Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hoja ya faragha ya mawakili, mahabusu yaibuka mahakamani

Muktasari:

  • Hoja ya mazingira yanayowezesha faragha ya mazungumzo kati ya mawakili na mahabusu imeibuka leo Alhamisi, Julai 23, 2026, wakati wa mahojiano baina ya wakili wa walalamikaji katika kesi ya Kikatiba, John Seka na Mkuu wa Gereza la Ukonga.




Dar es Salaam. Mawakili wameieleza Mahakama Kuu kuwa, vikwazo wanavyowekewa wanapokwenda Gereza la Ukonga kufanya mashauriano ya kisheria, vinakiuka haki ya mawasiliano ya faragha kati ya wakili na mteja inayotambuliwa na Katiba na kanuni za Magereza.

Hoja hiyo ya mazingira yanayowezesha faragha ya mazungumzo kati ya mawakili na mahabusu imeibuka leo Alhamisi, Julai 23, 2026, wakati wa mahojiano baina ya wakili wa walalamikaji katika kesi hiyo, John Seka na Mkuu wa Gereza la Ukonga.

Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna Mkuu wa Magereza, Mkuu wa Gereza la Ukonga, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu  na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kilichounganishwa kama mdau mwenye masilahi.

Mawakili waliofungua kesi hiyo ya Kikatiba ambao wanajitambulisha kuwa washauri wa kisheria wa Lissu ni Kulwa Maduhu, Nashon Nkungu na Paul Kisabo.

Katika kesi hiyo ya Kikatiba namba 7300/2026, mawakili hao wanapinga vikwazo wanavyodai kuwekewa wanapokwenda Gereza la Ukonga kufanya mashauriano ya kisheria na Lissu, wakieleza kuwa vinakiuka haki ya mawasiliano ya faragha kati ya wakili na mteja inayotambuliwa na Katiba na Kanuni za Magereza.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiondoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akiwa chini ya ulinzi wa Askari wa Jeshi la Magereza mara baada  kusikiliza kesi ya mawakili. Picha na Said Powa

Kesi hiyo iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Amir Mruma ( kiongozi), Dk Angelo Rumisha na Dk Everisto Longopa, linaloketi Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa kwa njia ya maandishi sambamba na pingamizi lililowekwa na Serikali.

Hata hivyo, Lissu aliomba na akaruhusiwa walalamikaji wafike mahakamani ili awaulize maswali ya dodoso dhidi ya madai yao.

Lissu alianza kuwahoji walalamikaji na akahitimisha na Mkuu wa Gereza la Ukonga jana Jumatano, Julai 22, 2026 ambaye leo mkuu huyo ameendelea kuhojiwa maswali ya dodoso na wakili wa walalamikaji, Seka.

Katika mahojiano, mkuu huyo wa gereza amekiri kuwa kanuni za uendeshaji wa magereza zinatambua haki ya mahabusu kuwasiliana na washauri wao wa kisheria na katika utekelezaji wa utaratibu huo, askari anatakiwa kuona kinachoendelea bila kusikia mazungumzo.

Sehemu ya mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo.

Seka: Unakubaliana na mimi taasisi ya magereza ni chombo kilichoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Magereza kifungu cha 13 kifungu kidogo cha (3)?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Wewe kama msimamizi wa Gereza la Ukonga, unakubaliana na mimi kwamba, wewe ndiye msimamizi wa haki na wajibu ndani ya Gereza la Ukonga?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Shahidi, nitakupeleka kwenye Ibara ya 16(1) na Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Nchi. Isome.

Mkuu wa Gereza: (Anasoma.)

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu (kulia) akijadiliana jambo na Mwanasheria wake, John Seka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Picha na Said Powa

Seka: Tunaongelea faragha, unakubaliana na mimi kwamba, kwa mujibu wa ibara hii, mamlaka zinaweza kuingilia faragha na mawasiliano binafsi?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Ili uweze kufanya hivyo, utafanya ukiwa unazingatia masharti na matakwa ya ibara hii?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Nataka nikupeleke kwenye Ibara ya 22(1). Shahidi, soma.

