IGP Wambura asisitiza huduma bora zahanati za Jeshi la Polisi

 Jeshi la Polisi likipokea maelezo ya msaada wa vifaatiba vilivyotolewa.

Muktasari:

 Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS Ltd) msaada wa vifaatiba vyenye thamani ya Sh235 milioni kwa Jeshi la Polisi

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura amesema utoaji huduma bora kwenye hospitali  na zahanati za taasisi hiyo ni muhimu kwa jamii inayowazunguka  ili kujenga uhusiano mzuri na wananchi.

Akizungumza leo Jumatatu Aprili 22 2024 wakati akipokea msaada wa vifaatiba vyenye thamani ya Sh235 milioni kutoka Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS Ltd) Dar es Salaam, Wambura amesema jambo hilo likifanyiwa kazi itakuwa rahisi wanaposhirikishwa kukabiliana na uhalifu.

“Napenda kuueleza uongozi na wataalamu wa hospitali na zahanati zetu zote tunazohudumia raia,  suala la huduma bora kwa mteja linapaswa kuzingatiwa kwani hapo ndipo tunajenga uhusiano mzuri kati yetu sisi na raia,” amesema Wambura.

Amesema mageuzi wanayoendelea kuyajenga ndani ya jeshi hilo kwa sasa ni kuona wanashirikiana na kufanya kazi  na raia vizuri kwa kutambua wana jukumu la pamoja la kulinda usalama wa wananchi na mali zao.

Akizungumzia msaada huo, Wambura amesema vifaatiba bei yake ni ghali duniani kote, hivyo ni wajibu kwa wataalamu katika zahanati na hospitali kuvitunza vidumu kwa muda mrefu.

“Tunakishukuru chama chetu cha Ura kwa msaada huu, msichoke kusaidia pale uwezo wenu unaporuhusu ubora wa huduma za kitabibu unategemea uwepo wa vifaatiba bora na vya kisasa,” amesema Wambura.

Awali, katika tukio hilo, Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu na Mwenyekiti wa Bodi ya URA SACCOS, Suzan Kaganda amesema wameweka utaratibu wa kutenga fedha kutokana na ziada inayopatikana na kuirudisha kwa jamii kwa mujibu wa  sheria na kanuni za kiushirika.

Kaganda amesema kuanzia mwaka 2017 ulipoanza utaratibu huo, chama hicho cha ushirika kimeshatoa kwa jamii vifaatiba vyenye thamani ya Sh581 milioni.

"Ushirika unaamini huduma ya hospitali sio tu inawanufaisha askari, lakini jamii ya Watanzania wanaohudumiwa kwenye hospitali zetu. Hivyo, kuleta maana halisi ya kurudisha kwa jamii na kuihudumia kupitia vifaatiba,” amesema Kaganda.

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dar es Salaam, Anjela Nalimi amesema msaada huo uwe chachu kwa vyama vingine vya ushirika kuiga kwa kutumia sehemu za fedha za ziada kuijali jamii.

Msaada huo unajumuisha mashine ya X-Ray ya kisasa, vifaa vya maabara, vifaa mbalimbali vya mazoezi tiba na vifaa vya wodini vya kulazia wagonjwa.

Vifaatiba hivyo vinakwenda kutumika katika Hospitali ya Rufaa ya Kilwa Road na zahanati sita za polisi ikiwamo zahanati ya Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Zahanati ya Shule ya Polisi Moshi, Zahanati ya Polisi Mkoa wa  Mtwara, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Tanga, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Dodoma na Zahanati ya Polisi Mkoa Kaskazini Pemba.