Wanakijiji wakumbushia ahadi ya mbunge wao kukamilisha zahanati

Muonekano wa jengo la Zahanati ya Kijiji cha Ikungumhulu Kata ya Shilalo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza ambayo ujenzi wake umesimama miaka mitatu bila kukamilika. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Wananchi wa Kijiji cha Ikungumhulu Kata ya Shilalo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wamemuomba Mbunge wao,  Alexander Mnyeti kutimiza ahadi yake ya kuwakamilishia ujenzi wa zahanati.

Mwanza. Wananchi wa Kijiji cha Ikungumhulu Kata ya Shilalo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wamemuomba Mbunge wao,  Alexander Mnyeti kutimiza ahadi yake ya kuwakamilishia ujenzi wa zahanati.

Ombi hilo ni baada ya ujenzi wa zahanati hiyo kukwama kwa miaka mitatu katika hatua ya lenta hali iliyopelekea Mbunge wa Jimbo hilo kutoa ahadi ya kukamilisha ujenzi huo katika moja ya mkutano wa hadhara aliyoufanya kijijini hapo mwaka 2022.

Wakizungumza na Mwananchi Digital hivi karibuni, wanakijiji hao pia wameiomba Serikali kuingilia kati kwa kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo ili kuwaondolea changamoto ya kwenda kutafuta huduma katika vijiji na kata zingine.

"Imeonekana kwamba hatuna uongozi ndio maana maendeleo yamesimama kwa mfano tuna zahanati hapa lakini alikuja Mbunge akatuambia wananchi tulieni tusubiri tu kwenda kutibiwa muda umeenda mno na Zahanati yetu imebaki tu imetulia bila kuendelezwa,"amesema Sylivester Manhyakenda, mkazi wa kijiji hicho.

Katibu Mkuu kikosi cha Sungusungu kijijini hapo, Sophia Simon ameiomba Serikali kuingilia kati kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo ili wananchi waanze kunufaika nayo.

"Tunaomba Mbunge na Serikali yetu tusaidie wananchi sisi nguvu zetu ziliishia hapo ahadi tuliyoahidiwa mpaka sasa kimya kwa sasa tunalazimika kwenye Zahanati za vijiji jirani vinavyotuzunguka kama Buhingo, Mwambuku na Shiwhuji tunaenda na ukiangalia katika kata yetu tuna zahanati mbili na ya tatu ndio hii ambayo bado haijakamilika,"amesema Sophia

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikungumhulu, Bumeme Kasubi alipofuatwa na Mwananchi ili azungumzie suala la ujenzi wa zahanati hiyo ilikataa kuzungumzia akidai hana muda.

"Sina muda kwa kweli," amesema Kasubi alivyotafutwa na mwandishi wa habari hii kuzungumzia zahanati hiyo.

Katibu wa Mbunge wa Jimbo hilo, Emmanuel Lyandi japo kuwa hajataka kuongelea suala hilo huku akisema ni vyema Mnyeti akizungumzia amesema jambo analolifahamu fedha tayari zilishaombwa na mchakato wa ujenzi muda wowote utaanza.

"Nadhani jambo hilo ni la kuongea na yeye moja kwa moja kwa sababu ninachokijua fedha alishaomba mahali panapo husika wakamruhusu sasa haijajulikana mambo yanakuwa namna gani kwahiyo hilo siwezi kulisemea sana lakini nina uhakika muda wowote fedha zitakapofika shughuli itafanyika na sio Ikungumhulu tu na maeneo mengine," amesema Lyandi

Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Alexander Mnyeti alipotafutwa hakupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi uliotumwa kwa njia ya kawaida ya simu na kwa njia ya Whasapp.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha amekana kuitambua Zahanati hiyo huku akidai kuwa itakuwa haipo kwenye mfumo au kutambuliwa na Serikali.

"Siijui hiyo Zahanati unayo niuliza kwa sababu zote zinazojengwa kwa utaratibu hamna inayobaki kwa muda huo sasa kama ilijengwa pasipo utaratibu au kukidhi viwango vya zahanati inawezekana ndio maana haijaendelezwa na kama ina miaka mitatu mimi sikuwepo kwa hiyo siwezi kuijua," amesema

"Kama imejengwa kwa nguvu za wananchi huwa kuna utaratibu wa kujenga inafuata michoro ya zahanati, Halmashauri inakuwa Inajua ikifika hatua fulani inaendeleza sasa kama mtu anaweza kujenga tu halafu anasema ni nguvu ya wananchi, kiukweli sijui kwa sababu zote zinazojengwa kwa nguvu za wananchi kwa utaratibu ikifika lenta au wakimaliza boma Serikali inaendeleza," amesema Chacha

Kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Kata ya Shilalo ina jumla ya wakazi 17,606 huku zahanati zikiwa mbili katika vijiji viwili.