Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huduma za usafirishaji Bandari ya Musoma kurejea mwakani

Nahodha msaidizi wa Kampuni ya huduma za meli nchini(MSCL) , Prisca Mniko akizungumza mjini Musoma juu ya mpango wa kampuni hiyo kurejesha usafiri wa meli katika bandari ya Musoma. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL) inatarajia kurejesha huduma za usafiri wa meli kwa Mkoa wa Mara baada ya huduma hiyo kusitishwa kwa miongo kadhaa kufuatia meli za kampuni hiyo kupata hitilafu na kuharibika kwa nyakati tofauti.




Musoma. Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL) inatarajia kurejesha huduma za usafiri wa meli kwa Mkoa wa Mara baada ya huduma hiyo kusitishwa kwa miongo kadhaa kufuatia meli za kampuni hiyo kupata hitilafu na kuharibika kwa nyakati tofauti.

Huduma hizo zinatarajiwa kurejea katika Bandari ya Musoma mwakani ambapo miongoni mwa safari zinazotarajiwa kuwepo ni pamoja na ile ya Musoma- Kisumu nchini Kenya hadi nchini Uganda.

Ofisa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Anthony Nyamhanga amesema mjini Musoma leo Alhamisi 8, 2022  kwenye maonesho ya biashara ya Mkoa wa Mara yanayoendelea kuwa safari hizo zinatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa meli zinazojengwa na kampuni hiyo.

Meli hizo ni Mv Mwanza na Mv Butiama na kwamba safari hiyo itahusisha huduma ya usafirishaji wa mizigo pamoja na abiria.

"Mv Butiama na Mv Mwanza ziko katika hatua kubwa tu ya ukamilishaji kwa hiyo zitakapokamilika lazima tutarejesha usafiri wa meli katika Bandari yetu ya Musoma ambayo kwa muda mrefu haifanyi kazi kutokana na kutokuwepo kwa meli," amesema.

Amesema kuwa baada ya vyombo vingi vya usafiri wa majini vinavyomilikiwa na kampuni hiyo kupata hitilafu Serikali iliamua kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutengeneza na kujenga meli mpya ili kuwezesha kampuni hiyo kutoa huduma zake bila kikwazo kutokana na umuhimu wa usafiri wa majini katika kukuza uchumi wa nchi.

Naye nahodha msaidizi kutoka kampuni hiyo, Prisca Mniko amesema kuwa kwa mara ya mwisho meli ya kampuni hiyo ilitia nanga katika Bandari ya Musoma mwaka 2017 wakati ilipokiwa imeleta nguzo za umeme wa REA kutoka nchini Uganda.

" Zamani tulikuwa na safari za huku ila kwa mara ya mwisho meli yetu ilitia nanga  mwaka 2017, niwaondoe wasiwasi  wakazi wa Musoma na Mara kuwa huduma zitarejea kama kawaida na pia wajue kuwa huduma zetu ni nafuu na salama kwani Serikali imewekeza pesa nyingi sana kuboresha usafiri wa majini," amesema Prisca.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo Nchini (TCCIA) Mkoa wa Mara, Boniface Ndengo amesema kuwa uamuzi wa kampuni ya huduma za meli kurejesha usafiri wa majini mkoani Mara ni wa kupongezwa kwani utasaidia  kuboresha uchumi wa mkoa huo na watu wake.

" Mbali na kwamba tunahitaji usafiri wa meli kutoka Musoma kwenda wilaya kama  Bunda na Rorya lakini usafiri huu ni kiungo kati ya Mara na nchi za Kenya na Uganda hivyo itakuwa ni rahisi kwa wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao kutoka ama kwenda katika nchi hizo," amesema Ndengo.

Amesema kuwa kutokana na fursa nyingi za kiuchumi zilizopo mkoani Mara mkoa huo unaweza kuwa wa kwanza kwa kuchangia pato la taifa kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa endapo kutakuwepo na miundombinu rafiki kwa ajili ya uwekezaji likiwepo suala la usafiri majini.

Meneja wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) Kanda ya Ziwa, Girson Ntimba amesema kuwa kurejeshwa kwa usafiri wa meli mkoani Mara ni moja ya  kichocheo kikuu cha uwekezaji katika mkoa huo.

" Uwekezaji  ni pamoja na kuwa na viwanda, sasa ili uweze kusafirisha bidhaa zako kwenda maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na nje ya nchi ni lazima uwe na usafiri wa uhakika na salama na usafiri wenyewe ni wa majini, meli zikianza kutoa huduma hapa moja kwa moja wawezekaji watakuja kwasababu fursa zipo," amesema.