Wanakijiji 3, 000 wapigwa jeki ujenzi wa zahanati

Zahanati ya kijiji cha Katembe kata ya Nyakabango wilayani Mleba iliyojengwa na Hifadhi ya Taifa ya Rubondo. Picha na Suzy Butondo

Muktasari:

Kabla ya ujenzi wa zahanati hiyo, wanakijiji hao walienda kutibiwa Muleba, Rubya, Kaigara  na Mugana umbali wa zaidi ya kilomita tano.

Muleba. Zaidi ya wakazi 3, 000 wa kijiji cha Katembe Wilaya ya Muleba mkoani Kagera wameondokana na changamoto ya kutembea kilomita tano kufuata huduma za afya baada ya Hifadhi ya Taifa Rubondo kuwajengea zahanati kwa gharama ya Sh10 milioni.

Kabla ya ujenzi wa zahanati hiyo, wanakijiji hao walienda kutibiwa Muleba, Rubya, Kaigara  na Mugana umbali wa zaidi ya kilomita tano.

Wakizungumza na waandishi wa habari Novemba 21, 2023 waliotembelea zahanati hiyo, wananchi hao wameishukuru hifadhi hiyo wakidai zahanati iliyojengwa imeepusha vifo vilivyotokana na kuchelewa kupata huduma za afya.

"Kwa kweli zahanati hii imetusaidia sana hivyo jukumu letu ni kuitunza miundombinu yake ili iweze kudumu kwa muda mrefu, kizazi na kizazi kikute huduma hizi zikiendelea,”amesema Clementina Richard Mkazi wa Kijij hicho.

Diwani wa Kata ya Nyakabango, Castory Wanchele amesema hifadhi hiyo imekuwa msaada kwa wananchi akidai awali wajawazito walipata shida ya kupata huduma, hali ambayo ilisababisha wengi wao kujifungulia njiani na wengine kupoteza watoto.

"Kutokana na huduma wanazotoa kwa jamii na sisi tumeahidi kutoa ushirikiano, pale wanapopita majangili kufanya hujuma kwenye hifadhi hiyo tutawasaka na kuwakamata  waweze kuchukuliwa hatua madhubuti  kwa sababu hawatakiwi kuvamia katika hifadhi hii,"amesema Wanchele

Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Abela Oscar ameishukuru Serikali na wafadhili kwa kuwajengea jengo la mama na mtoto ambalo linapokea wagonjwa wa nje kati ya 75 hadi 146.

“Tunashukuru sana kwa kujengwa zahanati hii. Tunaiomba hifadhi na Serikali iendelee kutusaidia kwani tunahitaji maji ili wagonjwa na wazazi wasipate shida kwani  kuna wakati inalazimika ndugu wa mgonjwa aje na maji  kwenye ndoo,”amesema

Ofisa Uhusiano wa Jamii wa hifadhi hiyo ambaye pia ni Mtaalamu wa Utalii na Ikolojia, Robart Mushi amesema pamoja na kuwajengea zahanati,  hifadhi hiyo iliweka vifaa tiba akiahidi kuimarisha ukaribu kati ya hifadhi na wananchi hao.

Naye Mhifadhi Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu, Anold Mwasuluka amewaomba watumishi wa zahanati hiyo kutunza vifaa tiba vilivyopelekwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu.