Huu ndio utajiri wa gesi Tanzania

Muktasari:

Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema tangu kuanza uzalishaji Julai 2004 hadi Januari 2024, kiasi kilichotumika ni futi za ujazo bilioni 700 kati ya trilioni 57 zilizogundulika.


Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema tangu kuanza uzalishaji wa gesi Julai 2004 hadi Januari 2024, kiasi kilichotumika ni futi za ujazo bilioni 700 kati ya trilioni 57 iliyogundulika. 

Kiwango hicho cha gesi kinatumika katika viwanda vinavyotumia nishati ya gesi vimefikia 53, magari ya kutumia mfumo wa nishati ya gesi 3,400, mchango wa zaidi ya asilimia 70 ya uzalishaji umeme, kaya zaidi ya 1,500 zinazotumia gesi ya kupikia pamoja na taasisi 13 ikiwamo magereza, vyuo na hoteli.

Aidha, gesi iliyotumika imewezesha kuokoa zaidi ya dola 17 bilioni sawa na Sh40 trilioni ambazo zingetumika kuagiza mafuta nje kwa ajili ya matumizi ya ndani kati ya mwaka 2004 hadi mwaka jana.

“Kiwango hicho ni sawa na wastani wa futi za ujazo bilioni 35 kila mwaka. Maana yake gesi bado ni nyingi na kasi ni ndogo sana ya matumizi kwa mwenendo huo,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni alipoulizwa kuhusu mwenendo wa matumizi leo Januari 8, 2024.

“Ndio maana Serikali imeongeza kasi katika hatua za utekelezaji wa mradi kusindika gesi ya kimiminika (LNG) ili kwenda na kasi ya mabadiliko ya kidunia, mwaka 2050 dunia inataka kufikia Net zero (Uwezo mkubwa wa kuzalishaji hewa safi kuliko hewa chafu).”

Hata hivyo, kwa mujibu wa Ripoti ya Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia Tanzania 2016-2045, Serikali imetenga futi za ujazo trillioni 8.8 za gesi kwenye umeme, futi za ujazo bilioni 500 kwenye kaya, futi za ujazo trilioni 3.6 kwenye viwanda na futi za ujazo bilioni 600 kwa magari.