Prime
Madai ya maombi kanisani yashindwa kumuokoa, ahukumiwa kunyongwa
Muktasari:
- Mbali na kudai alikuwa kanisani kwa siku tano mfululizo akiomba pamoja na mkewe aliyekuwa mgonjwa, Jastine Overdeus ameshindwa kujinasua na shtaka la mauaji baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Bukoba kumtia hatiani kwa kosa la kumuua bibi yake Hamadera Vedasto na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Arusha. Madai ya Jastine Overdeus kwamba alikuwa kanisani kwa siku tano mfululizo akiomba pamoja na mkewe aliyekuwa mgonjwa, yameshindwa kumsaidia kujinasua na hukumu ya kunyongwa hadi kufa baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Bukoba kumtia hatiani kwa kumuua bibi yake, Hamadera Vedasto.
Jastine aliiambia Mahakama kuwa kuanzia Julai 5 hadi Julai 10, 2024 alikuwa katika Kanisa la Kaanani, Omurusha-Nyakahanga, ambako alikuwa amempeleka mkewe kwa ajili ya maombi kutokana na ugonjwa wake. Alidai kuwa hakuwapo eneo la tukio wakati Hamadera aliposhambuliwa.
Hata hivyo, Mahakama ilikataa utetezi huo, ikisema haukuweza kuondoa uzito wa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, hususan ushahidi wa shahidi aliyedai kumuona Jastine akimshambulia marehemu kwa panga usiku wa tukio.
Hukumu hiyo ilitolewa Julai 10, 2026 na Jaji Ferdinand Kiwonde na nakala yake ikawekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, Hamadera alishambuliwa kwa panga usiku wa Julai 7, 2024 akiwa nyumbani kwake katika Kijiji cha Kafunjo, Wilaya ya Karagwe, Mkoa wa Kagera.
Alipata majeraha makubwa kichwani, kisogoni na magotini na baada ya kupelekwa hospitalini kwa matibabu, alifariki dunia Julai 11, 2024.
Ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu iliyowasilishwa mahakamani ilieleza kuwa chanzo cha kifo kilikuwa jeraha kubwa la ubongo lililosababishwa na kupigwa na kitu chenye ncha kali kilichopenya kwenye fuvu la kichwa.
Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita pamoja na kielelezo kimoja cha ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu.
Shahidi muhimu katika kesi hiyo alikuwa Irene Overdeus, ambaye ni dada wa mshtakiwa na shahidi pekee aliyedai kushuhudia tukio hilo. Irene alieleza kuwa alimwona Jastine akimshambulia Hamadera kwa panga ndani ya nyumba usiku wa tukio.
Alisema alimtambua mshtakiwa kwa msaada wa mwanga wa taa ya sola iliyokuwa ikiwaka ndani ya nyumba hiyo, akiwa umbali wa takribani mita moja kutoka alipokuwa amelala.
Kwa mujibu wa Irene, baada ya kupiga kelele, Jastine alimtishia na baadaye alimjeruhi pia kabla ya kutoroka.
Mahakama ilisema ushahidi wa Irene uliungwa mkono na ushahidi wa kitabibu pamoja na maelezo ya mashahidi wengine waliothibitisha mazingira ya tukio na kifo cha marehemu.
Utetezi wa mshtakiwa
Katika utetezi wake, Jastine alikana kuhusika na mauaji hayo na kusisitiza kuwa alikuwa katika Kanisa la Kaanani akimpeleka mkewe kwa maombi kuanzia Julai 5 hadi Julai 10, 2024.
Alidai kuwa kutokana na kuwepo kanisani katika kipindi hicho, hangeweza kuwa nyumbani kwa marehemu wakati wa tukio lililotokea Julai 7, 2024.
Mbali na ushahidi wake mwenyewe, Jastine aliwasilisha shahidi mmoja wa utetezi ambaye alieleza kuwa alikuwa pamoja naye katika mazingira ya kanisani.
Hata hivyo, Mahakama ilisema shahidi huyo alitoa ushahidi wenye mapungufu baada ya kukiri kuwa hakujua kwa usahihi siku ambayo Hamadera alishambuliwa au kuuawa, na pia hakuwa pamoja na mshtakiwa muda wote ambao alidai alikuwa kanisani.
Sababu za uamuzi wa Mahakama
Katika uamuzi wake, Jaji Kiwonde alisema utetezi wa kutokuwepo eneo la tukio haukuweza kuibua shaka katika ushahidi wa upande wa mashtaka.
Alisema ingawa Jastine alidai alikuwa kanisani kwa siku tano, ushahidi wa shahidi wake wa utetezi haukuweza kuthibitisha madai hayo kwa kiwango kinachoweza kuondoa ushahidi uliowasilishwa dhidi yake.
Mahakama ilisema ushahidi wa Irene ulikuwa wa kuaminika kwa sababu alimfahamu mshtakiwa kabla ya tukio, alimtambua wakati wa shambulio na alieleza mazingira yaliyomwezesha kumuona.
Kwa mujibu wa Mahakama, ushahidi huo ulimweka Jastine moja kwa moja katika eneo la tukio, hivyo madai yake ya kutokuwepo hayakuweza kusimama mbele ya ushahidi huo.
Katika kuchambua suala la nia ya kuua, Jaji Kiwonde alisema matumizi ya panga na kulenga maeneo nyeti ya mwili, hususan kichwa, yalionyesha kuwa mshtakiwa alikuwa na nia ya kusababisha kifo.
Mahakama pia ilisema ushahidi ulionyesha mshtakiwa alionekana karibu na nyumba ya marehemu siku moja kabla ya tukio, jambo lililoongeza uzito wa mazingira yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka.
Baada ya kupitia ushahidi wote wa mashahidi na vielelezo vilivyowasilishwa, Mahakama Kuu ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kosa la mauaji bila kuacha shaka yoyote.
Kutokana na uamuzi huo, Jastine Overdeus alikutwa na hatia ya mauaji chini ya Kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.