Hosteli ya kisasa ya wanafunzi yazinduliwa Moshi
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai akizindua hosteli ya kisasa ya wanafunzi katika chuo cha usimamizi wa wanyamapori, Mweka ambayo itaweza kubeba wanafunzi 295. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Profesa Jafary Kideghesho amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa hosteli ya kisasa itasaidia kuondoa changamoto ya malazi pamoja na kuongeza usalama na udhibiti wa nidhamu kwa wanafunzi.
Moshi. Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Profesa Jafary Kideghesho amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa hosteli ya kisasa itasaidia kuondoa changamoto ya malazi pamoja na kuongeza usalama na udhibiti wa nidhamu kwa wanafunzi.
Profesa Kideghesho ameyasema hayo wilayani Moshi wakati wa ufunguzi wa hosteli hiyo yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 295 ujenzi wake umegharimu Sh2.46 bilioni.
Amesema hosteli hiyo ina vyumba 85 ambapo kati ya hivyo15 ni vyumba maalumu (VIP) na 70 ni vyumba vya kawaida.
"Kukamilika kwa mradi huu wa hosteli hii itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa malazi kwa wanafunzi na kuongeza usalama na udhibiti wa nidhamu kwa wanafunzi wetu,"amesema Profesa Kideghesho
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RC), Stephen Kagaigai amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hosteli hiyo pamoja na kukipongeza chuo hicho kwa usimamizi mzuri.
"Chuo mmefanya kazi nzuri ya usimamizi wa jengo hili na niwapongeze Suma JKT kwa kazi hii kubwa ambayo mmeisimamia, mko makini sana nishauri baadhi ya taasisi zote za umma pale inapoonekana kuna miradi tumieni Suma JKT kwasababu wako makini kwenye kazi zao,"amesema RC Kagaigai
Mwenyekiti wa bodi ya magavana wa chuo hicho, Profesa Faustine Bee ameishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya ujenzi huo.
"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutupatia fedha hizi kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu, fedha hizi zimetumika vizuri na sisi bodi tulijiridhisha kwa kutembelea mradi huu mara kwa mara kuona shughuli zinazoendelea,"
Mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho, Rosemary Nkya amesema uwepo wa hoteli hizo itawapunguzia adha mbalimbali ikiwemo kuvamiwa na vibaka jioni.