Hukumu ya Sabaya yaahirishwa hadi Juni 10

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akishuka kwenye gari la Magereza leo Mei 31,2022 ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili yeye na wenzake sita. Picha na Janeth Mushi.

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeahirisha hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita kutokana na Hakimu kuwa na majukumu mengine.

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeahirisha hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita kutokana na Hakimu kuwa na majukumu mengine.

 Akiahirisha kesi hiyo leo Jumanne Mei 31, 2022, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Fadhil Mbelwa amesema shauri lilipangwa kwa ajili ya hukumu ila hakimu aliyekuwa akiisikiliza amepangiwa majukumu mengine ya kikazi nje ya ofisi.

"Shauri linakuja kwa ajili ya hukumu na liko kwa Hakimu Mkazi Mwandamizi, Patricia Kisinda lakini siku ya leo amepangiwa majukumu mengine ya kikazi nje ya ofisi hataweza kutoa hukumu leo hadi Juni 10, 2022," amesema Hakimu huyo

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021, mbali na Sabaya watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Leo Jamhuri iliwakilishwa na Mawakili wa Serikali waandamizi Janeth Sekule, Felix Kwetukia, Wakili wa Serikali Neema Mbwana na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Jacopiyo Richard.

Utetezi uliwakilishwa na Mawakili Mosses Mahuna, Fridolin Bwemelo, Edmund Ngemela na Sylvester Kahunduka ambao wanawatetea washitakiwa sita isipokuwa Mwahomange ambaye anajitetea mwenyewe mahakamani hapo.

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa matano, la kwanza wakidaiwa wote saba Januari 22,2021 kuongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha linawakabili washitakiwa wote saba wanadaiwa kupata Sh 90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis  Mrosso, huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.

Kosa la pili, tatu na nne Sabaya peke yake ameshitakiwa kwa makosa ya kujihusisha na rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh90 milioni na matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.