Prime
Huu hapa ujumbe wa Profesa Tibaijuka kwa Rais Samia sakata la Lissu
Muktasari:
- Ushauri huo alioutoa hauna tofauti na ule uliotolewa siku chache zilizopita na Jumuiya ya Madola baada ya kuipa Serikali ya Tanzania muda wa siku 30 kutafuta suluhisho la kisiasa na kisheria kuhusu kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema,Tundu Lissu.
Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe, Profesa Anna Tibaijuka, amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kutumia hekima, busara na kuzingatia sera ya 4R aliyoasisi ili kumuachia huru Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.
Amesema kuendelea kwa kesi hiyo, na simulizi zinazoripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa, kunazidi kuibua hisia tofauti miongoni mwa vijana na kuathiri taswira ya Tanzania pamoja na masilahi yake katika jumuiya ya kimataifa.
Ushauri huo alioutoa unaenda sambamba na ule uliotolewa siku chache na Jumuiya ya Madola baada ya kuipa Serikali ya Tanzania muda wa siku 30 kutafuta suluhisho la kisiasa na kisheria kuhusu kesi inayomkabili Tundu Lissu.
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa Julai 11, 2026, na aliyekuwa Rais wa Malawi na mjumbe maalumu wa Jumuiya ya Madola, Lazarus Chakwera, ambaye aliteuliwa kusuluhisha mivutano ya kisiasa na kuwezesha mazungumzo ya kitaifa kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 uliogubikwa na utata na kuzua maandamano.
Tundu Lissu alikamatwa baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika Mbinga, ambapo alitoa wito wa kufanyika kwa marekebisho ya mfumo wa uchaguzi na Katiba.
Serikali ilimfungulia mashtaka ya uhaini pamoja na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, ikidai kuwa kampeni yake ya "Hakuna Mabadiliko ya Sheria za Uchaguzi, Hakuna Uchaguzi" ilichochea uasi wa umma.
Leo Jumatatu, Julai 13, 2026, katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa X ukiambatana na video ya moja ya chombo cha habari cha kimataifa kikiangazia demokrasia na suala la Lissu na Profesa Tibaijuka akauweka ujumbe wake.
Profesa Tibaijuka ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Makazi (UN-HABITAT) ameandika: “Samia Suluhu Hassan, mheshimiwa Rais, naendelea kushauri kwa dhati Tundu Lissu aachiwe huru, kwani kesi haikamiliki.
"Hekima na busara iliyokufanya kutangaza sera ya 4Rs mara ulipoingia madarakani ikuongoze tena katika jambo hili. Simulizi hizi za kutisha za vyombo vya habari vya kimataifa zinaibua hisia kali, hasa kwa vijana. Hata wazee tumekumbushwa kadhia ya Operesheni Sogeza iliyounda vijiji vya ujamaa mwaka 1974 hadi 1976.
"Taarifa hizi zinaathiri kwa kiasi kikubwa taswira ya Taifa letu na masilahi yake. Athari ni kubwa. Tutafute muafaka kupitia uwajibikaji na maridhiano. Tuwe na hofu ya Mungu na kutambua miujiza yake, mfano wa risasi 16 kushindwa kukomesha uhai, ingawa maumivu ni makubwa. Tutubu na kusali kuliombea Taifa letu, kila mtu kwa imani yake.”
Hatua zilizowahi kuchukuliwa
Wakati mashinikizo ya kimataifa na wadau wa ndani yakiendelea kuhusu mwenendo wa demokrasia nchini, Serikali ya Tanzania imewahi kuchukua hatua mbalimbali za kisheria kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mahakama, hatua zilizotafsiriwa na baadhi ya wadau kuwa sehemu ya jitihada za kuimarisha maridhiano ya kisiasa.
Miongoni mwa hatua hizo ni kufutwa kwa kesi ya ugaidi iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, pamoja na wenzake. DPP aliondoa mashitaka hayo kwa kutumia mamlaka yake chini ya kifungu kinachoruhusu kuondoa mashitaka na hivyo Mbowe na wenzake wakaachiwa huru.
Mbali na hatua hizo za kisheria, mwaka 2022 Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chadema zilianza mazungumzo ya maridhiano yaliyolenga kupunguza mvutano wa kisiasa nchini.
Hata hivyo, mazungumzo hayo hayakufikia tamati baada ya kila upande kuutuhumu mwenzake kwa kusababisha kuvunjika kwake.
