IAA yazindua kamati ya ushauri wa kisekta, lengo kuboresha mitaala

Arusha. Chuo cha Uhasibu Arusha (IIA) kimezindua kamati ya ushauri wa kisekta (Industrial Advisory Committee) itakayoboresha mitaala sambamba na kuleta mabadiliko makubwa katika kuzalisha wataalamu bobezi katika fani mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo.
Akizingumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho, Dk Mwamini Tulli amesema kamati hiyo ndiyo itakayokua mshauri na kiunganishi kikubwa katika kuhuisha mitaala iliyopo, na kuandaa mitaala mipya ili wataalamu wanaosoma fani mbalimbali chuoni hapo waweze kutoa usuluhishi katika changamoto za kisekta.
Dk Tulli amesema kamati hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa HEET wenye lengo la kujenga daraja la kudumu kati ya chuo hicho na wadau hao katika sekta mbalimbali ambazo zitapokea watalaamu wanaoandaliwa katika fani mbalimbali zikiwemo uhasibu na fedha, benki, uchumi, kodi, Tehama utalii usimamizi wa biashara pamoja na ukaguzi wa fedha.
"Kamati hii ni muhimu sana kwetu Sisi katika kutushauri na kutuongoza kuhusu jinsi tunavyoweza kutoa elimu inayokidhi mahitaji ya soko la ajira na kamati hiyo itakuwa jukwaa la majadiliano, mawazo na ubunifu unaolenga kuboresha programu za masomo na kuweka mwelekeo sahihi," amesema Dk Tulli
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo IAA, Profesa Eliamani Sedoyeka amesema chuo kitaendelea kufanya tafiti na mabadiliko ya mitaala ili kuendana na ukuaji wa Sayansi na Teknolojia nchini na kutoa wataalamu bobezi.
Profesa Sedoyeka amesema tukio hilo ni moja kati ya majukumu ya msingi kwani chuo hicho kina wajibu wa kutoa mafunzo,ushauri wa kitaaluma na kufanya tafiti hivyo majukumu hayo hayawezi kuwa na uhalisia na kwenda kutoa majawabu katika maeneo mbalimbali bila ya kuwa na muongozo dhabiti wa kufanya hivyo na kamati hiyo ndo itakuwa kiunganishi kikubwa kati ya wao chuo na sekta mbalimbali.
"Na tunategemea baada ya bodi hiyo kuanza kufanya kazi itatupa mrejesho na miongozo ambayo itawasaidia wao kuweza kufanya kazi vizuri zaidi katika kuboresha mitaala mbalimbali ambayo itaendana na soko la ajira," amesema
Aidha amefafanua, chuo hicho ni kati ya vyuo ambavyo vimeweza kupata mradi wa HEET na wameshaanza kupokea dola 21 milioni, hivyo wanamshukuru Rais Samia Hassan kuona umuhimu wa kuwapatia mradi huo.
"Sisi kama chuo tunahitaji kutoa watu wanaoendana na mahitaji ya sasa na uzinduzi wa kamati hii ndo inaenda kujibu mahitaji hayo kwani wengi wa wajumbe wa kamati hiyo wanatoka maeneo mbalimbali ambayo kila mmoja kwa nafasi yake ataleta mchango pekee katika nafasi zao," amesema Profesa Sedoyeka
Nao Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo Elias Kajiba kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Liliani Riwa wamesema kwa pamoja watahakikisha wanatekeleza majukumu ya chuo hicho kwa kutoa ushauri na hatimaye kuweza kutoa late wanaokidhi soko la ajira na kuweza kuajirika kwa urahisi.