IAA yafungua dawati la jinsia, wanafunzi waaswa

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Profesa Eliamani Sedoyeka

Arusha. Wanafunzi vyuoni wameaswa kujiepusha na vitendo vya matumizi ya vilevi kwani vinachangia kwa kiasi kikubwa kufanyika kwa ukatili wa kijinsia.

Hayo yamesemwa leo Juni 20, 2023 jijini Arusha na Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Sedoyeka wakati akizindua rasmi dawati la jinsia chuoni hapo.

Aidha Profesa Sedoyeka amesema wanafunzi wengi wamekuwa wakijiingiza kwenye matumizi ya vilevi hali inayowapelekea kujikuta wakijiingiza kwenye matukio ya ukatili wa kijinsia na kuwapotezea  malengo yao.

Amesema kuzinduliwa kwa dawati hilo chuoni hapo kutaleta manufaa makubwa sana kwani wanafunzi watapata sehemu maalumu ya kuweza kuelezea changamoto zao wanazokutana nazo pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili.

Wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha

"Wanafunzi napenda kuwaasa muepukane na vitendo viovu ikiwemo matumizi ya vilevi ambavyo matokeo yake inapelekea kujiingiza kwenye matukio ya ukatili na mwishowe  kukatisha ndoto zenu mlizojiwekea  nawaombeni sana mkalenge  kwenye kufikia malengo yenu  kwani starehe  hizo  zipo tu mtazikuta ila kwa sasa fanyeni  yaliyowaleta hapa chuoni," amesema Profesa Sedoyeka.

Aidha kauli mbiu katika uzinduzi huo ni; ‘IAA bila ukatili wa kijinsia inawezekana’ ambapo aliwataka wanafunzi hao kukitumia kituo hicho kuripoti matukio ya ukatili wanayofanyiwa au kuyaona katika maeneo yao.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii jiji la Arusha, Habiba Madebe amesema kuna aina mbalimbali za ukatili zinazofanyika kwenye jamii ila zimekuwa haziripotiwi zote kutokana na asilimia kubwa ya jamii kutojua sehemu sahihi ya kuripoti matukio hayo hivyo kuwataka wanafunzi hao kutumia dawati hilo kuripoti matukio mbalimbali .

Mwakilishi wa wanafunzi katika dawati la jinsia IAA, Ophen Felician amesema dhumuni la kuanzishwa kwa dawati hilo ni ili kuhakikisha chuo hicho kinakuwa sehemu salama kwa wanafunzi, wafanyakazi na watoa huduma wote.

Amesema pamoja na masuala yote ya ukatili wa kijinsia, dawati litakuwa  linapokea na kushughulikia taarifa zote za ukatili wa kijinsia, kutoa ushauri nasaha na kuwalinda wahanga wa ukatili wa kijinsia.

Aidha amesema kupitia dawati hilo watakuwa wanatoa  elimu kwa wana IAA kuhusu ukatili wa kijinsia ikiwa ni  pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.