukumu ya miaka 30 jela ikaachwa kama ilivyotolewa na Mahakama ya Wilaya.
Hata hivyo, kuhusu shtaka la kumpa mimba mwanafunzi, Mahakama ilisema pamoja na kuthibitika kuwa mwathiriwa alikuwa mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Mugango na kwamba alikuwa na ujauzito wa mwezi mmoja, ushahidi huo haukutosha kuthibitisha kuwa Makoye ndiye aliyesababisha ujauzito huo.
Jaji amesema kwa kuwa Makoye alipinga kuhusika na ujauzito huo, upande wa mashtaka ulipaswa kuwasilisha ushahidi wa kisayansi wa DNA au ushahidi mwingine madhubuti unaounganisha mtuhumiwa na ujauzito huo, jambo ambalo halikufanyika.
"Kwa mazingira ya kesi hii, shtaka la kumpa mimba mwanafunzi halikuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote," imesema sehemu ya hukumu.
Kutokana na hitimisho hilo, Mahakama ilifuta hatia na adhabu ya kosa la kumpa mimba mwanafunzi, lakini ikaamuru Makoye aendelee kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji.