Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ifahamu programu mpya kupima masikio kupitia kishkwambi

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa WHO, watu zaidi ya bilioni 1.5 duniani wanaishi na changamoto za usikivu.

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limezindua programu mpya ijulikanayo kama WHOears, inayolenga kurahisisha upimaji wa usikivu wa masikio kupitia kishkwambi (tablets), hatua inayotarajiwa kusaidia kubaini mapema matatizo ya kusikia kwa mamilioni ya watu duniani.

Programu hiyo, ambayo inapatikana bila malipo katika mifumo ya Android na iOS, imeundwa kutumiwa na wahudumu wa afya waliopatiwa mafunzo katika vituo vya afya vya msingi na maeneo ya jamii.

Kupitia kishkwambi, muhudumu wa afya anaweza kufanya uchunguzi wa awali wa uwezo wa kusikia kwa mtu mwenye umri wa miaka mitano na kuendelea.

Tofauti na vipimo vya kina vya kitabibu, WHOears hutumika kama chombo cha uchunguzi wa awali. Programu hiyo hutoa maelekezo ya hatua kwa hatua kwa muhudumu wa afya na baada ya kipimo kutoa matokeo yanayoonyesha kama mtu amefaulu uchunguzi au anahitaji uchunguzi zaidi.

Kwa mujibu wa WHO, watu zaidi ya bilioni 1.5 duniani wanaishi na changamoto za usikivu, huku wengi wao wakikosa huduma za uchunguzi wa mapema kutokana na ukosefu wa vifaa na wataalamu wa kutosha. Hali hiyo imeifanya taasisi hiyo kuja na suluhisho la kidijitali linaloweza kutumika hata katika maeneo yenye rasilimali chache. 

Faida nyingine ya programu hiyo ni uwezo wake wa kutambua kiwango cha kelele katika mazingira ya upimaji. Endapo eneo lina kelele nyingi zinazoweza kuathiri usahihi wa matokeo, programu humjulisha mtumiaji kutafuta sehemu tulivu zaidi kabla ya kuendelea na uchunguzi.

WHO imesisitiza WHOears si mbadala wa uchunguzi rasmi wa kitabibu, bali ni nyenzo ya kusaidia kubaini mapema watu wanaoweza kuwa na changamoto za usikivu ili waweze kupata huduma stahiki kwa wakati.

Uzinduzi wa programu hiyo ulifanyika mwanzoni mwa Juni, 2026 kupitia mkutano wa kimataifa wa mtandaoni uliowakutanisha wataalamu wa afya, watafiti na watunga sera kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Wataalamu wa afya wanaamini matumizi ya teknolojia kama WHOears yanaweza kusaidia kupunguza idadi ya watu wanaoishi na matatizo ya usikivu bila kuyafahamu, hususan watoto wa shule na wanaofanya kazi katika mazingira yenye kelele nyingi.