Mkuu wa Gereza: (Anasoma.)

Seka: Unafahamu kwamba mawakili wana haki ya kufanya kazi ya uwakili mahali popote na wewe, kama mzoefu wa magereza, unafahamu wanaweza kufanya uwakili ndani ya magereza kwa kufuata taratibu?

Mkuu wa Gereza: Nafahamu.

Seka: Nataka nikupeleke kwenye Ibara ya 26(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, soma.

Mkuu wa Gereza: (Anasoma.)

Seka: Na wewe una wajibu wa kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Pia una wajibu wa kuheshimu sheria za nchi?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Bila shaka moja ya sheria unazopaswa kuziheshimu ni Sheria ya Magereza ambayo umeisomea na umeibobea?

Wafuasi wa Chadema wakivutana kwa maneno na Askari wa Jeshi la Polisi nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo, July 23, 2026. Chadema wakitaka kuzungumza na vyombo vya habari huku Jeshi hilo likisema hawana kibali cha kufanya hivo. Hata hivyo wafuasi hao waliamua kuondoka. Picha na Said Powa

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Bila shaka una wajibu pia wa kutii, kuzingatia na kuheshimu kanuni za uendeshaji wa Magereza za mwaka 1968?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Bila shaka kanuni hizo unazo?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Bila shaka unapaswa kuheshimu Kanuni ya 13 ya Kanuni za Uendeshaji wa Magereza?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Nitakupeleka kwenye Ibara ya 29(1) ya Katiba.

(Shahidi anasoma.)

Seka: Kwa mujibu wa Katiba hii, nani ana haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu?

Mkuu wa Gereza: Watu wote.

Seka: Ili watu hao wafaidi haki hizo, wewe pia una wajibu wa Kikatiba kutekeleza wajibu wako?

Mkuu wa Gereza: Ni kweli.

Seka: Nakupeleka kwenye Ibara ya 29(2).

(Shahidi anasoma). Unakubaliana na mimi kuwa Lissu anastahili kupata hifadhi sawa chini ya sheria?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Sasa shahidi, twende kwenye Kanuni ya 13 ya Kanuni za Uendeshaji wa Magereza, kwa uzoefu wako wa miaka 31, mara yako ya kwanza kukutana na kanuni hii ilikuwa lini?

Mkuu wa Gereza: Tangu nilipoanza kazi.

Seka: Kwa miaka hiyo 31 unajua ofisa wa magereza anapofanya kazi lazima aheshimu kanuni ya 13?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Isomee Mahakama Kanuni ya 13 inasemaje.

Mkuu wa Gereza: (Anasoma.)

Seka: Kwa uzoefu wako, tufafanulie kanuni hii inamaanisha nini.

Mkuu wa Gereza: Mfungwa au mahabusu atapewa nafasi ya kuwasiliana na mshauri wa kisheria, mwanasheria au mtu yeyote baada ya Officer in Charge kuhakikisha anawakilisha masilahi ya mfungwa huyo, mazungumzo ya kisheria yatafanyika kwa kuona bila kusikia.

Seka: Nitakuwa sahihi nikisema kwenye kanuni hii kuna haki ya mfungwa na mshauri wa kisheria?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Na haki ya kwanza iliyopo kwenye kanuni hii ni haki ya mfungwa au mahabusu kupewa mazingira ya kuwasiliana na mawakili wake?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Haki ya pili ni ya mawakili kupata fursa ya kuzungumza na mfungwa kwa faragha bila kusikilizwa, bali kutazamwa tu?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Kwa miaka yako 31, jukumu la kuona bila kusikiliza ni la kujifunza au uzoefu?

Mkuu wa Gereza: Ni katika utekelezaji, naona hapa natakiwa nione, nisikie.

