IEBC yapunguza kura 10,000 za Ruto

Muktasari:

  • Wakati Wakenya wakisubiri kwa hamu kutangazwa kwa matokeo ya kura za urais, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Kenya (IEBC) imerekebisha matokeo ya kura za urais kwenye jimbo la Kiambui kutoka kwenye fomu 34B, mabadiliko hayo yamepunguza idadi ya kura za mgombea wa tiketi ya Kenya Kwanza William Ruto.


Nairobi. Wakati Wakenya wakisubiri kwa hamu kutangazwa kwa matokeo ya kura za urais, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Kenya (IEBC) imerekebisha matokeo ya kura za urais kwenye jimbo la Kiambui kutoka kwenye fomu 34B, mabadiliko hayo yamepunguza idadi ya kura za mgombea wa tiketi ya Kenya Kwanza William Ruto.

Kenya ilifanya Uchaguzi Mkuu, Agosti 9, 2022 na katika matokeo ya awali kwenye jimbo hilo, IEBC ilionyesha kwamba Naibu Rais Ruto amepata kura 51,050 kabla ya baadaye kusahihisha  idadi hiyo hadi kufikia kura 41,050.

Masahihisho hayo yanatokea siku moja tangu ugomvi uibuke kwenye kituo kikuu cha kuhesabia kura na kutangazia matokeo ya urais cha Bomas ambapo mawakala wa kambi ya Azimio la Umoja anakotokea Raila Odinga kuwashutumu mawakala wa Kenya Kwanza kuingilia mfumo wa matokeo wa IEBC na kuongeza kura kwa Ruto.

Hata hivyo mpaka sasa kambi ya Ruto haijatoa kauli yoyote juu ya uamuzi wa IEBC ambao unaweza kuathiri matokeo ya mwisho.

Tayari kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya kambi ya Ruto na Odinga juu ya matokeo ya urais ambapo kila kambi inajinasibu kushinda huku ikieleza kuwa wanasubiri tangazo la IEBC.

Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo matokeo ya nafasi ya urais yanatangazwa ndani ya siku saba tangu kura zipigwe.