Hukumu kigogo Vodacom, wenzake hii hapa

Thursday April 11 2019
VODACOM PIC

Mkurugenzi Mtendaji wa kamapuni ya Mawasiliano ya Vodacom ,Hisham Hendi Kizimbani katika mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaaam jana. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu, Mkurungenzi Mtendaji wa Kampuni ya  Mawasiliano ya simu ya mkononi  nchini Vodacom, Hisham Hendi na wenzake nane, kulipa faini na fidia ya zaidi ya Sh6 bilioni baada ya kukiri mashtaka yao.

Pia, mahakama hiyo imetaifisha mitambo na vifaa vyote vya  mawasiliano vilivyotumika katika uhalifu huo.

Mashtaka yaliyowatia hatiani washtakiwa hao ni kuingiza, kutumia na kusimika vifaa vya mawasiliano, kugawa namba za simu, kupiga simu za kimataifa nje ya nchini bila leseni kutoka TCRA.

Mengine ni kumiliki vifaa kilaghai pamoja na mashtaka mawili ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh5.8 bilioni.

Mbali na Hendi, washtakiwa wengine ni Ahmed Ngassa, ambaye ni meneja uendeshaji wa biashara kutoka kampuni ya Inventure Mobile Tanzania Ltd/ A Tala Tanzania; mtalaamu wa IT ambaye ni raia wa Kenya, Brian Lusiliola  na kampuni ya Inventure Mobile Tanzania Ltd, iliyopo katika jengo la Tanzanite Park, eneo la Victoria.

Washtakiwa wengine ni Mkuu wa Idara ya Mapato wa Kampuni ya Vodacom, Joseph Nderitu; Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Vodacom, Olaf Mumburi;  na Mkuu wa Idara ya Mauzo wa Vodacom, Joseph Muhere.

Advertisement

Wengine ni Meneja wa Fedha wa Vodacom, Ibrahim Bonzo na Kampuni ya Mawasiliano ya simu za mkononi ya Vodacom.

Akisoma hukumu hiyo leo April 11, 2019 na hakimu Huruma Shaidi alisema kitendo cha kuingilia masuala ya usalama ni hatari kwa nchi, hivyo mahakama imewatia hatiani washtakiwa hao kwa makosa tisa.

"Kitendo  walichofanya washtakiwa hawa cha kuingilia masuala ya usalama ni hatari kwa nchi, hivyo mahakama imewatia hatiani washtakiwa kwa makosa tisa," alisema hakimu Shaidi.

Hakimu Shaidi alisema katika kosa la kuingiza, kutumia na kusimika vifaa vya mawasiliano, pamoja kupiga simu nje ya nchi na kupokea bila kuwa na kibali cha TCRA linalowakabili washtakiwa wote, mahakama hiyo imewaamuru kulipa faini ya Sh5 milioni kila mmoja.

Kwa maana hiyo mahakama imewapiga faini ya jumla ya Sh120 milioni washtakiwa hao kwa pamoja..

Katika shtaka la kuisababishia Serikali hasara, Mahakama imeamuru washtakiwa kwa pamoja kuilipa fidia ya zaidi ya Sh5.89 bilioni baada ya kampuni za Vodacom na Inventure Mobile Tanzania Ltd / Tala Tanzania kukwepa kodi.

Alisema kama washtakiwa watashindwa kulipa fadia hiyo, watarudishwa mahakamani kwa ajili ya kuhukumiwa tena kwa mujibu wa sheria.

"Kama washtakiwa hawa watashindwa kulipa fidia ya zaidi ya Sh5.89 bilioni basi watarudishwa mahakamani hapa kwa ajili ya kuhukumiwa tena kama sheria inavyoelekeza," amesema Shaidi.

Awali, kabla ya kusomewa hukumu hiyo, washtakiwa hao  wamekiri mashtaka yao.

Soma zaidi>>Kigogo Vodacom, wenzake wakiri makosa

>> Bosi wa Vodacom Tanzania afikishwa mahakamani

Advertisement