Huyu ndiye Daniel Chongolo

Huyu ndiye Daniel Chongolo

Muktasari:

  • Hatimaye  Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imejaza nafasi ya ukatibu mkuu iliyoachwa tangu Machi 26, mwaka huu, kwa kumteua Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Dar es Salaam. Hatimaye  Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imejaza nafasi ya ukatibu mkuu iliyoachwa tangu Machi 26, mwaka huu, kwa kumteua Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Nafasi hiyo iliachwa wazi baada ya aliyekuwa akiishikilia, Dk Bashiru Ally, kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Nyota ya Chongolo kupanda kisiasa ilianza kuonekana zaidi tangu Juni 27, 2016 wakati Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli, alipowateua wakuu 100 wa wilaya na kuwafukuza kazi wakuu wawili wa mikoa.

Katika uteuzi huo Chongolo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido. Katika uteuzi huo, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anna Kilango Malecela na mwenzake wa Mara, Magesa Mulongo walifutwa kazi. Julai 28, 2018, Chongolo alihamishwa kutoka Wilaya ya Longido kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Rais Magufuli kufanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala, makatibu wakuu na manaibu wao, akiteua wanasiasa waliotokea vyama vya upinzani, mshiriki wa shindano la urembo na makada wa CCM.

Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya  Kinondoni, Ally Hapi, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Agosti 11, 2018, Chongolo aliwaaga rasmi watumishi wa Longido na kuwakabidhi kwa mkuu wa wilaya mpya ya Longido, Frank Mwaisumbe.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Chongolo alisema anawaamini watumishi wa Longido na kwamba, hakuwa na shaka nao kuwa ni wachapa kazi na wamekuwa msaada mkubwa kwake kwani bila wao asingeweza kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Akiwa Kinondoni, Novemba 6, 2018 Chongolo aliiagiza Polisi Kata ya Kijitonyama kuwakamata wanaume wanaonunua machangudoa.

Chongolo alitoa agizo hilo kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Kijitonyama, Said Lujuo, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Kisiwani.

Kauli hiyo ya Chongolo aliitoa baada ya mkazi mmoja wa Mtaa wa Nzasa kulalamikia suala la biashara ya ukahaba kukithiri kwenye mtaa anaoishi.

 Septemba 22, 2019, aliunda kamati ya watu sita kuchunguza tukio la ajali ya moto uliotekeleza Hoteli ya Coco Beach.

 Hoteli hiyo ilianza kuteketea kwa moto saa 7:30 mchana wa Jumapili ya Septemba 22, 2019 ambapo mmiliki wa hoteli hiyo, Alphonce Buhatwa, alisema asilimia 80 ya mali zote katika hotel hiyo zimeteketea. Novemba 9, 2019, alitekeleza agizo la Rais John Magufuli, la kumrudishia nyumba bibi mwenye umri miaka 80, Amina Muhenga, aliyoidai zaidi ya miaka 30.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo miezi miwili iliyokuwa imepita. Januari 17, 2020, Chongolo alipiga marufuku wanafunzi walioanza kidato cha kwanza mwaka huo kurudishwa nyumbani kwa sababu ya kutokuwa na sare za shule.

Alitoa agizo hilo katika hafla ya kuzipongeza shule na walimu waliofanya vizuri katika mitihani ya darasa la saba mwaka 2019 wilayani humo. Chongolo alitoa agizo hilo baada ya kupata taarifa kuwa baadhi ya maeneo wanafunzi hawapokelewi kwa sababu ya kutokuwa na sare.

“Jambo la msingi kwa mwanafunzi ni kuripoti shule na kuwa na daftari na vifaa vya kujifunzia, sijui hana sare, viatu au jembe, hicho si kigezo cha kutompokea.” Februari 25, 2020, alisema wilaya yake ilitenga Sh3.4 bilioni kwa ajili ya kuwakopesha wanawake, vijana na wenye ulemavu katika bajeti ya mwaka 2020/21.

Januari 10, 2021, alifanya operesheni maalum iliyofichua nyumba zinazohifadhi watu wenye ulemavu wanaotumika kuomba jijini Dar es Salaam. Aprili 1, 2021, alitoa siku 21 kwa wataalamu wa Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka (Dawasa) kwenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Kata ya Mbezi Juu.

Alitoa kauli hiyo baada ya kusikiliza kero zinazowakabili wakazi wa eneo hilo. Hatimaye jana, Halmashauri Kuu ya CCM imemteua kuwa katibu mkuu.

Kikao hicho pia kimemteua Christina Mndeme kuwa naibu katibu mkuu Bara huku Abdallah Juma Sadala akiendelea kuhudumu nafasi hiyo upande wa Zanzibar.

Itakumbukwa kuwa wakati Dk Bashiru anateuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, alikuwa Katibu Mkuu wa CCM, nafasi aliyoihudu[1]mu kwa kipindi cha miaka miwili na miezi minane. Alipendekezwa na Dk Magufuli Mei 29, 2018 na kuthibitishwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu iliyo[1]kutana Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aliteuliwa kushika wadhifa huo akiwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuchukua nafasi ya Abdulrahman Kinana aliyekuwa amestaafu. Kwa wadhifa wake wa sasa, Chon[1]golo anakuwa Katibu Mkuu wa kumi wa CCM tangu kilipozaliwa Februari 5, 1977.

Kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya, Chongolo amewahi kuwa Ofisa wa chama kwenye Idara ya Uenezi makao makuu wakati huo Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi akiwa Nape Nnauye. Pia, amewahi kuwa Mhariri wa Redio Uhuru ambayo inamilikiwa na CCM.

Kwa nyakati tofauti, Chongolo pia amewahi kuwa Katibu wa Bodi ya Shirika la Magazeti ya Chama (Uhuru na Mzalendo).