Hukumu ya kifo mwalimu aliyeua mwanafunzi wake

Mwalimu wa Shule ya Msingi Kibeta, Respicius Mutazangira akiwa ameanguka na kupoteza fahamu kwenye kizimba cha Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa, mahakamani hapo jana. Picha na Phinias Bashaya

Muktasari:

  • Jaji atumia hoja 12 kujibu maswali yaliyojitokeza wakati wa usikilizaji wa kesi, huku akieleza namna mwalimu husika alivyopaswa kuzingatia mwongozo wa kiserikali wa kuadhibu mwanafunzi

Bukoba. Jaji wa Mahakama Kuu, Lameck Mlacha ametumia hoja 12 kujibu swali la mwalimu Respicius Mutazangira (51) aliyemuua mwanafunzi Sperius Eradius (13) wa Shule ya Msingi Kibeta na kumhukumu kunyongwa hadi kufa huku akimwachia huru mwalimu mwenzake Heriet Gerald (47).

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba huku ikishuhudiwa na umati wa watu uliokuwa na shauku ya kutaka kujua hatima ya kesi hiyo.

Jaji Mlacha alilazimika kutumia kipaza sauti kusoma hukumu hiyo, akilenga kila aliyekuwa eneo la Mahakama aweze kusikia alichokuwa akisema.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani mapema na walionekana kuzungumza na mawakili wao mara kwa mara kabla ya Mahakama kuanza.

Ndani na nje ya Mahakama kulikuwa na askari wengi waliokuwa na silaha za moto kwa lengo la kuimarisha ulinzi.

Mshtakiwa wa kwanza, Mutazangira kwa takriban dakika tatu alionekana akisoma Biblia, ambayo baadaye ilionekana imeshikiliwa muda wote na mshtakiwa wa pili, Heriet wakati hukumu ilipokuwa ikisomwa.

Jaji Mlacha aliingia kwenye ukumbi wa Mahakama saa 4:00 asubuhi na alisoma hukumu hiyo kwa dakika tano na baadaye upande wa Jamhuri na utetezi ulisema uko tayari kwa ajili ya hukumu.

Baada ya kusoma maelezo yaliyotolewa na mashahidi wa pande zote mbili, Jaji alizitaja hoja 12 alizozijibu zilizotolewa na mshtakiwa aliyemchapa fimbo Sperius na kusababisha kifo chake.

Alisema washtakiwa hawakukana kufahamu kuwa Sperius alichapwa fimbo.

Pia alisema hawakukana marehemu kukutwa na majeraha na hoja ya mwisho ilikuwa mshtakiwa wa kwanza hakukana kuwa ndiye alikutwa na Sperius njiani baada ya kuwa ameadhibiwa.

Jaji Mlacha alisema ushahidi wa kwanza uliungwa mkono na shahidi wa sita na wa nane kuwa mshtakiwa wa kwanza alimpiga mwanafunzi huyo huku akisema hakuna uthibitisho kuwa Heriet alimchapa baada ya mashahidi kugongana kwenye maelezo.

Mahakama pia ilizingatia ushahidi wa daktari bingwa wa magonjwa na vifo kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando, Kahima Jackson iliyoonyesha kuwa baada ya uchunguzi mwili ulikuwa na majeraha na kifo kilisababishwa na mshtuko wa moyo uliotokana na kipigo.

Pia, alirejea sheria na waraka wa elimu unaotoa maelekezo ya utoaji wa adhabu kwa mwanafunzi kuwa itumike fimbo nyepesi, izingatie umri, afya na viboko visizidi vinne ambavyo lazima viandikwe kwenye kitabu na mwalimu aliyetoa adhabu hiyo.

Washauri wawili wa Mahakama kati ya watatu walisema wamebaini washtakiwa wote wana hatia kwa kuwa walishiriki kusababisha kifo cha mwanafunzi huyo huku mshauri mmoja akimuondoa hatiani mshtakiwa wa pili ambaye aliachiwa huru.

Alisema mwalimu Mutazangira hakuwa na ruhusa ya kuadhibu na alitumia fimbo na baadaye kipande cha kuni kumpiga mara nyingi na kumsababishia majeraha akimuona mwanafunzi huyo kama jeuri na katiri.

Baada ya kauli hiyo, Jaji Mlacha alisema Mahakama inamtia hatiani mshtakiwa wa kwanza, Mutazangira na inamwachia huru Heriet kwa kutokuwa na hatia.

Hatua hiyo ilifuatiwa na sauti iliyotoka karibu na meza ya Jaji kutaka watu wote kusimama na baadaye Jaji Mlacha alihitimisha kwa kusema anamhukumu mshtakiwa wa kwanza adhabu moja tu ya kunyongwa hadi kufa. Baada ya kauli hiyo mshtakiwa alianguka kizimbani na watu kuombwa watoke nje.

Siku ya tukio

Mauaji hayo yalitokea Agosti 27, 2018 katika Shule ya Msingi Kibeta baada ya mwalimu Heriet kupotelewa na pochi na mwanafunzi huyo kutuhumiwa kuichukua kabla ya kukabidhiwa kwa Mutazangira ambaye alikuwa anasimamia nidhamu ya wanafunzi.

Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri ulileta mashahidi tisa wakiwemo walimu na wanafunzi ambapo Wakili wa Serikali Mkuu, Hashimu Ngole alisema kesi hiyo ilikuwa na masilahi ya umma ndio sababu ilipewa kipaumbele na kwamba hawana mpango wa kukata rufaa.

Wakili Aaron Kabunga aliyemtetea mshtakiwa wa kwanza ambaye aliachiwa huru alisema kuwa Mahakama imetekeleza wajibu wake na mshtakiwa wa kwanza amehukumiwa kadri ya kosa alilofanya.