Seka: Sasa kwenye utekelezaji huo mlifundishwa kuwa kuna umbali maalumu ili uweze kuona bila kusikia?

Mkuu wa Gereza: Hakuna umbali maalumu.

Seka: Kwa hiyo utekelezaji wake unategemea mtu na mtu?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Shahidi, nitahama kidogo utanisaidia kwenye uzoefu, nikumbushe, najua ofisi ya mkuu wa gereza pale Ukonga kwa miaka mitano au sita haijabadilika.

Mkuu wa Gereza: Na mimi siwezi kujua kama imebadilika.

Seka: Ina ukubwa kiasi gani?

Mkuu wa Gereza: Ni kubwa ya kutosha.

Katika hilo, mmoja wa majaji alitaka afafanue ni ya kutosha kiasi gani?  akiuliza kama ni ya kutosha watu wote waliokuwa  kwenye ukumbi huo wa Mahakama wakifuatilia kesi hiyo au ukubwa wa kiasi gani.

Mkuu wa Gereza: Hapana.

Seka: Anaanza kuonesha ukubwa kwa vitendo.

Mkuu wa Gereza: Naye anaonesha urefu kwa makadirio.

Seka: Na mapana?

Mkuu wa Gereza: Siwezi kukadiria.

Seka: Upo chini ya kiapo.

Mkuu wa Gereza: Anaonesha upana kwa ishara.

Hata hivyo, mmoja wa mawakili wa Serikali ameiomba Mahakama, shahidi asizungumzie ukubwa wa ofisi yake kwa kuwa ni suala la kiusalama.

Mahakama imeikataa hoja hiyo ya wakili wa Serikali ikieleza kuwa, "hatuoni kama ni jambo lolote la kiusalama kuzungumzia ukubwa wa ofisi yake, aseme kama ni kubwa zaidi au ndogo zaidi."

Seka:  Ofisi ya Bwana Rachel, ambaye ni msaidizi wako, ni kubwa kuliko yako?

Mkuu wa Gereza: Ni kubwa kidogo.

Seka: Nikikaa hapa nikiongea, unanisikia?

Mkuu wa Gereza: Inategemea sauti gani.

Seka: Hii ninayoongea.

Mkuu wa Gereza: Ndiyo, nasikia.

Seka: Shahidi, wewe na walalamikaji kwenye mahojiano mmekuwa mkiongelea sana ofisi ya admission.

Mkuu wa Gereza: Mimi na mashahidi?

Seka: Ndiyo, mmekuwa mkiongelea kufanyia mikutano ofisi ya admission.

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Ni kubwa kiasi gani?

Wakili akaonesha ukubwa kwa vitendo na akauliza akiwa mbali kama anasikika, kisha akaongea kwa sauti ndogo na kumuuliza mkuu wa gereza kama anasikia.

Mkuu wa Gereza: Siwezi kusikia.

Seka: Huwezi, halafu unajibu?

Seka: Umewahi kufika ofisi ya admission karibuni?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Kuna meza ambayo mawakili wanakaa?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Ukubwa wake ni kama huu? (Akaonesha kwa ishara.)

Mkuu wa Gereza: Sijui.

Seka: Nisaidie ufahamu tu, umewahi kuhudhuria mahojiano kati ya wakili yeyote na mfungwa ndani ya ofisi ya admission tangu umefika Ukonga au hata kupita?

Mkuu wa Gereza: Kupita, siyo kuudhuria.

Seka: Sawa. Umewahi kupita ofisi ya admission ukakuta kuna mahojiano kati ya wakili na mteja wake?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Seka: Tumia meza hii kama mfano (akionesha meza ndani ya chumba cha Mahakama) na kuuliza, huwa wanakaaje?

Mkuu wa Gereza: Wanakaa wakitazamana.

Seka: Uliona na kushuhudia?

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Hata hivyo, uamuzi wa shauri hilo utatolewa Septemba 16, 2026.