Pamoja na kutofikia makubaliano ya mwisho, baadhi ya hoja zilizowasilishwa na Chadema zilifanyiwa kazi. Kati ya hoja 11 zilizowasilishwa mezani, tisa zilipatiwa ufumbuzi.
Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kufutwa kwa zaidi ya kesi 400 zilizokuwa zinawakabili wanachama na viongozi 77wa Chadema, kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, viongozi wa chama waliokuwa wamekimbilia nje ya nchi kuhimizwa kurejea na kuhakikishiwa usalama wao, pamoja na kulipwa kwa malimbikizo ya ruzuku ya chama kwa kipindi cha miaka mitatu, yaliyofikia Sh2.7 bilioni.
Akizungumza na wanachama wa CCM jijini Dar es Salaam Februari 4, 2024, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, alisema mazungumzo hayo, yaliyodumu kwa takribani mwaka mmoja tangu yalipoanza Mei 2022, yalikwama kutokana na sababu mbili.
Kwa mujibu wa Kinana, sababu hizo ni Chadema kuendelea kuwashambulia na kuwatukana viongozi wa CCM katika mikutano ya hadhara, pamoja na kupeleka malalamiko yao katika kila kikao cha mazungumzo.
"Tuliwasihi wenzetu kwamba mikutano ya hadhara imeanza, tafadhali tusitumie mikutano hiyo kukashifiana, kutukanana na kudhalilishana, hasa kumdhalilisha kiongozi wa nchi. Hatukuomba jambo kubwa; wakosoe Serikali, waeleze mapungufu ya CCM, lakini si kutukana viongozi," alisema Kinana.
Alichokisema Profesa Bana
Mchambuzi wa masuala ya siasa na diplomasia, Profesa Benson Banna, amesema Jumuiya ya Madola si taasisi ya kutoa shinikizo, bali ni chombo cha kidiplomasia kinachotoa ushauri, ingawa wakati mwingine hutumia lugha yenye msisitizo.
"Nafikiri Rais ana vyombo vingi vya kumshauri ndani ya nchi. Ni muhimu apewe muda wa kutafakari na kupima mambo. Ni vyema tumuachie uhuru wa kufanya uamuzi anaouona unafaa. Ushauri unaotolewa unapaswa kuzingatiwa na kufanyiwa kazi," amesema Profesa Banna.
Amesema Rais anatambua hali inayoendelea si nzuri kwa mustakabali wa siasa nchini, na amepokea ushauri mbalimbali, ikiwemo ule wa Jumuiya ya Madola. Kwa maoni yake, Rais atafanya uamuzi kuhusu ama kumwachia huru Lissu au kuiruhusu kesi hiyo iendelee hadi itakapofikia mwisho.
Profesa Banna amesema Tanzania ilijiunga na Jumuiya ya Madola kwa hiari, hivyo ushauri unaotolewa na jumuiya hiyo unapaswa kupewa uzito kwani kuna baadhi ya nchi ambazo zimewahi kukumbana na hatua mbalimbali baada ya kushindwa kutekeleza ushauri wa jumuiya hiyo.
"Kuna nchi zilizowahi kupata madhara, ikiwemo Zimbabwe, Nigeria na nyingine ambazo sizikumbuki kwa sasa. Baadhi yao waliwahi kusimamishwa uanachama ili kuzipa nafasi ya kujipanga upya na kurekebisha mambo ambayo Jumuiya ya Madola iliona hayakuwa yanaendana na misingi yake na taratibu zake," amesema.
Koga: Tanzania si kisiwa
Mchambuzi wa masuala ya diplomasia, Denis Konga, amesema ni jambo la busara kumwachia huru Lissu ili kuweka msingi imara wa demokrasia, kwani mtu hawezi kushiriki katika ujenzi wa taifa au mchakato wa maridhiano akiwa gerezani.
Konga amesema sauti za wadau mbalimbali pamoja na jumuiya za kimataifa zina uzito mkubwa haziwezi kupuuzwa kwani Tanzania si kisiwa na haiwezi kujitenga na mataifa mengine.
"Sauti hizi za wadau na jumuiya za kimataifa zina maana. Tanzania si kisiwa; hatuwezi kujitenga. Hatuwezi kufanikiwa bila kuzingatia jinsi wenzetu wanavyotuona. Lazima tuangalie wanatutazamaje," amesema.
Amesema ni muhimu Tanzania kuzingatia ushauri wa Jumuiya ya Madola ili kuepuka kutengwa katika shughuli za biashara, akieleza Uingereza ni taifa kubwa na mshirika muhimu wa maendeleo pamoja na ushawishi wake katika Siasa za dunia.